NIJUZE NIJUZE Author
Title: YANGA SC YAMKALIA KOONI STEWART HALL, YATAKA AONDOKE NCHINI KAMA ASIPOSIBITISHA HAYA
Author: NIJUZE
Rating 5 of 5 Des:
Kocha wa Azam FC, Stewart Hall. Khadija Mngwai na Mohammed Mdose, Dar es Salaam UONGOZI wa Klabu ya Yanga umedhamiria kumuondoa nchini ...
Stewart Hall
Kocha wa Azam FC, Stewart Hall.
Khadija Mngwai na Mohammed Mdose, Dar es Salaam
UONGOZI wa Klabu ya Yanga umedhamiria kumuondoa nchini Kocha wa Azam FC, Stewart Hall, kwa kutaka Bodi ya Ligi kuvunja mkataba wake wa kuifundisha Azam FC, iwapo hatathibitisha madai ya rushwa aliyoyasema katika mechi iliyowakutanisha Jumamosi iliyopita.

Stewart Hall, raia wa Uingereza, alitoa tuhuma hizo kufuatia penalti waliyopewa Yanga dakika za mwisho iliyotokana na kipa, Aishi Manula, kugongana na kiungo mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva.

Akizungumza na Championi Jumatano, Katibu Mkuu wa Yanga, Jonas Tiboroha, amefunguka kwa kusema, Stewart anatakiwa athibitishe madai yake ya rushwa aliyoyatoa katika mchezo huo na kudai kuwa watalifikisha suala hilo kwenye Bodi ya Ligi na iwapo atashindwa kuthibitisha, basi kibali chake cha kufundisha soka hapa nchini kiondolewe.
“Tunatarajia kuandika barua Bodi ya Ligi kwa ajili ya kumshitaki Stewart ili aweze kuthibitisha madai yake kuhusu rushwa aliyosema kwani hilo ni kosa kisheria na atueleze ni nani aliyeitoa na iwapo hatatoa vielelezo, inabiti tuchukue hatua zaidi.

“Tunataka kibali chake cha kufundisha soka hapa nchini kiondolewe, yeye ni kocha mgeni na anatakiwa aondoke hapa nchini na huo ndiyo msimamo wetu kama Yanga, tunataka aachane na soka letu, kwani atakuja kutuharibia".

“Tuhuma zilizotolewa si sahihi, wao walikuja kwa ajili ya rafu na sisi tulikwenda kwa ajili ya ushindi, kuna wachezaji wetu watatu walitoka nje baada ya kuchezewa rafu lakini hakuna kadi yoyote iliyotolewa, pia kipa wao Manula alimchezea rafu Msuva na alitakiwa kupewa kadi nyekundu lakini hakupewa na imetolewa penalti analalamika".

“Stewart anatakiwa awe na busara, timu yake ya Azam inafanya mambo mengi ambayo siyo mazuri katika soka letu na akiendelea na hali hiyo, tutayasema yote yanayofanywa na viongozi wa timu yake.
“Anatakiwa kuheshimu makocha wazawa na soka letu kwa ujumla, kwanza ni mtu mwenye bahati kuendelea kufundisha Bongo kwa kuwa hakuna kitu chochote kipya alichokifanya hapa nchini.

“Tunashangaa Stewart alipewa kadi ya kutokaa kwenye benchi katika mchezo wetu lakini ameingia kwenye ‘Conference Room’ kuzungumza na waandishi pamoja na kutukana, licha ya kujua kuwa ni kosa na TFF wamekaa kimya,” alisema Tiboroha.

Hata hivyo, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura, amesema bodi hiyo itakaa na kuchunguza tukio hilo kwani kiutaratibu alitakiwa kupeleka malalamiko yake kwenye bodi hiyo.
“Kwanza hakutakiwa kuongea tu kwani kwa sasa kuna utaratibu wa kupokea malalamiko na kuyafanyia kazi, Kamati ya Masaa 72, itakaa kupitia mechi nzima na pia tunaweza kumuita ili atoe ushahidi kwani tuhuma za rushwa siyo kitu kidogo, unatakiwa uwe na ushahidi kamili,” alisema Wambura.

About Author

Advertisement

 
Top