Unknown Unknown Author
Title: YANGA KUIBUKIA KWA MAAFANDE WA JKT RUVU LEO?
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
DAR ES SALAAM, Tanzania BAADA ya kuyumba katika mechi mbili za kwanza za Ligi Kuu ya Bara, Yanga, leo Jumamosi wanashuka dimbani kwa mara...
DAR ES SALAAM, Tanzania
BAADA ya kuyumba katika mechi mbili za kwanza za Ligi Kuu ya Bara, Yanga, leo Jumamosi wanashuka dimbani kwa mara ya tatu kuwakabili JKT Ruvu ya Pwani kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Yanga iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa ya kufanya vema kutokana na usajili mzuri, iliianza ligi kwa sare ya 0-0 dhidi ya Prisons kabla ya kufungwa 3-0 na Mtibwa Sugar.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga leo kukutana na JKT Ruvu ikiwa nafasi ya pili kutoka mkiani, ikiwa na ponti moja, haijafunga bao huku nyavu zake zikitikiswa mara tatu.

Wapenzi na mashabiki wa timu hiyo wameshikwa na butwaa wakihoji yako wapi mashuti ya akina Saidi Bahanunzi, Didier Kavumbagu, Hamisi Kiiza na vipi ukuta imara wa timu hiyo, uruhusu mabao matatu.
Licha ya ukuta wake kusukwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite na viungo Athumani Idd ‘Chuji’, Haruna Niyonzima, waliruhusu nyota wa Mtibwa kufunga mara tatu.
Akizungumzia mechi ya leo, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Tom Saintfiet, amewataka nyota wake kusahau kipigo hicho, wapambane kuhakikisha wanashinda kuanza safari upya.
Alisema ni matumaini yake kushinda mechi ya leo licha ya ubora wa wapinzani wao, ambao nao watakuwa wakitaka ushindi kusawazisha makosa ya kufungwa mabao 2-0 na Simba. 
Hata hivyo, Saintfiet alisema kwa kuitambua vizuri taaluma yake, hata ikitokea akapoteza mechi ya leo, hatajuta akitambua kuwa ni sehemu ya mchezo.
Pia, amewasihi wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi kuipa sapoti timu yao kwa kuishangilia, akitambua kuwa hamasa ina nafasi yake katika kupigania ushindi.
Kuhusu kikosi chake, Tom amesema Bahanunzi, Salum Telela na Juma Seif ‘Kijiko’ ndio majeruhi, wengine wote wako fiti kuipigania timu yao.
Vita nyingine ya ligi hiyo iliyoanza Septemba 15, itakuwa kwenye Uwanja wa Chamazi kwa wenyeji Azam kuwakaribisha wababe wa Yanga, Mtibwa Sugar.
Mechi nyingine itakuwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha kwa JKT Oljoro kuwakabili Polisi Moro huku Coastal Union ikiwaalika Toto African ya Mwanza Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.











About Author

Advertisement

 
Top