West Brom yavurumishiwa 3-1 na Newcastle

Newcastle ikionesha kandanda safi ilifanikiwa kuilaza West Brom na kufikisha pointi sawa 50 na wanaoshikilia nafasi ya tano Chelsea.Papiss Demba Cisse aibuka shujaa wa Newcastle

Mkwaju wa pembeni wa Hatem Ben Arfa kwa Papiss Cisse ulikuwa ni bao la kwanza kwa Newcastle ambapo alifunga bao kwa urahisi huku wachezaji wa West Brom wakidhani ameotea.
Baadae alikuwa Ben Arfa aliyeipangua ngome ya West Brom na kuandika bao la pili kabla hajamlisha pande zuri Cisse na kuandika bao la tatu ambapo mlinda mlango wa West Brom Ben Foster aliachwa akigaagaa.
Kipindi cha pili kujichanganya kwa safu ya ulinzi ya Newcastle kulimpatia nafasi Shane Long kufunga bao pekee la kufutia machozi kwa West Brom, lakini Newcastle ilifanikiwa kulinda mabao yake na kujizolea pointi tatu na kujiweka katika mazingira mazuri ya kucheza ligi ya Ulaya msimu ujao.

Spurs wanahisi bado wataipiku Arsenal

Harry Redknapp amewaonya mahasimu wao wakubwa wa Kaskazini mwa London Arsenal kwamba Tottenham itapigana kiume kuishikilia nafasi ya tatu ya msimamo wa Ligi Kuu ya England.Redknapp anahisi wataipiku Arsenal                                                      Wakiwa wametoka sare ya 0-0 katika uwanja wa Stamford Bridges, Spurs ambao wapo katika nafasi ya nne wameweza kupanua wigo wa pointi hadi kufikia tano dhidi ya Chelsea katika mbio za kuwania nafasi nne bora na hivyo kujipatia upenyo wa kucheza Ligi ya Ubingwa wa Ulaya.
Lakini kwa sasa wapo pointi tatu nyuma ya Arsenal, wakati mwezi mmoja tu uliopita walikuwa wameipiku Arsenal kwa jumla ya pointi 10.
"Nahisi hali inatupendelea, Arsenal inakabiliwa na baadhi ya michezo migumu," alisisitiza Redknapp.
"Watacheza na Man City nyumbani kwao, vile vile Chelsea nyumbani kwao. Mechi zote hizo ni ngumu.
"Ghafla tumejikuta tukipitwa na Arsenal ambao tuliwazidi kwa pointi 10.
"Hali inaweza kubadilika. Hatuna budi kupigana kiume na kushinda michezo inayofuata."
Redknapp amewapa changamoto wachezaji wake wa Tottenham kushinda angalao mechi zao sita kati ya nane zilizosalia za Ligi Kuu na kujipatia nafasi ya nne bora na hivyo kujihakikishia kurejea tena katika hekaheka za Ubingwa wa Ulaya msimu ujao.

"Tunakabiliwa na michezo afueni, ninavyohisi," aliongeza Redknapp.
Naye meneja wa muda wa Chelsea Roberto di Matteo alikiri kikosi chake huenda kinahitaji kushinda mechi zilizosalia ili kuiengua Spurs katika nafasi nne bora.
Di Matteo alisema: "Kuziba pengo, hatuna budi tushinde mechi zote zilizosalia."
"Itakuwa kibarua kigumu lakini kutoka siku ya kwanza nilipoteuliwa, tulifahamu kazi itakuwa ngumu.
"Kuna michezo minane imesalia na tutajaribu kushinda mechi nyingi kadri iwezekanavyo kujaribu kupata nafasi ya nne."
Di Matteo pia alionesha kukerwa kwa kikosi chake kunyimwa mkwaju wa penalti baada ya Ramires kuangushwa alipogongana na mlinzi wa Spurs Benoit Assou-Ekotto.

Post a Comment

Hii ni Blog kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Nchi yetu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...

Previous Post Next Post