YANGA inaweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kabla ya ligi kumalizika endapo tu itashinda mechi tano mfululizo na kufikisha pointi 60.Vinara hao wa ligi na pointi 42 kibindoni, baada ya kucheza mechi 19 kwasasa wamebakisha mechi saba kukamilisha ligi hiyo.
Endapo, Yanga itashinda mechi tano kati ya saba, itafanikiwa kufikisha pointi 60 ambazo hazitafikiwa na timu nyingine yeyote.
Timu inayoifukuzia Yanga kwa karibu ni Azam FC inayokamata nafasi ya pili ikiwa na pointi 37 lakini ikisaliwa pia na mechi saba.
Bingwa mtetezi, Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 34 na ikiwa na mechi saba mkononi.
Kama Azam itafanikiwa kushinda mechi zake saba ilizohifadhi mkononi itafikisha pointi 58, wakati Simba ikifanikiwa kushinda mechi nane itafikisha pointi 55 ambazo haziwezi kuiondoa Yanga kileleni.
Hata hivyo,Yanga inafahamu kuwa inatakiwa kupigana kufa na kupona ili isipokwe tonge mdomoni kwani endapo itapoteza mechi tatu mfululizo inaweza kuiruhusu Azam kutwaa ubingwa kama itashinda mechi zote zilizosalia.
Mechi saba za Yanga zilizosalia ni pamoja na dhidi ya Ruvu Shooting ,Polisi Morogoro,JKT Oljoro,Mgambo JKT ,Coastal Union,JKT Ruvu na Simba SC.
Faida nyingine iliyonayo Yanga ni kwamba mechi mbili tu ambazo ni dhidi ya Polisi Morogoro na Mgambo JKT ndiyo itacheza ikiwa ugenini lakini zilizobaki itakuwa nyumbani.
Kwa upande mwingine, African Lyon licha ya kuburuta mkia ikiwa na pointi 13 na Toto African iliyoko katika nafasi ya 14,zote zinafursa ya kuepuka kushuka daraja kama kila moja itashinda mechi zake sita zilizosalia.
Lyon ikishinda mechi zote itafikisha pointi 31 ambazo kwa sasa zimefikiwa na timu nne ikiwemo Simba iliyoko katika nafasi ya tatu,Coastal Union ya nane,Mtibwa Sugar ya tano na Kagera Sugar inayoshika nafasi ya sita.
Hivyo hivyo, Toto ina fursa ya kufikisha pointi 32 na kuzishusha timu nyingine 10 zilizoko juu yake isipokuwa Yanga na Azam pekee ingawa pia itakuwa ikiomba timu nyingine zipate matokeo mabaya.
Tags
SPORTS NEWS