Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
Wakazi wa mkoa wa Lindi wametakiwa kutodanganyika na kundi la watu wachache wanaotaka kuvuruga amani iliyopo bali waitunze na kuhakikisha kuwa haipotei kwani amani ikitoweka hao wanaowadanyanga watakimbia na kuwaacha wakiteseka .
Wito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa wakati wa uzinduzi wa sherehe za kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinnduzi (CCM) mkoani Lindi zilizofanyika katika kata ya Kiwalala wilaya ya Lindi vijijini ambapo chama hicho kinatimiza miaka 37.
Mama Kikwete alisema CCM imefanya mambo mengi katika harakati za ukombozi Barani Afrika kwani Tanzania ilikuwa kimbilio la wanyonge kwa kuwa wapigania uhuru wengi kutoka nchi za Kusini mwa Afrika ambazo hazikuwa zimepata uhuru walipokelewa , walihifadhiwa , walisaidiwa na kuwakarimu kwa dhati jambo ambalo si dogo na hii yote ilitokana na amani iliyopo.
“Chama chetu kimefanya mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuleta Demokrasia ya vyama vingi toka mwaka 1992 na leo hii tunatimiza miaka 22 ndani ya mfumo wa vyama vingi huku tukiwa na amani, umoja na ushikamano miongoni mwa watanzania, tumeleta usawa kwa wananchi wote bila kujali jinsia, rangi kabila wala dini.
Chama cha Mapinduzi kupitia Serikali zake zinawajali wananchi kwa kuwasogezea huduma mbalimbali za kijamii hadi vijijini na kupanua fursa za kiuchumi na kimaendeleo kwa wananchi”, alisema Mke wa Rais.
Aidha Mjumbe huyo wa NEC pia aliwataka wananchi hao kujishughulisha na kazi mbalimbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na kulima japo mazao ya chakula kama muhogo kwani Serikali tayari imeshafanyia mambo mengi ya maana ambayo yanawasaidia katika shughuli zao za maendeleo.
Mama Kikwete alisema, “Serikali imejenga Shule, Hospitali, barabara na kuimarisha miundombinu ya barabara na leo hii kama mtalima kwa bidii mtaweza kusafirisha na kuuza mazao yenu mbali na hapa kwakuwa barabara ni nzuri na usafiri ni wa uhakika”.
Kwa upande wake Mlezi wa Chama hicho katika mkoa wa Lindi Dk. Maua Daftari aliwataka wanachama wa chama hicho kuwa na umoja na mshikamano kwa kufanya hivyo wataweza kushinda na kutekeleza ilani ya chama chao.
Katika uzinduzi wa sherehe hizo ambazo kilele chake kitafanyika leo katika wilaya ya Ruangwa jumla ya wanachama 17 walijiunga na chama hicho ambapo wanachama wapya ni 12, kutoka chama cha upinzani cha Civic United Front(CUF) wanne na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mmoja.
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.