Brandts katikati akiwa na BIN ZUBEIRY kushoto na Meneja wa Yanga SC, Hafidh Saleh
Na Mahmoud Zubeiry,
KOCHA Mkuu wa klabu bingwa ya soka Tanzania na Afrika Mashariki na Kati, Yanga SC, Mholanzi Ernie Brandts amesema kwamba anataka kushinda mataji yote msimu ujao na kufika mbali katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY, baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam usiku wa jana, beki huyo wa zamani wa Uholanzi, alisema kwamba anaamini hayo yote yatawezekana kama uongozi utaendelea kumsikiliza na kufuata ushauri wake kuhusu ujenzi wa timu na maandalizi kwa ujumla.
Brandts aliyekuwa kwao kwa likizo fupi baada ya kumaliza msimu kwa mafanikio, alisema wakati anaondoka aliwaagiza viongozi wasajili wachezaji wazuri kadiri wawezavyo katika idara zote ili kuleta ushindani ndani ya timu, kwani bila hivyo wachezaji ambao wanafanya vizuri kwa sasa kwenye timu watabweteka.
Akitoa mfano, alisema mwanzoni mwa msimu uliopita kuna wachezaji walikuwa hawajitumi, hadi alipopambana nao ndipo wakaongeza juhudi. “Kwa hivyo timu kama inakuwa na wachezaji wengi wazuri, ni changamoto nzuri kwa wengine kujituma ili kulinda namba zao,”alisema.
Akimzungumzia mchezaji mpya aliyesajiliwa kutoka kwa mahasimu wa jadi, Simba SC, Mrisho Khalfan Ngassa, Brandts alisema ni mzuri na anafahamu vyema uwezo wake, lakini akamuasa; “Inabidi anihakikishie uwezo wake kuanzia mazoezini ili nimpange, vinginevyo nitakuwa nakaa naye benchi,”alisema.
Kuhusu mshambuliaji Mganda, Hamisi Friday Kiiza aliyegoma kusaini Mkataba mpya kwa kushindana dau na uongozi, Brandts alisema; “Acha aende, kama anataka fedha nyingi kuliko wenzake, aende tu. Viongozi watafute mchezaji mwingine,”.
Brandts alisistiza sera yake ni kuangalia uwezo wa mchezaji mazoezini na hatampanga mtu kwa sababu ya jina lake. Alisema katika msimu mpya anataka kuongeza kasi zaidi ya uchezaji ndani ya timu.
Hata hivyo, alisema changamoto kubwa anayokabiliana nayo kwa sasa ni Uwanja mzuri wa mazoezi na ameomba viongozi wajitahidi kumpatia Uwanja mzuri wa mazoezi na baada ya hapo watafurahia timu.
Hata hivyo, Brandts alisikitishwa na kitendo cha wachezaji wachache tu kujitokeza mazoezini tangu timu ianze kujifua juzi na akasema kama hali hiyo itaendelea hawezi kutarajia kufanya vizuri kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
“Nimeambiwa wachezaji saba tu wa kikosi cha kwanza ndio wanafika mazoezini, wengine wote ni wa kikosi cha pili. Sasa hii si nzuri, ila kwa sasa siwezi kulizungumzia sana hili, hadi nitakapokutana na uongozi. Nahitaji nidhamu katika timu ili kutimiza malengo na kuwafurahisha mashabiki wetu,”alisema.
Na kuhusu Kombe la Kagame, michuano iliyopangwa kuanza Juni 18 nchini Sudan, Brandts amesema ikithibitika kuna machafuko atapendekeza timu isiende.
Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), chini ya rais wake Mtanzania, Leodegar Chillah Tenga limeipa Sudan uenyeji wa Kagame msimu huu, licha ya kwamba kuna mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanaendelea nchini humo.
Tayari Serikali ya Tanzania, kupitia Waziri wa Mambo ya Nje, Mh. Bernard Membe imetoa onyo kwa wawakilishi wa nchi kwenye michuano hiyo kwamba hakuna amani Sudan.
Klabu ya Simba, kupitia kwa Mwenyekiti wake, Alhaj Ismail Aden Rage, imesema haitakwenda kucheza mashindano hayo Sudan, kwa kuwa kuna vita, lakini Yanga ambao ndio mabingwa watetezi kwa miaka miwili mfululizo bado haijatoa tamko rasmi.
Yanga wamepangwa Kundi C katika michuano hiyo pamoja na Ports ya Djibouti, Express ya Uganda na Vital 'O' ya Burundi, wakati wapinzani wao wa jadi, Simba SC wamepangwa Kundi A pamoja na wenyeji El-Mereikh, Elman ya Somalia na APR ya Rwanda.
Katika michuano hiyo inayotarajiwa kufikia tamati Julai 2, mwaka huu mjini Khartoum, Sudan, mabingwa wa Kenya, Tusker wamepangwa Kundi B pamoja na wenyeji wengine, Al-Hilal, Falcons ya Zanzibar, Al Ahly Shandy ya Sudan na Al-Nasir Juba ya Sudan Kusini.
Yanga wataanza kampeni zao za kutetea taji hilo Juni 20 kwa kumenyana na Express, wakati Simba SC itashuka dimbani Juni 21 kufungua dimba na El-Mereikh, na mechi zote zitachezwa Elfashar.
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.