YANGA U20 YAICHAPA COASTAL UNION U20 1-0

clip_image001
LEO vijana wa Coastal Union wamekubali uteja kwa kuchapwa bao 1-0 na vijana wa Yanga kwenye michuano ya Uhai inayoshirikisha timu za vijana zinazoshiriki Ligi kuu ya Vodacom, katika uwanja wa Karume Ilala jijini Dar es salaam.

Mechi hiyo ilichezwa asubuhi saa mbili na kukamilika saa tatu na nusu, ilianza kwa timu zote kucheza kwa kujihami kipindi kizima cha kwanza.

Kipindi cha pili kilianza kwa Coastal Union kulikamia lango la Yanga lakini mabeki wa timu hiyo walikuwa makini kuhakikisha golikipa wao hapati kashkash zozote.

Ilipofika dakika ya 65 Yanga waliliandama lango la Coastal Union hali iliyowafanya mabeki wa pembeni kupoteza mwelekeo hasa beki wa kulia Aoub, alionekana kuzidiwa nguvu.

Ilipofika dakika ya 68 Hamis Issa wa Yanga aliipatia bao la kwanza na la pekee katika mechi ya leo baada ya piga nikupige katika lango la Wagosi na kumuacha golikipa akiwa peke yake mabeki wameanguka pembeni.

Kutokana na matokeo hayo Yanga wamejizolea pointi sita na mabao mawili baada ya mechi ya kwanza kuwafunga Mbeya City bao 1-0. Coastal Union wataendelea kubaki na point tatu na mabao mawili baada ya mechi ya juzi kuwafunga mabingwa watetezi wa michuano hiyo Azam FC mabao 2-1 katika uwanja huohuo wa Karume.

Mechi ijayo ya Coastal Union katika kundi lao itachezwa katika uwanja wa Chamazi Saa kumi alasiri siku ya Jumamosi Novemba 23.

Hii ni mara ya pili Coastal Union, wanashiriki michuano hiyo ya Uhai ambapo mwaka jana walifika mpaka hatua ya fainali wakatolewa kwa matuta na Azam FC.

Post a Comment

Hii ni Blog kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Nchi yetu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...

Previous Post Next Post