Hali ya wasi wasi bado inazingira maeneo ya mabondeni katika jiji la Dar Es Salaam kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kusababisha vifo vya watu wasiopungua 20 na uharibifu mkubwa wa mali na miundombinuIdara ya utabiri wa hali ya hewa (Tanzania Meteorological Agency) imeonya kuwa mvua hizo nzito zitaendelea kunyesha na imeshauri watu wanaoishi maeneo ya mabondeni kuhama haraka.
Mvua hizo zilizoanza kunyesha Jumanne alfajiri zimesababisha shughuli nyingi kusimama hasa kutokana na barabara muhimu zinazounganisha jiji na vitongoji vyake kutopitika na madaraja kubomoka.
Baadhi ya maeneo yaliyoathirika zaidi ni kama Jangwani, Kigogo, Mburahati na Bonde la Mto Msimbazi ambalo linamwaga maji katika bahari ya Hindi.
Kutokana na kiasi kikubwa cha maji kuingia baharini, hata maji katika Bahari ya Hindi yamebadilika rangi na kuwa ya maji machafu ya mafuriko.
Kuna maelfu ya watu wanaoishi katika maeneo ya mabondeni ambao mpaka sasa makazi yao yamebomolewa na wamekuwa wakihifadhiwa katika vituo vya dharura.
Shirika la msalaba mwekundu linakadiria kuwa watu zaidi ya 5,000 wameathirika kwa njia moja au nyingine kwa kukosa makazi au miundombinu kuharibiwa.
Mmoja wa waathirika ni Tabu Kibwa ameeleza kuwa nyumba yake yote imezingirwa na kumezwa na maji.
"Tumepoteza kila kitu, kwa kweli tumebaki mikono mitupu. Kila kitu katika nyumba kimepotea ikiwa ni pamoja na televisheni na majokofu," alisema.
Hata hivyo wengi wa wakazi hao wamegoma kuhama kwa miaka mingi licha ya kufahamishwa hatari ya mafuriko.
Kwa mujibu wa Idara ya hali ya hewa, hizi ni mvua nzito zaidi kuwahi kunyesha Dar Es Salaam tangu Tanzania ilipopata uhuru mwaka 1961.
Kamanda wa polisi wa mkoa maalum wa Dar es Salaam, Suleiman Kova, amewasihi watu kuhama mabondeni, lakini amekiri baadhi yao wamegoma kabisa.
"Tulikwenda kuwaokoa baadhi yao na waligoma kuhama wakisema hawawezi kuondoka kwa kuwa wanachunga mali zao," alisema.
Ingawa mvua zimeonekana kusababisha maafa makubwa zaidi Dar Es Salaam, lakini zimekuwa zikinyesha kwa nguvu katika maeneo mengi kama Iringa na Rukwa ambako madaraja na barabara vimebomolewa.
MBUNGE WA MAFIA AKIWA KATIKA BOTI ALIYOIKODI KUOKOA WANANCHI WALIOKUMBWA NA MAFURIKO.DAR
Hapa ni Airport DSM hali ilivyokuwa jana
Kama ambavyo tunafahamu linapotokea janga kama hili panahitajika misaada mingi sana kama vile maji, chakula, mavazi, n.k. hivyo Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Bw. Said Mecky Sadick amewaomba wale wote wenye lengo la kutoa msaada wapeleke misaada hiyo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa iliyopo Ilala Boma jijini Dar Es Salaam.
Bw. Sadick amezungumza hayo wakati wa mahojiano maalum aliyoyafanya na East Africa Radio katika walipotaka kufahamu mambo mbalimbali yanayoendelea kutokana na maafa hayo yaliyoikumba Taifa.