Unknown Unknown Author
Title: ASKARI 12 WAFUKUZWA KAZI, WASHITAKIWA KWA KUHUSIKA NA MAGENDO, RUSHWA
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
HATIMAYE Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, limeamua kuwafukuza kazi askari wake 12 wanaotumiwa kujihusisha na biashara za magendo...

clip_image001

HATIMAYE Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, limeamua kuwafukuza kazi askari wake 12 wanaotumiwa kujihusisha na biashara za magendo na kuwalinda wafanyabiashara wanaokwepa kodi.

Awali kabla ya hatua hiyo kufikiwa askari 16 walikuwa wakishikiliwa katika kituo cha kati na uchunguzi uliofanyika dhidi yao wanne walibainika kutohusika na tuhuma hizo.

Tanzania Daima imedokezwa kuwa askari 12 waliofukuzwa kazi wakati wowote kuanzia sasa watafikishwa katika mahakama za kiraia kujibu mashtaka yao.

Habari za uhakika kutoka ndani ya jeshi hilo zinapasha kwamba jana askari wote 16 walikuwa wakishikiliwa katika kituo cha polisi Kati kabla ya kuhamishiwa kituo cha Kijitonyama (Mabatini) walikosomewa hukumu yao.

Askari hao walisomewa hukumu hiyo na Kamanda mpya wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, aliyeripoti kazini mwanzoni mwa wiki hii akitokea mkoani Arusha alikokuwa akishikilia wadhifa wa Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO).

“Wambura kaingia kwa kishindo, kawasomea hukumu leo asubuhi wale askari waliokuwa mahabusu, wanne wameachiwa huru na wamesema wenzao wamefukuzwa kazi,” kilisema chanzo cha habari.

Tanzania Daima, iliwasiliana kwa njia ya simu na afande Wambura juu ya hukumu yake ya kuwatia kitanzini askari 12 ambapo alisema suala hilo mwenye uwezo wa kulizungumzia ni Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova.

“Hilo ni suala kubwa sana kwangu, ni la kanda, mpigie kamanda wa Kanda Maalum atakupa kila kitu unachohitaji,” alisema Wambura.

Tanzania Daima, lilipowasiliana na Kamanda Kova alihoji gazeti lilivyopata habari hizo kabla hazijafika ofisini kwake.

“Unapataje taarifa hizo kabla hazijafika kwangu wakati mimi nazisubiri? Huyo jamaa anakupaje taarifa kabla ya kufika kwangu? Mwambie aliyekupa hizo taarifa akwambie yote,” alisema.

Hata hivyo Kamanda Kova aliitaka Tanzania Daima impe muda zaidi alishughulikie jambo hilo na likiwa tayari ataliweka wazi kwa umma.

Mwanzoni mwa mwezi uliopita, Tanzania Daima, iliandika habari za polisi na baadhi ya maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kujihusisha na biashara za magendo na kuwakingia kifua wafanyabiashara wanaokwepa kodi Kamuhanda ahamia Dar

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP, Saidi Mwema, amemhamishia makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Michael Kamuhanda.

Kamuhanda anakumbukwa kwa kusimamia operesheni ya jeshi hilo mkoani Iringa dhidi ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliokuwa wakifungua tawi la chama hicho katika kijiji cha Nyololo Septemba 2 mwaka jana katika operesheni hiyo mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Chanel Ten, Daudi Mwangosi, aliuawa na bomu lililodaiwa kutoka kwa mmoja wa askari waliokuwa wakimdhibiti mwandishi huyo.

Kutokana na mabadiliko hayo nafasi ya Kamuhanda imechukuliwa na ACP, Ramadhan Mungi (aliyekuwa Makao Makuu ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai).

Katika taarifa ya Jeshi la Polisi kwa vyombo vya habari, mbali na Kamuhanda, makamanda wengine waliohamishwa ni ACP Charles Kenyela (RPC Kinondoni) aliyehamishiwa makao makuu ya upelelezi wa makosa ya jinai.

DCP, Ally Mlege, aliyekuwa Makao Makuu ya Polisi amehamishiwa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na kuwa mkuu wa utawala na rasilimali watu.

ACP Duwani Nyanda aliyekuwa makao makuu ya idara ya upelelezi amehamishiwa mkoani Arusha kuwa mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa uhamisho huo ni wa kawaida kwa mujibu wa kanuni, taratibu na miongozo ya Jeshi la Polisi.

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top