Unknown Unknown Author
Title: SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 03
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 03 MTUNZI: NYEMO CHILONGANI Kareem alimpenda Saida, hakutaka kuona akimpoteza msichana huyo ambaye kwa...
SIMULIZI:: SITALIA TENA
SEHEMU YA 03
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI

SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 03
Kareem alimpenda Saida, hakutaka kuona akimpoteza msichana huyo ambaye kwake alikuwa kila kitu, kubwa zaidi ni kwamba alikuwa na mimba yake, hivyo kwa namna moja ama nyingine ilikuwa ni lazima amuokoe kutoka katika mkono wa kifo. Alikuwa chumbani, hakutulia, alikuwa akizunguka huku na kule akifikiria ni kitu gani alitakiwa kufanya. Alihitaji msaada kipindi hicho, akaanza kuwafikiria marafiki zake ambao aliamini kwamba wangemsaidia kumnasua mpenzi wake katika kifo kilichokuwa kikimsogelea. 

Alikuwa na marafiki wengi ambao aliamini kwamba wangeweza kumsaidia lakini wakati akiwafikiria hao wote, kichwani mwake alikuja mmoja ambaye alikuwa na uhakika asilimia mia moja kwamba angemsaidia kumtorosha msichana huyo nchini humo. 

Rafiki yake huyo alikuwa Al Khalid, mtu ambaye alikua naye tangu akiwa mtoto mpaka kipindi hicho. Alichokifanya ni kuchukua simu yake na kuanza kulitafuta jina lake, alipolipata, hakutaka kuchelewa, harakaharaka akampigia simu. Simu iliita pasipo kupokelewa, iliendelea kuita mpaka ilipokatika. 

Hakutaka kukoma, alichokifanya ni kupiga tena kwani mtu huyo alikuwa muhimu sana, alikuwa mtu pekee ambaye angeweza kumuokoa kutoka katika tatizo kubwa alilokuwa nalo kipindi hicho. “Al Khalid! Can we meet somewhere! (Al Khalid! Tunaweza kuonana sehemu?) aliuliza Kareem mara baada ya simu kupokelewa, hata salamu hakutaka kutoa. “What is it?” (kuna nini?) “There is something I want you to help me,” (kuna jambo nataka unisaidie mara moja!) alijibu Kareem. Hilo lilikuwa jambo dogo kwa Al Khalid, mara kwa mara walikuwa wakipigiana simu na Kareem kuomba kusaidiana katika mambo mengi ambayo kwa namna moja au nyingine yaliufanya urafiki wao kuendelea kukomaa zaidi. 

Alimjua Kareem, alikuwa mtu wa kupenda kuyafanya mambo mengi kivyakevyake na kama kulikuwa na kitu alichokuwa akihitaji msaada, basi kitu hicho kilikuwa kikubwa ambacho kwa namna moja au nyingine alikwama kabisa kukifanya. “Lipi? Baadaye nitakwenda Masjeed, unataka nikusaidie katika lipi?” aliuliza Al Khalid kwenye simu. “Naomba tuonane kwanza.” “Ila si unajua kwamba leo tunasubiri mwezi uandame ndiyo tuanze kufunga?”
“Najua! Ila naomba tuonane kwanza.” 

Al Khalid na Kareem walikuwa marafiki wakubwa huku wote wakiwa watoto wa mabilionea wakubwa nchini Oman. Waliaminiana kwa kila kitu, walipendana ila tofauti yao ilikuwa moja tu. Al Khalid alikuwa mtu wa dini haswa, alikuwa mtu wa swala tano, hakutaka kusikia adhana akiwa nje ya msikiti, katika maisha yake yote, alimpenda Mungu na hakutaka kufanya dhambi kabisa. Kwa Kareem ilikuwa tofauti, hakuwa mtu wa swala, wakati mwingine aliombea misikiti yote ya Oman ibomolewe na kujengwe klabu kwa ajili ya kula bata usiku kama ilivyokuwa Dubai, Qatar na nchi nyingine zilizokuwa katika muunganiko wa Emirates. 

Wawili hao wakaonana katika Mgahawa wa Ya Sadeek uliokuwa katikati ya Jiji la Muscat. Wakaonana hapo na kuanza kuzungumza mambo mengine kabisa. Kichwani mwa Kareem kulikuwa na mambo mengi, alikuwa akijiuliza kama lilikuwa jambo sahihi kumuomba msaada Al Khalid au amuache na kuomba msaada sehemu nyingine. 
“Nina kitu nahitaji unisaidie,” alisema Kareem. “Kuhusu nini rafiki?” Kareem akamwambia ukweli Al Khalid kilichokuwa kimetokea, hakutaka kumficha kitu chochote kile, alikuwa rafiki yake wa dhati, akamuweka wazi kwamba alimpa mimba msichana ambaye alikuwa mfanyakazi wa ndani hivyo alihitaji msaada wa kuweza kumtorosha kutoka nchini humo. 

Al Khalid alishangaa, hakuamini alichokisikia kutoka kwa Kareem. Alishangaa kwani lilikuwa jambo lisilo la kawaida kwa Mwarabu kufanya kitu kama hicho, kumpa mimba msichana na wakati alijua fika kwamba adhabu kubwa kwa msichana ilikuwa ni kunyongwa. “Unanitania Kareem,” alisema Al Khalid. “Ni kweli! Naomba unisaidie. Mpaka nimekwambia hili ni kwamba ninahitaji msaada wako,” alisema Kareem. “Mmh! Hebu nikajifikirie, nitajua ni kipi tunachotakiwa kufanya,” alisema Al Khalid na kisha kuagana. 

Moyo wa Kareem ukarudi kwenye tumaini kubwa, akaona kwamba hatimaye angeweza kusaidiwa na rafiki huyo na kumtorosha Saida nchini humo. Aliporudi nyumbani, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuonana na msichana huyo kisha kuzungumza naye. Alimwambia mpango aliokuwa ameufanya wa kumtorosha nchini hapo pasipo mtu yeyote kugundua hilo. 

Saida akashusha pumzi, ni kweli alitamani kuondoka nchini humo lakini kitu kilichomtisha ni kwamba Kareem alilitoa jambo hilo nje ya nyumba yao, akahisi hapo ndipo kulipokuwa na tatizo. “Kareem, utamuamini vipi rafiki yako?” aliuliza Saida. “Usijali! Ni rafiki yangu sana, hawezi kufanya kitu chochote kibaya. Naomba umuamini!” alisema Kareem huku akimwangalia Saida. Walibaki sebuleni wakizungumza, walionekana kama marafiki wa kawaida na hakukuwa na kitu chochote kilichokuwa kikiendelea. 

Suala hilo bado liliendelea kuwa siri, hakukuwa na mtu yeyote ndani ya nyumba aliyelifahamu zaidi ya wao wawili. Ilipofika saa moja usiku, wazazi wake Kareem wakarudi nyumbani. Kila mmoja alibaki akisikilizia kuona kama mwezi uliandama au la! Kwa siku hiyo, redio zote nchini Oman zikiwemo TunIn Fm, Hi Fm na nyingine zilitangaza kwamba siku hiyo mwezi haukuwa umeandama hivyo ilikuwa ni lazima siku inayofuata kula ila siku nyingine inayofuata ni kufunga. 
“Kesho itatubidi twende kufanya manunuzi sokoni kwa ajili ya futari ya keshokutwa,” alisema mama yake. “Hakuna tatizo!” alijibu Kareem. Wakatulia sebuleni lakini muda mwingi Kareem na Saida walikuwa wakiangaliana kwa macho ya kimahaba. Ilipofika saa tatu usiku, wakasikia geti kubwa likigongwa. 

Kupitia kamera za CCTV zilizofungwa kila kona nyumbani humo, wakaliona gari la polisi likiwa limesimama nje ya geti. Kila mmoja akashtuka, halikuwa jambo la kawaida kwa polisi kufika nyumbani hapo, tena kwa usiku kama huo. Wakamwambia mlinzi afungue geti kwa rimoti maalumu, geti likafunguliwa na polisi wawili waliokuwa na silaha kuingia ndani. Wakamuulizia mzee Abdoulaziz, wakaambiwa yupo, wakaufuata mlango na kuingia na kuanza kugonga. Kareem akahisi kitu, harakaharaka akasimama kutoka kitini, akamshtua Saida naye asimame, akafanya hivyo na kuanza kuelekea chumbani. “Kuna nini?” aliuliza Saida. “Nina hofu na hawa polisi. Mungu wangu! Al Khalid atakuwa amewaambia polisi,” alisema Kareem huku akionekana kuchanganyikiwa. “Unasemaje?” “Nahisi itakuwa hivyo!” 

Wakati wakizungumza hivyo chumbani. Mara mlango wa chumba hicho ukaanza kugongwa. Kareem akajiuliza kama alitakiwa kuufungua au la. Wakati huo, Saida alikuwa akitetemeka mno chumbani humo, alitamani kufumba macho na kufumbua awepo nchini Tanzania. Wakati akijiuliza, akashtukia mlango ukipigwa teke, polisi wawili wakaingia chumbani humo. Hawakutaka kumkamata Kareem, walichokifanya ni kumchukua Saida. 
“Kuna nini?” aliuliza Kareem huku akijaribu kuwazuia wasimchukue mpenzi wake. “Taarifa zinasema ana mimba.” “Hapana! Hana mimba!” “Unabishana na wapelelezi wetu. Tumekuja na daktari kwa ajili ya vipimo,” alisema polisi mmoja. Wakatoka ndani ya chumba hicho huku wakiwa wamemfunga pingu Saida. 

Kareem alibaki akitetemeka. Saida alikuwa akilia kwa sauti, hakutaka kutoka ndani ya nyumba hiyo, hakutaka kumuacha mpenzi wake lakini kutokana na kutolewa kinguvu, hakuwa na jinsi. Wakamchukua na kumuingiza ndani ya gari, alikuwa akilia mno, polisi hao hawakutaka kujali, kwao, sheria ya nchi ilipewa kipaumbele kuliko kitu chochote kile. 

Gari likawashwa na kuondoka mahali hapo, lilipoelekea, lilikwenda katika kituo kikubwa cha polisi hapo Muscat kwa ajili ya kupelekwa mahakamani kesho asubuhi na mchana adhabu ya kupigwa mawe itolewe na kufanyiwa kazi hata kabla mfungo wa Ramadhani haujaanza. 

***************************
Al Khalid aliondoka katika Mgahawa wa Ya Sadeek. Moyo wake ulimuuma mno mara baada ya kuambiwa na Kareem kilichokuwa kimetokea. Moyoni mwake, kufuata misingi ya dini kilikuwa kitu cha kwanza kabisa, alikipa kipaumbele na ndicho kitu ambacho mara kwa mara aliwaambia wenzake kwamba walitakiwa kukifuata. 

Kitendo cha kuambiwa hivyo na Kareem kwamba alikuwa na msichana aliyempa ujauzito, moyo wake ulimuuma mno, aliona katika maono yake kwamba malaika wa shetani wakimfuata, wakamshika na kumuingiza katika shimo la moto kulipokuwa na mateso makubwa kutokana na kushiriki kitu ambacho aliamini ni dhambi kubwa mbele za Mungu.

Hakutaka kukubali, hakutaka kushiriki dhambi hiyo kubwa. Kwake, kudanganya na kusengenya zilionekana kuwa dhambi ndogo ambazo zisingekuingiza motoni kuliko kumpa mimba mwanamke hata kabla ya kuolewa. Moyo wake ulimfurukuta, akashindwa kula, akashindwa kupumzika, muda wote alikuwa akimfikiria Kareem. Hakutaka kuona akiendelea kushiriki dhambi hiyo, alichokifanya, tena kwa kusukumwa na sauti ambayo aliamini ni ya Mungu, akaenda kituo cha polisi na kutoa taarifa juu ya kilichokuwa kimetokea. 
“Una uhakika?” aliuliza polisi huku akimwangalia Al Khalid. “Ndiyo! Nina uhakika! Nimeamua kuja kuiosha mikono yangu kwa maji masafi, sitaki kushiriki kikombe hiki kilichojaa dhambi,” alisema Al Khalid huku akionekana kumaanisha alichokizungumza. 
“Safi sana...ukiwa unafanya hivi, unapata swawabu nyingi kwa Mungu! Tutakwenda huko na atakulinda katika maisha yako yote,” alisema polisi mmoja. 

Moyo wake ukawa na amani, hakujisikia mzigo wowote moyoni mwake, hakujihukumu kwani kile alichokifanya aliona kilikuwa kizuri na halikuwa jambo baya. Kareem alikuwa mkosaji kama wakosaji wengine hivyo serikali ilitakiwa kuchukua sheria mkononi kwa kwenda kumkamata msichana huyo, kwa mwanaume, hakutakiwa kukamatwa kwani hakukuwa na uhakika kama kweli mimba ile ilikuwa yake au ya mtu mwingine. 
Ila kwa mwanamke, hakukuwa na utetezi wowote ule.
Polisi wakafika huko na kumkamata Saida na kuondoka naye huku wakimuacha Kareem akiwa na mawazo tele. Kilichokuja moyoni mwake, ilikuwa ni lazima kumuokoa Saida, hakutaka kuona msichana huyo akifa na wakati alikuwa akimpenda na tumboni alikuwa na mtoto wake. 

Je, nini kitaendelea? Je, Saida atauawa kwa kupigwa mawe? Je ni nani alisema hatolia tena? Kwa nini aseme hivyo? Tukutane Saa Moja Usiku

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top