Kapombe akilia baada ya kuumia Jumapili. hajaenda Mbeya
SIMBA SC ipo tayari mjini Mbeya kwa ajili ya mchezo wao wa kesho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya wenyeji Tanzania Prisons, utakaopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini humo.
Huo utakuwa mchezo wa tatu kwa Simba SC tangu kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, ikiwa imeshinda mechi moja tu 3-1 dhidi ya African Lyon na kutoa sare mbili, dhidi ya JKT Ruvu na JKT Oljoro, zote 1-1.
Simba imefika Mbeya bila wachezaji wake nyota watano, ambao ni majeruhi, Jonas Mkude, Shomary Kapombe, Paul Ngalema, Christopher Edward na Mussa Mudde. Edward na Mkude wanasumbuliwa na maumivu ya nyama za paja, Mudde ameenda kwao Uganda kushiriki msiba wa mwanawe na Ngalema anasumbuliwa na maumivu ya goti.
Kapombe aliumia misuli baada ya mechi dhidi ya Recreativo de Libolo ya Angola Jumapili na jana alifanyiwa vipimo katika hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga amesema kwamba majibu ya vipimo yanaonyesha Kapombe hana tatizo kubwa, bali misuli ilishituka kidogo.
Kamwaga amesema Kapombe ametakiwa kupumzika kwa siku nne, akipatiwa tiba za miale na atakuwa tayari kucheza mechi ijayo dhidi ya Mtibwa Sugar.