NIJUZE NIJUZE Author
Title: Taifa Queens yanusa medali Maputo
Author: NIJUZE
Rating 5 of 5 Des:
WAKATI timu ya Taifa ya Netiboli 'Taifa Queens' ikikaribia kutwaa medali ya fedha au shaba katika Michezo ya Afrika inayoendelea nch...

imageWAKATI timu ya Taifa ya Netiboli 'Taifa Queens' ikikaribia kutwaa medali ya fedha au shaba katika Michezo ya Afrika inayoendelea nchini Msumbiji, timu ya ngumi yadai ilikuwa ombaomba jijini Maputo.
Tanzania na Zambia zinagombea medali fedha au shaba baada ya wote kufikisha pointi 10, lakini Taifa Queens wakiongoza kwa mabao kabla ya mechi za leo dhidi ya Botswana, huku Zambia ikiivaa Ghana.Uganda wenyewe imejihakikishia kupata medali ya dhahabu baada ya kushinda michezo yake yote.
Kwa matokeo yoyote ya leo, Tanzania itakuwa inapata medali yake ya kwanza kwenye michezo hiyo mikubwa ya Afrika.Taifa Queens itafanikiwa kutwaa medali hiyo baada ya jana kuicharaza Afrika Kusini kwa magoli 32-29 kwenye mchezo huo uliofanyika jijini Maputo.
Wakati neema hiyo ikinukia kwa mchezo wa netiboli hali ilikuwa tofauti kwa timu ya taifa ya ngumi za ridhaa ambapo kocha wa timu hiyo Pimentel Hurtado amedai kuwa dalili za kufanya kwao vibaya zilianza kuonekana mapema hata kabla mabondia wake hawajapanda ulingoni.
Timu hiyo ya Tanzania iliingia kwenye aibu ya aina yake nchini Msumbiji kufuatia kufanya mazoezi kwa kusuasua huku wakiazima vifaa vya mashindano kutoka kwa mabondia wa Zambia.
Ngumi ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Tanzania kuaga michezo hiyo baada ya mabondia wake watatu kukung'utwa katika hatua ya robo fainali na mmoja kuondolewa katika hatua ya makundi ya fainali hizo zinazoendelea nchini humo.
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya mchezo wa ngumi raia wa Cuba, Pimentel Hurtado alisema  ilikuwa vigumu kwao kushinda wakati hata vifaa vya mashindano hawakuwa navyo zaidi ya kutegemea kutoka kwa mabondia wa Zambia.
"Kuna wakati kocha wa Zambia alikuwa akitusema kuwa tunawasumbua kwa kuwa hatukuwa na vifaa vya mashindano kila wakati wanatuazima wao ilifikia mahali tukaona dalili za kushindwa ziko mbele yetu," alisema Hurtado kwa masikitiko.
Hurtado alisema siku wanaondoka nchini Agosti 28 kwenda Msumbiji waliwauliza viongozi wa Shirikisho la Mchezo huo nchini (BFT) kuhusu vifaa hivyo vya mashindano na wakaambiwa bado havijatolewa.
"Nadhani unaelewa vizuri matatizo tunayopata timu ya taifa ya ngumi tangu tuko 'Indoor' uwanja wa ndani wa Taifa hadi tunakwenda kambi Kibaha kabla ya mashindano, lakini kumbe hali hiyo imeendelea hadi kwenye mashindano ya Msumbiji.
"Wakati tunaondoka sisi tulitangulia na kuacha michezo mingine hapa nchini tukijua ratiba ya mashindano yetu ni Septemba Mosi, lakini ajabu wakati tunaondoka hatukupewa vifaa vya mashindano," anasema Hurtado.
Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga alipoulizwa juu ya madai hayo ya mabondia kukosa vifaa vya mashindano alisema kuwa wakati mabondia wanaondoka wao BFT waliwapa raba, fulana na bukta za mazoezi moja moja kwa kila bondia ambavyo vifaa hivyo ni msaada waliopewa na  NSSF na LAPF Ambazo zilikuwa za rangi ya bluu.
"Sielewi kama hawakupewa, lakini vitu ambavyo sisi BFT tuliwapa ndivyo hivyo, ambapo hadi nawasindikiza Uwanja wa Ndege walikuwa navyo sasa hivyo vya mashindano sijui kama walikuwa navyo ama la kwa kuwa mimi sikukagua mabegi yao labda uwaulize Serikali," alisema Makore.
Hata hivyo taarifa zisizo rasmi ambazo  zilipatikana zilieleza kuwa mmoja wa mabondia wa Tanzania, Emilian Patrick alikatwa pointi katika pambano lake la robo fainali dhidi ya bondia wa Congo baada ya kukiuka kanuni za mavazi za mchezo huo hivyo kumpa mpinzani wake ushindi wa pointi 14-10 kwa sababu hakuwa na vifaa vya mashindano.

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top