Unknown Unknown Author
Title: MAGUFULI: MIMI SIJARIBIWI NA WALA SITAJARIBIWA NA KATIKA UTAWALA WANGU HAKUNA KUMBEMBELEZANA
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
Rais Dk. John Magufuli, akihutubia wakazi wa Manyoni mkoani Singida jana baada ya kuwasili wilayani humo katika ziara ya kuwashukuru wan...
Rais Dk. John Magufuli
Rais Dk. John Magufuli, akihutubia wakazi wa Manyoni mkoani Singida jana baada ya kuwasili wilayani humo katika ziara ya kuwashukuru wananchi kwa kumchagua.

Na. Agatha Charles, 
KATIKA kile kilichoonekana wazi kukasirishwa na operesheni Ukuta iliyotangazwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) itakayokwenda sambamba na mikutano ya hadhara na maandamano nchi nzima, Rais John Magufuli amesema hajaribiwi na wala hataki nchi iingie kwenye vurugu, kwamba watakaokwenda kinyume na hapo atawashughulikia kikamilifu bila huruma.

Kauli hiyo ya Rais Magufuli imekuja ikiwa ni takribani mwezi mmoja Chadema kiingie kwenye operesheni hiyo waliyotangaza kuianza Septemba mosi mwaka huu kwa kile walichodai imelenga kukomesha matukio ya ukandamizaji wa haki na demokrasia.

Akizungumza jana Manyoni, mkoani Singida, Rais Magufuli ambaye yupo katika ziara ya siku nne katika mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga na Geita kwa lengo la kuwashukuru kwa kumpigia kura katika Uchaguzi Mkuu uliopita, alisema kwa sauti ya ukali huku akionekana kuwalenga viongozi wa juu wa Chadema kwamba wanaotetea maandamano watangulie wao halafu wataona cha mtema kuni.

“Nataka hao wanaotetea maandamano watangulie wao halafu wataona cha mtema kuni. Wasiwatangulize watoto wa masikini, wao wanakaa gesti wanalala, watoto wa masikini wanawapa viroba tangulieni huko, watangulie wao. Na mimi nataka watangulie wao siku waliyoipanga. Nataka nchi yenye nidhamu tutekeleze majukumu yetu tuliyoyapanga kwa ajili ya nchi hii.
“Lakini najua wakati mwingine ukikutana na nyoka ukampiga ukamuua, mkia lazima utikisike tu, unaweza kufikiri ni mzima kumbe nyoka alishakufa. Vyama vyenyewe (vya upinzani) vimechoka, wananchi wameshaona,” alisema.
Rais Magufuli ambaye ameambatana na mkewe Janeth, aliwaonya viongozi hao wa vyama vya upinzani wanaohamasisha maandamano na mikutano akisema wasije wakamjaribu na kwamba yeye si mtu wa kujaribiwa.
“Sitaki nchi hii iwe ya vurugu, watakaoleta vurugu mimi nitawashughulikia kikamilifu bila huruma na wasije wakanijaribu, mimi ni tofauti sana na kama wapo watu wanaowatumia wakawaeleze vizuri, mimi sijaribiwi na wala sitajaribiwa,”
“Tunataka nchi iende mbele, wananchi hawa wana shida na siasa nzuri ni wananchi washibe, siasa nzuri ni wananchi wetu wapate madawa, siasa nzuri ni wananchi wetu wapate elimu bila kusumbuliwa sumbuliwa na siasa nzuri ni wananchi wetu wapate maisha mazuri. Hicho ndicho nilichoahidi na mimi sitaki mtu yeyote anicheleweshe,” alisema Rais Magufuli.
Alisema wapo watu ambao yakitolewa maamuzi wanapotosha na kutaka wabembelezwe na kusisitiza kuwa katika uongozi wake hilo halipo.
“Wengine nikitoa maamuzi hayo wanabadilisha maneno, walizoea vitu vya kubembelezana bembelezana, wanasema tunaandamana unambembeleza! Kaandamane ukione,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli aliwasihi Watanzania kufanya kazi kwa juhudi na kujiepusha na vitendo vya vurugu vinavyohamasishwa na baadhi ya wanasiasa huku akionya kuwa Serikali yake haitamvumilia yeyote ambaye atathubutu kuchochea vurugu ikiwemo maandamano kinyume cha sheria.

Katika hilo Rais Magufuli alitangaza utaratibu mpya wa kufanya mikutano akisema wanasiasa waliochaguliwa na wananchi ndio wanaopaswa kufanya siasa za maendeleo katika maeneo yao na si kutoka sehemu moja kwenda eneo lingine.

Kuhusu suala la Serikali kuhamia Dodoma, Rais Magufuli alisema watakaoshindwa kuhamia katika mji mkuu huo wajiandae kuacha kazi na kwamba atahakikisha anauza majengo ya wizara mbalimbali yaliyopo Dar es Salaam kwa mnada ili wasiotaka kuhama wahame kwa lazima.

“Atakayeamua kubaki mule atabaki peke yake na nikishahamia huku yeye bado yuko kule atabaki kule hana kazi na mshahara hamna, ni lazima tufike mahali Tanzania tuamue, Dodoma pazuri wakitaka wakajifunze hata Kigogo,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli ambaye hii ni ziara yake ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa CCM Jumamosi iliyopita, alishangaa kuona agizo la kuhamia Dodoma lilishindikana kutekelezwa kwa muda wa miaka 50 licha ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuwahi kulizungumzia.
“Ni nchi gani hii ambayo mnatoa maamuzi ya miaka 50 hamtaki kutekeleza, Baba wa Taifa alizungumza mpaka ametangulia mbele ya haki sisi hatutekelezi, si mimi, mimi watahama, watahama na wasiohama wajiandae kuacha kazi kwa sababu wafanyakazi wapo wengi wa kufanya kazi, hiyo ndiyo Serikali yangu,” alisisitiza Rais Magufuli.
Rais Magufuli alitumia hadhara hiyo pia kuzungumzia hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali yake ya awamu ya tano tangu aingie madarakani Novemba mwaka jana.

Alizitaja hatua alizozichukua kuwa ni pamoja na kufuta ada kwa shule za msingi na sekondari za Serikali, kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu zaidi ya 100,000 pamoja na kuongeza fedha za miradi ya maendeleo katika bajeti ya Serikali kutoka asilimia 26 ya mwaka 2015/2016 hadi kufikia asilimia 40 katika bajeti ya mwaka huu 2016/2017.

Hatua nyingine zilizochukuliwa ni pamoja na kuondoa wafanyakazi hewa 12,500 katika orodha ya waliokuwa wanalipwa mshahara na Serikali, kudhibiti upotevu wa mapato serikalini na kutenga shilingi trilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa yaani standard gauge.

Pamoja na hayo, Rais Magufuli alizungumzia pia hatua zilizochukuliwa dhidi ya wala rushwa na wanaojihusisha na ufisadi kwa kuunda mahakama ya mafisadi huku akiapa kuwa katika kipindi chake hakuna fisadi atakayeendelea kutamba.

CHANZO : MTANZANIA

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top