Unknown Unknown Author
Title: SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 15
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 15 MTUNZI: NYEMO CHILONGANI ILIPOISHIA...!!! Muda wote aliokuwa humo, moyo wake ulikuwa ukidunda kup...
SIMULIZI:: SITALIA TENA
SEHEMU YA 15
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI
SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 15

ILIPOISHIA...!!!
Muda wote aliokuwa humo, moyo wake ulikuwa ukidunda kupita kawaida. Kabla hajajiuliza atafanya nini, wakaletewa Qur-aan (Kitabu Kitakatifu cha Kiislamu) na kupewa, wajiandae kwa ajili ya kusoma aya mbalimbali kwa kichwa huku wakichanganya na zile zilizokuwa ndani ya kitabu hicho kitakatifu.

ENDELEA NAYO.....
Kareem akaanza kuelekea baharini, moyo wake ulikuwa na majonzi tele, alichokifikiria alikuwa mpenzi wake tu, moyo wake ulimpenda mno na hakuwa tayari kumuona akiondoka mikononi mwake.

Alisafiri kwa umbali mrefu, macho yake yalikuwa makini kuangalia kila kona, alitaka kumuona Saida, hakukuwa na kitu kingine alichokuwa akikitaka tofauti na mpenzi wake huyo tu.

Siku ya kwanza ikakatika akiwa huko baharini, alipambana na mchafuko wa bahari lakini bado hakurudi nyuma, alitaka kuhakikisha anampata msichana huyo na kurudi naye nyumbani salama.

Alizunguka mpaka siku ya pili, napo aliambulia patupu, hakuweza kumuona msichana huyo kitu kilichompa uhakika kwamba tayari mpenzi wake alikuwa amefariki dunia, akasimamisha boti na kuanza kulia kama mtoto.

Moyo wake ukawa umejeruhiwa, akahisi ukiwa na tundu kubwa mno ambalo asingeweza kuliponya hata kama angempata msichana wa aina gani, alikaa huko baharini kwa siku tatu ndipo alipoamua kurudi nyumbani huku bado akiwa na majonzi tele.

Hakuwaambia wazazi wake, alifanya kila kitu kuwa siri, mara kwa mara alikuwa akielekea baharini na kuweka maua kama kumuenzi mpenzi wake aliyekuwa akimpenda mno.

Baada ya mwezi mmoja, mfungo ukaisha, Sikukuu ya Iddi ikaingia na kumalizika na baada ya siku kadhaa, Waislamu wote wakatakiwa kuingia kwenye Sikukuu ya Maulidi kwa ajili ya kukumbuka kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW).

Kwa kawaida kwa nchini kama Oman na nyingine kama Iran, Iraq na Pakistan walikuwa wameweka tabia ya kuwa na mashindano ya kusoma aya ambapo hukutana katika nchi moja na kushindania huko.

Katika mwaka huyo, watu kutoka katika nchi hizo walitakiwa kukutana nchini Iran kwa ajili mya mashindano hayo ambapo mshindi alikuwa akipata zawadi ya kuzunguka sehemu mbalimbali duniani kwani alikuwa akitangazwa kama mtu aliyekuwa akisoma sana, aliyezishika aya nyingi kichwani mwake.

Kwa kuwa shindano hilo lilidhaminiwa na wadhamini wengi akiwemo Abdulaziz, baba yake Kareem, naye Kareem alitakiwa kwenda huko kushuhudia shindano hilo, na yeye alipewa nafasi ya kumpa zawadi mshindi wa shindano hilo.

Kwa Kareem ilikuwa ngumu kufanya hivyo, hakujisikia, hakutaka kuondoka nchini kwao na wakati alikuwa na majonzi tele, aliamua kubaki Oman na kumwambia baba yake achague mtu mwingine lakini si yeye.

“Kwa nini?” aliuliza baba yake huku akionekana kukasirika.
“Nina mambo mengi baba!”
“Kiasi kwamba huwezi kwenda?”
“Ndiyo!” alijibu na kuingia chumbani kwake.

Baba yake hakuwa na jinsi, akamtafuta mtu mwingine na kwenda kumuwakilisha huko Iran ambapo tayari matangazo yalikuwa yametangazwa kila kona, masikio ya kila mtu yalikuwa huko kwani hakukuwa na kitu kilichokuwa kikiheshimiwa kama hicho.

Katika mashindano hayohayo ndipo alipokuwa Saida, alikuwa na wanawake wengine, kwa sababu naye alichukuliwa kutoka kwa wanawake wale, akaonekana kuwa mmojawapo kutoka hapo nchini Iran.

Wanawake waliotakiwa kuwepo humo ni ishirini na tano lakini cha kushangaza, walikuwa ishirini na sita. Viongozi hawakujua kwa nini mmoja aliongezeka, hawakujua kama kulikuwa na mwanamke aliyeongezeka hata kabla ya kuingia hapo.

Katika ukumbi mkubwa waliokuwemo, kulikuwa na zaidi ya watu elfu moja, kila mmoja alikuwa mahali hapo kwa ajili ya kuangalia ni jinsi gani wanawake walikuwa na uwezo mkubwa katika kusoma aya mbalimbali za Qur-aan.

Waandishi wa habari kutoka katika vituo mbalimbali vya habari kama Al Jazeera, Tammim na vituo vingine walikuwa mahali hapo, tukio hilo lilikuwa muhimu, lililokuwa likifuatiliwa na watu wengi katika nchi za Kiarabu.

Wakati watu wakitakiwa kujiandaa, Saida alikuwa amekaa nyuma kabisa, mapigo yake ya moyo yalikuwa juu, pale alipokuwa alikuwa akitetemeka, Kitabu cha Qur-aan alichokuwa amekishika, alitamani kukiacha katika mkeka na kuondoka lakini aliogopa kufanya hivyo.

Kila mmoja alionekana kujiandaa vilivyo, baada ya dakika arobaini na tano, mashindano yakaanza, wakaanza wanawake kutoka Iraq na nchi nyingine, kila mmoja alijitahidi kuzisoma aya zile walizokuwa nazo vichwani mwao, walizisoma na kuzisoma, walionekana kawaida sana, hakukuwa na jipya, walifanya kama wale wa miaka ya nyuma walivyofanya.

Kwa kawaida, katika nchi za Uarabuni hakukuwa na wanawake wengi waliokuwa wakipitia madrasa, wengi walijifunza aya walipokuwa wakiingia katika maisha ya ndoa, tena kwa kulazimishwa na waume zao.

Haikuwa kama nchini Tanzania ambapo mtoto alipokuwa akikua, alipelekwa madrasa kujifunza, alitakiwa kujua aya nyingi na wakati mwingine kulikuwa na mashindano ya vyuo kwa vyuo, mtaa kwa mtaa au mkoa kwa mkoa.

Wanawake wote wakasoma aya zao, walibaki wawili, mwanamke mmoja na Saida tu. Walimu wao hawakujua ni nani alitakiwa kuzungumza kwani idadi kamili iliyotakiwa ilikuwa ishirini na tano tu, na tayari ishirini na nne walikuwa wamekwishazungumza.

Saida hakutaka kujiuliza, hakutaka kuchaguliwa, harakaharaka akasimama na kwenda kule mbele kulipokuwa na kipaza sauti. Walimu wakashangaa, haikuwa kawaida mtu kukimbilia kutaka kuzungumza, wengi waliogopa kwa kuwa hawakujua.

Alipofika hapo, akanyamaza kwa muda. Kamera zilikuwa mbele yake, kila mmoja alitaka kumsikiliza msichana huyo ambaye alikuwa akitafutwa sana nchini Oman na taarifa zake zilifika mpaka katika nchi nyingine na kueleza kwamba mtu huyo alikuwa hatari sana.

“Leo nitakwenda kuzungumza kuhusu Mtume Muhammad (SAW), maisha yake na pia nitakwenda kuzungumzia jinsi tunavyotakiwa kutenda mema,” alisema Saida, alipomaliza, akayafumba macho yake kidogo, alipoyafumbua, akaichukua Qur-aan na kuibusu.
“Surah al Maeda:92-Aya hii inaeleza kwamba imani yetu katika Uislamu haijakamilika mpaka tutakapomtii Allah na mtume wake, Muhammad (SAW). Ndugu zangu Waislamu, dunia imebadilika, tumeshuhudia dunia ikibadilika, kila mtu amekuwa akifanya kile akitakacho, kuna watu wengi wanatamani kufuata yale Allah aliyotuagiza lakini wamekuwa hawatii kile kilichoandikwa. 

“Mtume alitukumbusha kwamba inatakiwa tuyaheshimu maneno ya Allah, tushike nguzo tano za Kiislamu lakini leo hii Waislamu hawataki kuswali, leo hii Waislamu hawataki kufunga kwa kusingizia vidonda vya tumbo, tunamdharau Mtume Muhammad SAW, tunamdharau Allah, tunakwenda kinyume na kile kilichoandikwa,” alisema Saida, akanyamaza, akayafumba macho yake, kijasho chembamba kikaanza kumtoka, akameza mate na kuendelea.

Hakuishia kusoma aya hiyo tu, alisoma Surah al Qalam: aya ya nne, akasoma Sural al anbiya, aya ya 107, akasoma Surah al Maida aya ya 19, Surah al Yunus aya ya 15, katika kuelezea maisha ya Mtume Muhammad, akamalizia na Sural al Ahzab aya ya 40. 
Kila mtu aliyesikia akabaki kimya akimwangalia Saida. 

Hawakuamini kama kungekuwa na mwanamke ambaye angesoma aya zote hizo tena kwa kichwa, kila mmoja akahisi kwamba mwanamke huyo alikuwa mtu wa tofauti na wapo wengine ambao walihisi kwamba huyo alikuwa malaika ambaye alishushwa kwa ajili ya kuwaambia wanadamu kile ambacho walitakiwa kufanya.

Kadiri alivyokuwa akizungumza, Saida alipata nguvu ya kuongea zaidi, jinsi watu walivyokuwa akimshangaa, akaamini kwamba walimuelewa sana na hawakuamini kama angekuwa na uwezo huo kwani kulikuwa na mashehe wengine ambao hawakujua kabisa baadhi ya aya, tena kuzitaja kwa kichwa.

Aliendelea na kuizungumzia Surah al Maida aya ya 48 ambayo ilizungumzia jinsi ya kutenda mema. Akazungumzia jinsi baadhi ya Waislamu walivyokuwa wakijiita Waislamu na wakati hawakuwa wakitenda mema, Allah alichukizwa kwani hakumuumba binadamu kumchukia binadamu mwenzake, hakumpa mtu utajiri kwa ajili ya kumkandamiza masikini.

Maneno aliyokuwa akizungumza, kuna wengine wakaanza kulia, alizungumza maneno yaliyochoma mioyo ya watu wote waliokuwa mahali hapo ambao waliifanya dini kuwa kama kivuli na wakati nyuma ya pazia walikuwa wakifanya mambo ambayo Mtume Muhammad (SAW) aliwaambia waache kuyafanya kwa kuwa yalikuwa chukizo mbele za Allah.

Katika kumalizia, akamalizia na jinsi Waislamu wanavyotakiwa kudumisha amani. Akasoma Surah al Baqarah 2 aya ya 208 na kuzungumzia jinsi Allah anavyowasisitizia watu kuachana na njia za muovu shetwani na kufuata njia yake yeye.

Siku hiyo ikaonekana kama siku ya ukombozi, mpaka Saida anamaliza kuzungumza, wengi walikuwa wakilia huku wengine wakimtaka aendelee kuzungumza kwani kile alichokisema hakikuwa kikizungumzwa hata na mashehe wakubwa katika nchi hizo, wengi waliwafundisha watu kuhusu kutoa sadaka ili waneemeke katika sadaka hizo lakini hawakukemea dhambi, hawakuwaambia watu kwamba Mungu hakupenda dhambi, hakumuumba binadamu ili amuabudu shetani.

“Ni maajabu kwa mwanamke kusema aya hizi, hata mimi sikuwa nikizijua kabisa,” alisikika shehe mmoja, alikuwa mtu wa heshima kubwa lakini pamoja na kusoma kwake sana, hakuwahi kuzisoma aya hizo, alitumia ujanjaujanja mpaka kukipata cheo hicho.

Kwa sababu kila kitu kilichokuwa kikiendelea kilirushwa moja kwa moja kwenye televisheni, watu wengi hawakuamini, mwanamke aliyeonekana kwenye televisheni zao alionekana kama malaika.

Akapigwa sana picha lakini hakuvua nikabu yake, hakutaka kugundulika kama yeye ndiye alikuwa Saida aliyekuwa akisakwa sana nchini Oman. Akajibatiza jina la Salmah Sadiq Al Muntah.

Siku hiyohiyo akatangazwa mshindi, hakutakiwa kurudi, alitakiwa kukaa hotelini tayari kwa kuzungumka sehemu mbalimbali duniani kwa ajili ya kuwafundisha watu kuhusu Qur-aan kwani kwa sababu wao hawakujua, waliamini kwamba dunia nzima hawakujua na wakati aya alizokuwa amezisoma Saida, kwa Waislamu wa Kitanzania zilikuwa za kawaida kwa kuwa walifundishwa tangu madrasa.

Alipofikishwa hotelini, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuchukua simu yake na kumpigia Kareem, alizikumbuka namba zake, alikuwa nazo kichwani, simu ikaanza kuita, baada ya sekunde kadhaa, ikapokelewa na sauti ya mwanaume huyo ikaanza kusikika upande wa pili.

“Hallo...” aliita Kareem.
“Kareem mpenzi...” aliita Saida, hapohapo akaanza kulia. Kareem akashtuka.
“Saida. Upo wapi? Saida mpenzi, nimekutafuta sana, upo wapi, niambie upo wapi nije, siwezi kuishi bila wewe mpenzi, naomba uniambie ulipo nije,” alisema Kareem huku naye akianza kulia.
“Nipo Iran.”
“Iran? Unafanya nini huko?”
“Ni habari ndefu. Unamfahamu Salmah Sadiq Al Muntah?”
“Huyu mwanamke aliyeushangaza ulimwengu leo?”
“Ndiyo!”
“Nimemuona! Amefanya nini? Upo naye?”
“Hapana! Huyo ni mimi!”
“Ni wewe?”
“Ndiyo mpenzi!”
“Imekuwaje? Mbona sielewi?”
“Naomba uje Iran unichukue. Nataka kurudi nyumbani, siwezi kuendelea kuishi huku. Naomba uje kunichukua mpenzi,” alisema Saida huku akilia.
“Ninakuja kukuchukua. Tena leo hiihii! Nakuja kukuchukua mpenzi,” alisema Kareem na kukata simu.

********************************
Upande wa pili, Kareem hakuamini kama kweli alikuwa amezungumza na Saida, moyo wake ulikata tamaa na kuhisi kwamba mpenzi wake huyo alikuwa amekufa baharini lakini alipoisikia sauti yake, akaamini kwamba kweli Mungu yupo na alikuwa akitenda miujiza.

Alikumbuka kwamba baba yake alimwambia aende Iran kwa ajili ya kumkabidhi zawadi mshindi wa mashindano hayo, hakutaka kwenda huko lakini mwisho wa siku, msichana yule aliyeonekana kuwa hatari kwenye usomaji wa aya, kumbe alikuwa mpenzi wake na kama angekwenda, yeye ndiye ambaye angemkabidhi zawadi hiyo.

Moyo wake ulijuta, alihuzunika sana, hakutakiwa kabisa kukataa lakini huo haukuwa muda wa kujuta tena, kwa sababu Saida alimwambia kwamba yupo Iran ilikuwa ni lazima aelee huko, amchukue na kuondoka naye.

“Ni lazima niende Iran,” alijisemea.
Hakutaka kuchelewa, akaanza kufanya harakati za safari, baada ya saa moja, alikuwa na vibali vyote, akachukua ndege ya baba yake na kuondoka zake kuelekea huko huku moyo wake ukiwa na presha ya kumuona Saida aliyekuwa na mtoto wake tumboni.

Je, nini kitaendelea?, Usikose Sehemu Ijayo....!!!
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
KUWA KARIBU NASI LINDIYETU.COM
Usipitwe!! Ungana na Familia hii kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata Infortainment zote!! Usikose kujiunga na Youtube channel yetu ili kupata Exclusive mbalimbali kali kutoka LindiYetu TV

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top