Msanii wa muziki wa Pop, Mtanzania Dati, akiongea na Waandishi wa habari katika Ukumbi Denfrance, Sinza-White Inn.
Dati akiulizwa swali na waandishi wa habari.
Msanii wa muziki wa Pop RnB, Mtanzania mwenye maskani yake nchini Sweden ,Khairat Carlo Omar, ’Dati’ anatarajiwa kupiga shoo jukwaa moja na staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ nchini Sweden hivi karibuni.
Dati ambaye kwa sasa yupo nchini kwa ajili kusambaza video ya wimbo wake mpya wa Can Do iliyopikwa na Prodyuza Fundi Samweli na video kufanywa na Khalfan na Hanscana amesema mipango yote imeenda sawa na anatakiwa kurudi Sweeden kwa ajili ya shoo hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar leo Jumapili, Dati alisema kuwa alikuja nchini kwa ajili ya likizo fupi ndipo akapewa taarifa ya kuhitajika kwenye shoo hiyo ambapo alikubali bila kinyongo.
“Nimefurahi kufanya shoo jukwaa moja na Diamond kwani ni msanii mkubwa ndani na nje ya nchi yetu ya Tanzania pia amekuwa akifanya poa kila siku kwa kuchukua tuzo mbalimbali, kwa upande wangu ni nafasi nzuri ya kunitangaza zaidi kimataifa na kuitangaza nchini yangu,” alisema Dati.
Diamond anayebamba na Wimbo wa Utanipenda anatarajia pia kupiga shoo Krismasi hii (Desemba 25), ndani ya Uwanja wa Taifa, Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem jijini Dar.
(Picha, habari: Deogratius Mongela/ GPL)