Unknown Unknown Author
Title: MASTAA KWA HIKI MLICHOKIFANYA TUNAKIITA NI UNAFKI WA KUPITILIZA, SOMENI HAPA
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
NAJUA bado kuna baadhi yenu mastaa wa Kibongo mna maumivu. Ni kweli mmempoteza mfalme wa freestyle Afrika, Albert Keneth Mangweha ‘Ngwea’....
NAJUA bado kuna baadhi yenu mastaa wa Kibongo mna maumivu. Ni kweli mmempoteza mfalme wa freestyle Afrika, Albert Keneth Mangweha ‘Ngwea’. Pole ziwafikie mastaa wote na mashabiki wake kwa jumla yenu.
Wiki iliyopita mastaa mlijitahidi kujitokeza kwenye msiba. Kuna niliowaona uwanja wa ndege, Viwanja vya Leaders na kule mkoani Morogoro.
Baada ya kutokea kwa tatizo baadhi yenu mlitumia nafasi hiyo ili nanyi mjulikane mpo. Hata wale wabaguzi wasiofika kwenye misiba ya wengine, nao walijitokeza na kumwaga sifa kemkemu.
Kila mmoja wenu alikuwa akisema lake ilimradi tu apate ‘kick’ kwenye vyombo vya habari.
Maajabu kila mtu alikuwa akidai kuwa aliwasiliana na Ngwea muda mfupi au saa kadhaa kabla ya kukutwa na umauti.
Kuna aliyeniambia alikuwa anamsubiri Ngwea akitua tu afanye naye kolabo! Nilipomuuliza alikuwa na muda gani tangu alipomtaarifu kuwa anataka kufanya naye kolabo aliniambia hakuwa amemwambia lakini angeongea naye.
Kila mmoja wenu alikuwa akisema lake. Kuna mliokuwa mkipishana Mlimani City kununua miwani kubwa nyeusi ya kutokelezea msibani. Kwanza hata mchango wenyewe sina hakika kama mlitoa. Ishu ilikuwa ni kuuza ‘nyago’ kama kawaida yenu. Kuonekana kwingi kuliko hata hiyo sanaa unayoifanya.
Kuna aliyejichimbia saluni kutengenezwa nywele ili akafunike msibani. Huo unaitwa ‘umbulula’ kama mnavyoitwa baadhi yenu mtaani.
Sikatai kwamba kila mtu alikuwa na mpango wa kufanya kazi na Ngwea kwani haina ubishi alikuwa ni kichwa. Hilo tuliache kwa sababu kama kweli kila mtu alitaka kufanya naye kazi basi asingepata hata muda wa kupumzika!
Kuna taarifa kuwa jamaa alikuwa na msongo wa mawazo (stress) na wengi wenu mlilijua hilo. Wapo aliowatamkia kabisa kuwa hana raha kwa sababu alikosa au alidhulumiwa mapato ya muziki wake ambao baada ya kifo, nyimbo zake mmezifanya za taifa.
Kama ndivyo na mlikuwa mnampenda, mbona hamkumsaidia akiwa hai hadi akaamua kwenda kujitafutia maisha ya kuungaunga nchini Afrika Kusini? Huo ndiyo unafiki mkubwa uliopitiliza.
Ukweli ni kwamba kuna tabia inayoshika kasi kwenye jamii ya kutambua mchango wa mtu anapokutwa na umauti.
Lakini tatizo halipo kwa mastaa tu kwani hata jamii ina tatizo kubwa. Wapo mashabiki waliotumia nafasi hiyo kujisevia nyimbo zake bila malipo. Inaitwa kufa kufaana. Ni tabia mbaya mno kwani huo nao ni ufisadi wa haki ya mtu hata kama ametangulia mbele ya haki.
Kwa nini msitoe sapoti kwa mtu anapokuwa hai badala yake mnasubiri akifariki dunia ndiyo mnajitokeza na kuanza kummwagia sifa kibao? Au ndiyo mbwembwe au mbovumbovu za mastaa? Huo ni unafiki unaoondoa ubinadamu.
Kuna kila sababu ya kubadilika la sivyo mnaonekana watu wa ajabu na sanaa inayowapa mkate wa kila siku itaanguka. For the love of game!

SOURCE : GPL

About Author

Advertisement

 
Top