Unknown Unknown Author
Title: SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 11
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 11 MTUNZI: NYEMO CHILONGANI ILIPOISHIA....!! “Mlitupa mapipa yote?” aliuliza Yusuf Al Sadiq huku akione...
SIMULIZI:: SITALIA TENA
SEHEMU YA 11
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI

SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 11ILIPOISHIA....!!
“Mlitupa mapipa yote?” aliuliza Yusuf Al Sadiq huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Ndiyo! Yalikuwa mazito lakini yote tuliyatupa baharini usiku huohuo,” alijibu kijana mmoja huku akionekana kutabasamu.
“Unasemaje?”
“Tuliyatupa yote mkuu!” alijibu kijana huyo. Yusuf Al Sadiq akashika kichwa na kukaa chini. Hakuamini alichokisikia kwani aliamini kwamba Saida alikuwa ndani ya pipa mojawapo.


HAYA SONGA NAYO SASA.....
Saida alisikia kila kitu, alibaki akiwa ametulia tu ndani ya pipa, hakutaka kuzungumza kitu chochote kile, alihisi akibebwa na watu hao kutoka nje, hakujua mahali alipokuwa akipelekwa, lakini ghafla akahisi kama yupo hewani na baada ya sekunde chache akashtuka baada ya kuhisi pipa limetupwa ndani ya maji.

Akashangaa, maji yakaanza kuingia ndani ya pipa lile, akagundua kwamba alikuwa ametupwa baharini hivyo alichokifanya ni kufungua mfuniko wa pipa na kisha kutoka nje na kulishika.

Alikuwa katikati ya bahari, hakujua ni mahali gani alitakiwa kwenda, bahari ilichafuka na alikuwa akipelekwa huku na kule, ilikuwa ni usiku, hakuona dalili ya kisiwa chochote karibu yake na mbaya zaidi aliiona meli ile ikianza kuondoka, alijitahidi kuita ili aje aokolewe lakini sauti yake haikusikika sehemu yoyote ile kutokana na mawimbi makubwa yaliyokuwa yakipiga.

Akalifunika pipa vilivyo ili kulipa nafasi ya kuelea, akafanikiwa na hivyo kutulia juu yake. Kwa usiku huo kulikuwa na baridi kali hapo alipokaa, alikuwa akilia kama mtoto, alitamani itokee meli nyingine na kumuokoa lakini hilo halikuwezekana kabisa.

Mawimbi yaliendelea kupiga kwa nguvu, hakuweza kuliongoza pipa hilo zaidi ya kuliacha hivyo kupelekwa huku na kule, popote pale mawimbi yalipoamua kumpeleka. Akakata tamaa, akahisi kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wake, hakuona dalili kama angeweza kupona, alisikia kuhusu bahari, jinsi watu walivyokuwa wakifa, kufa huku wakijiona, akajiona kwamba hatimaye naye angekufa kama watu hao.

Hiyo ilikuwa saa saba usiku, alikuwa peke yake baharini na hakujua ni sehemu gani alitakiwa kwenda. Bahari ilitisha, wakati mwingine alililalia pipa, alikaa hivyo kwa saa kadhaa kisha kuteremka na kulishikilia huku kuanzia kifuani mpaka miguuni kukiwa ndani ya maji.

Yalikuwa mateso makubwa, kuanzia usiku huo mpaka alfajiri alikuwa baharini akipigwa na baridi kali. Bahari ilitulia, aliangalia huku na kule na kuona kama kulikuwa na meli yoyote iliyokuwa ikija kule alipokuwa lakini hakuweza kuona meli yoyote ile.

Siku nzima alishinda ndani ya bahari, alilia sana, alimkumbuka mno Kareem, alitamani kuwa naye lakini ilishindikana kabisa. Akabaki akilia siku nzima, baridi lile lilianza kumtetemesha, mwili ulipokuwa ukikosa nguvu, alipanda juu ya pipa kisha kulilalia.

Hiyo ilikuwa siku ya kwanza, ikakatika, tumbo lilikuwa likimuuma kutokana na njaa kali, aliposhikwa na kiu, alikunywa maji ya bahari, ni kweli yalikuwa na chumvi mno lakini hakujali kwani alijua kwamba kama asingekunywa basi angekufa, hivyo hakuwa na jingine la kufanya zaidi ya hilo.

Usiku ulipoingia, kama kawaida bahari ikachafuka tena, alipelekwa huku na kule, alikosa msaada kabisa. Alipigwa na baridi, alivumilia kwa kuhisi kwamba labda kuna meli ingekuja pale alipokuwa na kumuokoa, lakini kila alipoangalia, hakuona meli yoyote ile.

Mungu naomba unisaidie,” alisema huku akilia.
Hakukuwa na msaada wowote ule, alipoangalia Mashariki, hakukuwa na meli wala kisiwa, alipoangalia Magharibi na sehemu nyingine kote huko hakuona kitu chochote kile, aliendelea kutulia katika bahari hiyo mpaka siku ya tatu kuingia.

“Mungu! Nimechoka, nimechoka kukaa baharini, naomba nife, naomba uichukue roho yangu,” alisema Saida huku akionekana kukata tamaa.

Tumbo lake lilisinyaa, kutokana na baridi na mwili kukaa ndani ya maji kwa siku hizo tatu, tayari ngozi yake ikaanza kuharibika kwa kuwa laini sana kitu kilichomfanya kuanza kuhisi kama kulikuwa na wadudu walikuwa wakimtembelea mwilini.

Alitulia hivyohivyo, hakula chochote zaidi ya kunywa maji hayo yenye chumvi nyingi. Maisha yake yalikuwa humo, alikonda lakini hakuacha kumuomba Mungu. Ghasia zote za baharini zilikuwa zake, alipelekwa na maji kila kona, alivumilia lakini siku ya nne akashindwa kuvumilia, asubuhi ya saa moja, mwili wake ukachoka mno, asingeweza kuendelea kulishikilia pipa lile, vidole vilikosa nguvu, alitamani kulipanda lakini akashindwa kabisa.

Alichokifanya ni kuanza kumuomba Mungu sala yake ya mwisho kwani asingeweza kuvumilia, kama kufa, alikuwa tayari kufa kwani aliteseka sana, kwa siku zote hizo, sasa akawa tayari kuliachia pipa lile.

“Mungu naomba uipokee roho yangu,” alisema huku akiliachia pipa taratibu na kuanza kuzama baharini. Huku mwili wake ukiendelea kuzama, akaanza kusikia honi za meli kubwa, alitamani kuogelea na kurudi juu lakini alishindwa kabisa, asingeweza kurudi juu zaidi ya kuendelea kwenda chini kwani hata kuichezesha mikono yake alishindwa.

Pumzi ikaanza kukata na baada ya sekunde kadhaa, macho yakalegea na hatimaye kuingiwa na giza kabisa.

Kilichoendelea baada ya hapo, hakukifahamu zaidi ya kujua kwamba hiyo ndiyo ilikuwa nafasi yake ya mwisho kuishi ndani ya dunia hii.

***************************
Moyo wa Kareem ulikuwa na furaha tele, hakuamini kama kweli alifanikiwa kumsafirisha mpenzi wake katika mikono salama kuelekea Dubai. Huku nyuma nchini Oman, bado serikali iliendelea kumtafuta Saida kila kona, hawakutulia, matangazo yaliendelea kusambazwa huku zawadi nono ikiwa imetangazwa kwa mtu yeyote ambaye angefanikisha kupatikana kwa msichana huyo.

Wakati yote yakiendelea, Kareem alikuwa akicheka, alijiona kuwa mjanja kuliko hata serikali, kila alipokaa, alivuta kinywaji na kuanza kunywa, hakujali mfungo wa Ramadhani, kwake ilikuwa ni kula bata kwenda mbele.

Siku ya kwanza ikakatika, ya pili, ya tatu mpaka siku ambayo alitakiwa kuwasiliana na ndugu yake aliyekuwa Dubai kwa ajili ya kumpokea, lakini hata kabla hajawasiliana na ndugu huyo, akapigiwa simu na Yusuf Al Sadiq.

Kitendo cha kuiona simu yake ikiita huku jina likionyesha ni la Yusuf Al Sadiq, akafurahi kwani alihisi kwamba angepewa habari njema kwamba mpenzi wake alifika salama Dubai hivyo amfuate na kuanza safari ya kuelekea Tanzania.

Akaipokea kwa mbwembwe.
“Mmefika salama?” aliuliza Kareem huku uso wake ukiwa umetawaliwa na tabasamu pana.
“Kareem. Kuna tatizo,” alisema Yusuf Al Sadiq, Kareem akashtuka.
“Tatizo? Tatizo gani?”
“Kuhusu Saida.”
“Nini kimetokea? Unanitisha!”

Alichokifanya Yusuf Al Sadiq ni kuanza kumuhadithia kile kilichokuwa kimetokea tangu mwanzo wa safari mpaka mapipa yalipotupwa baharini. Kareem hakuamini alichokisikia, alihisi kama alikuwa ndotoni na baada ya muda fulani angeshtuka kutoka kitandani.

Alijitahidi kwa nguvu zote kumuokoa mpenzi wake lakini mwisho wa siku aliambiwa kwamba mwanamke huyo alitupwa baharini tena akiwa ndani ya pipa katika sehemu iliyojulikana kama kifo.

Alihisi mwili wake ukitetemeka mno, kijasho chembamba kikaanza kumtoka ingawa ndani ya chumba kile kulikuwa na kiyoyozi, akasimama, akahisi kabisa kwamba angeweza kuangukia kitandani.

“Unasemaje?”
“Saida alitupwa baharini, vijana hawakujua kama alikuwa ndani ya pipa amejificha!” alisikika Yusuf Al Sadiq kwenye simu.

Kareem aliishiwa nguvu na kurudi tena kitandani, machozi yakaanza kujikusanya machoni mwake na baada ya sekunde chache yakaanza kutiririka mashavuni mwake. Aliumia, alihisi kisu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake kwa jinsi maumivu yalivyokuwa makubwa.

Hakutaka kubaki nyumbani, alichokifanya ni kutoka na harakaharaka ndani ya nyumba yao, hakutaka kuona akimpoteza mpenzi wake, alitaka kwenda hukohuko baharini kumtafuta kwani asingevumilia kubaki nyumbani na wakati mpenzi wake akiteseka huko.

Alichokifanya ni kuchukua boti ya baba yake, hakutaka kuwaaga, akaondoka Oman na kuanza kuelekea huko baharini, hakujua kulikuwa na umbali gani ila kwa sababu alikuwa na nahodha ambaye alifahamu njia za kuelekea Dubai, hakuwa na hofu, hata kama angeipata maiti yake, ingemfariji kuliko kuikosa na kuliwa na samaki.

Je, nini kitaendelea? TUKUTANE SAA MOJA ASUBUHI.
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
KUWA KARIBU NASI LINDIYETU.COM
Usipitwe!! Ungana na Familia hii kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata Infortainment zote!! Usikose kujiunga na Youtube channel yetu ili kupata Exclusive mbalimbali kali kutoka LindiYetu TV

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top