Unknown Unknown Author
Title: POLISI WAKINUSURU KITUO CHA POLISI KUVMIWA, WALAZIMIKA KUTUMIA MABOMU
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama. Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, limelazimika kutumia mabomu ya machozi na silaha za m...
Leonidas Gama
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama.

Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, limelazimika kutumia mabomu ya machozi na silaha za moto, kuzima maandamano ya wafugaji wa jamii ya Kimasai kutoka mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, waliokuwa wamejipanga kuvamia Kituo Kikuu cha Polisi Sanya Juu, Wilaya ya Siha mkoani hapa.

Wafugaji hao wanadaiwa walikuwa wakishinikiza kiongozi wao anayeshikiliwa (jina halijafahamika), kuachiwa na Polisi Wilaya ya Siha.

Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kutoka Mjini Moshi waliokuwa na magari manne, walilazimika kutumia nguvu walipokutana na wafugaji hao wakiwa wamefika eneo la mwisho wa lami njia panda ya Karansi na Magadini, Wilaya ya Siha wakielekea kilipo kituo hicho umbali wa kilomita tano.

Habari zilizopatikana jana na baadaye kuthibitishwa kwa njia ya simu na Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Geofrey Kamwela, zilisema makundi ya wafugaji hao yaliingia Wilaya ya Siha kwa nyakati tofauti yakitumia malori, pikipiki aina ya bajaj, bodaboda na magari ya kukodi.

“Kwa sasa niko Siha kwenye operesheni maalum baada ya kuwatawanya wafugaji kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro. Bahati nzuri tumefanikiwa kuzima maandamano hayo yaliyokuwa na lengo la kuvamia Kituo cha Polisi, na hivi sasa tunakusanya taarifa za kiuchunguzi kwa hiyo kesho au baadaye nitatoa taarifa ya kilichotokea,” alisema Kamanda Kamwela.

Kwa mujibu wa Kamanda Kamwela, wafugaji hao ambao idadi yao hadi sasa haijajulikana, licha ya kuingia mkoani hapa wakitokea mikoa hiyo ya jirani kwa ajili ya kuunganisha nguvu na wenzao wa Wilaya ya Siha kutafuta malisho ya mifugo yao, walikuwa wakitumia mbinu mbalimbali kuwakwepa Polisi.

Novemba 14, mwaka jana, vurugu kama hizo zilizuka kati ya wafugaji wa jamii ya Kimasai wa Wilaya za Siha mkoani Kilimanjaro na mikoa ya Arusha na Manyara baada ya kuvamia na kuteketeza kwa moto hoteli ya kitalii ya Ndarakwai na kambi sita zinazolaza watalii.

Uvamizi huo ulisababisha zaidi ya vyumba 300, mali mbalimbali za mwekezaji wa Kampuni ya Tanganyika Films & Safari inayomilikiwa na Peter Jones, raia wa Uingereza ambaye anajishughulisha na utalii wa picha na uhifadhi wa mazingira, kuteketezwa kwa moto.

Kambi zilizotekezwa na wafugaji waliodaiwa kuvamia eneo la mwekezaji huyo Novemba mwaka jana, ni Ndarakuwai, Kiseriani, Kambi ya Kati, Karakana, Casablanca na Rafiki.

Kambi hizo zilikuwa na uwezo wa kupokea wageni kati ya 2,500 hadi 3,000 kwa mwaka kutoka mataifa mbalimbali.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, akizungumza jana kwa njia ya simu alisema kama wafugaji hao walikuwa wanataka kiongozi wao aachiwe na Polisi, walipaswa kufuata utaratibu wa kumwekea dhamana na si kufanya maandamano ambayo yanaweza kuvunja amani.

“Mimi niko kwenye maandalizi ya kumpokea Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, na sijapata taarifa ila hao wafugaji walipaswa kufuata sheria kwa kumwekea dhamana huyo anayeshikiliwa na Polisi, si kuandamana kwa sababu huko ni kuvunja amani…nakuomba jaribu kumtafuta RPC (Kamanda wa Polisi) yeye atakupa taarifa za uhakika,” alisema Gama.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Siha, Dk. Charles Mlingwa, ambaye pia ni Mkuu wa wilaya hiyo, alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo alisema:

“Wilaya yangu iko vizuri, naamini hizo ni operesheni za Polisi na itapendeza zaidi ukiwasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa.”

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top