Kiungo wa Simba, Ramadhani Chombo (kulia), akifanyiwa faulo na beki wa Tusker, Fredrick Onyango katika mechi ya kirafiki ya kimataifa kwenye Uwanja wa Taifa. Simba ililala 3-0. Picha na Michael Matemanga
MABINGWA wa soka Bara, Simba jana waliogelea kipigo cha mabao 3-0 kutoka Tusker ya Kenya katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa, huku ujio wa kocha wao, Patrick Liewig kutoka Ufaransa ukizidi kutia shaka. Juzi, uongozi wa klabu hiyo ulitoa taarifa kuwa kocha huyo angewasili jana, na jioni angeshuhudia mchezo dhidi ya Tusker, lakini hata hivyo hakutokea uwanjani.
Viongozi wote wa Simba, akiwamo Mwenyekiti Aden Rage jana hawakupokea simu walipotafutwa ili kutoa ufafanuzi juu ya ujio wa kocha huyo, ambao haueleweki kutokana na kila siku kutolewa kauli mpya.
Katika mchezo dhidi ya Tusker kwenye Uwanja wa Taifa, Simba iliingiza wachezaji wengi yosso, na mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika tayari walishanyukwa 2-0.
Ukindoa, Haruna Shamte, Komabil Keita, Mussa Mudde, Kigi Makasi na Ramadhan Chombo, wachezaji waliobaki ni wale wa kikosi cha pili, kabla ya kuwaingiza wa kikosi cha kwanza kipindi cha pili, ambao nao hawakuweza kugomboe kipigo hicho.
Simba walikaribia kufunga bao katika dakika ya 33 kama siyo Mudde kupoteza nafasi nzuri ya kufunga, na badala yake akatoa pasi kwa mshambuliaji Abdallah Juma aliyeshindwa kuitumia vizuri.
Wekundu hao wa Msimbazi waliadhibiwa kwa makosa hayo baada ya kufungwa bao la utangulizi kupitia kwa mshambuliaji wa Tusker, Jesse Were dakika ya 35 akiwapiga chenga mabeki wa Msimbazi na kipa wao, William Mweta.
Tusker ikiwa na kikosi kamili na wachezaji kama, Joseph Shikokoti, Samuel Odhiambo, Ismail Dunga na Were, waliindesha puta ngome ya Simba na kufunga bao la pili dakika ya 45 kupitia Were tena aliyefunga kwa staili ya bao la kwanza. Kipindi cha pili, Simba ilifanya mabadiliko ya kuwaingiza Salum Kinje, Jonas Mkude, Ramadhan Singano, Nassor Masoud, Haruna Moshi, Emily Mgeta na Christopher Edward kuchukua nafasi za Paul Ngalema, Shamte, Juma, Seseme, Mudde, Ramadhan Redondo na Kigi Makasi.
Hata hivyo mabadiliko hayo hayakuonekana kuisaidia Simba, kwani dakika ya 53 Fredrick Onyango wa Tusker alizitikisa kamba za Simba kwa kufunga bao la tatu kwa kichwa.
Hii ni mechi ya pili Tusker kushinda, baada ya mchezo wa kwanza kuifunga Yanga bao 1-0 kwenye uwanja huohuo. Tusker iko nchini kucheza mechi kadhaa za kirafiki lakini pia ikijiandaa kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi itakayoanza Zanzibar mwezi ujao.