SIKU chache baada ya Serikali kuahidi
kusaka kokote duniani wachochezi wa vurugu za Mtwara, Chama cha Wananchi
(CUF) kimeibuka na kudai hakihusiki.
Chama hicho kimedai kupata taarifa ya
kuwapo mpango wa kukamata viongozi wa CUF na kuuaminisha umma kuwa ndio
wahusika wa kuchochea, kupanga na kufanya vurugu za Mtwara.
Hayo yalielezwa jana na Mwenyekiti wa
chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba kupitia taarifa yake kwa vyombo vya
habari, akidai Serikali imekuwa ikiwabambikia kesi nzito watu wasio na
hatia.
Alidai CUF inafanya siasa kwa kujenga
hoja na katika suala la gesi imejenga hoja za kiuchumi na maendeleo na
uwajibikaji wa kisiasa kuhusu utekelezaji wa miradi ambayo CCM na
serikali yake iliahidi kuitekeleza.
“Viongozi wa CUF hawajachochea vurugu
wametumia majukwaa ya mikutano ya hadhara na maandamano ya amani kujenga
hoja za kimsingi,” alibainisha.
Alitaka Serikali iache kushikilia hoja kuwa mgogoro huo ni matokeo ya uchochezi wa wanasiasa wachache wanaojitafutia umaarufu.
Akizama zaidi katika hoja zake, alisema
kukamata viongozi wa CUF wa wilaya za Mtwara na Lindi na wa kitaifa,
hakutamaliza mgogoro wa Serikali na wananchi wa Mtwara ikiwa serikali
itaendelea kuwabeza, kuwadharau na kutowasikiliza, badala yake itaongeza
chuki dhidi ya Serikali.
Aidha, ametaka Bunge liunde kamati teule
ya kuchunguza kwa nini mradi wa kufua umeme megawati 300 umesitishwa na
serikali, upembuzi yakinifu wa mradi wa bomba la gesi na mikataba yote
inayohusiana na mradi huu.
Kauli ya Profesa Lipumba ambaye
kitaaluma ni mchumi, imekuja siku chache baada ya Rais Kikwete kutoa
tamko kali, akisema serikali itakamata wanasiasa wanaochochea vurugu
Mtwara kwa kisingizio cha kuzuia gesi isitoke mkoani humo.
Kikwete alitoa kauli hiyo Dodoma
alipohutubia wananchi wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya
Dodoma-Iringa eneo la Bahiroad. Barabara hiyo ya kilometa 70 ni kutoka
Dodoma mpaka Fufu. Asubuhi yake alizindua Iringa-Migori.
Ilikuwa ni siku moja baada ya vurugu
kubwa zilizoanzishwa na watu wanaopinga uamuzi wa serikali wa kujenga
bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam, licha ya Serikali mara
kadhaa kuelezea umuhimu na faida ya bomba hilo kwa uchumi wa Tanzania
kwa ujumla.
Akihutubia, alisema gesi ya Mtwara ni
rasilimali ya Taifa na hakuna mtu anayeweza kusema, kwamba ni mali yake,
huku akiongeza kuwa madai yanayotolewa na wachochea vurugu kuhusu
rasilimali hiyo ya gesi hayakubaliki na hayana nafasi katika Tanzania.
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.