RIWAYA: SITAISAHAU FACEBOOK
MTUNZI: EMMY JOHN PEARSON
SIMU: 0654960040
SEHEMU YA KUMI NA TISA
Tulilolifanya hapo lilikuwa kosa kubwa sana. Alama za 666 zilizokuwa zinaanguka katika mfumo wa vipande v ya nyama. Ukaleta balaa.
Joka kubwa kuliko lile la awali likaibuka. Joka hili sasa lilikuwa halijulikani wapi mbele na wapi nyuma.
Lilikuwa na vichwa viwili. Mbele na nyuma.
Halikujulikana linatambaa kwenda kaskazini ama kusini, magharibi wala mashariki.
Yule bingwa wa mapambano Samson akajikuta analiachia jambia lake, Jenny aliyekuwa anaanza kunogewa na shughuli ya kukata nyama za watu naye akatulia tuli.
Nami nikakumbwa na uoga na nikakiona kifo kikibisha hodi.
Isabela nakufa!! Nakufa nikiwa katika u…”
Kabla sijamaliza kuwazua. Ghafla……..Ghafla!!!!!
Ilikuwa ghafla sana!!!!
Joka lilijinyanyua juu. Sote tukawa chini yake. Joka lenye rangi ya dhahabu!! Sasa ikawa patashika kila mtu analazimisha kujificha nyuma ya mwenzake. Hakuna aliyetaka kufa. Mimi, Jenipher na wale wengine waliokuwa wanatambua yule nyoka amekuja kufanya nini pale tulijiweka mbali na vile vipande vya zile nyama zenye namba 666.
Joka likavimba kama linataka kutema sumu. Likavimba zaidi kama linataka kupasuka. Hatimaye likautoa ulimi nje. Likatanua mdomo kama linataka kutumeza sote. Kisu chan gu bado kilikuwa mkononi.
Mara likajirusha na kujizungusha kama pangaboi. Hapa hakuna kitu kilichosalia. Kila mmoja wetu alirushwa mbali kabisa. Mimi sikuumia lakini wenzangu waliumizwa.
Nilipogeuka nilimwona kiumbe akiwa amelowa damu akiwa na jambia mkononi. Alikuwa akikimbia mahali ambapo joka lipo. Alikuwa ni Samson yule jasiri wa kisukuma.
Macho yako yalifumba kisha yalipofumbua alikuwa ameingia mzimamzima katika kinywa cha yule nyoka. Jambia na yeye wakawa wamemezwa.
Hali ya hatari!! Nilijitahadharisha.
Joka lilikuwa linameza vile vipande vya mabaki ya nyama yenye chapa ya 666. Ndipo hapa nilimuona tena yule Osmani aliyetambuliwa kama waziri wa miundombinu. Nikakumbuka kuwa ni huyu bwana nimeambiwa kuwa anazijua njia zote za kutoka katika mji huu wa kishetani. Nikamnyemelea huku nikiwa makini na yule joka na pia nikiwa makini asiweze kuhisi chochote kile.
Nikamfikia nikamkaba shingoni. Nilikuwa na nguvu za ajabu sana. Nikamvuta hadi katika kichaka nilichokuwa nimejihifadhi hapo.
Hakuwa ananiona!! Jambo hilo lilinipa nafasi nzuri ya kumtawala. Kwa ukombozi wa wengi na kujitoa katika adha ya kufia katika mji huo. Nikanyanyua kisu changu nikazamisha katika paja lake. Akatoa kilio kikubwa sana. Kilio kile kikasababisha lile joka linyanyuke mara moja. Likaanza kuangaza huku na huko. Nami nikatulia tulii kuangalia nini kinatokea. Joka likanyanyuka kisha likatanua midomo yake. Kisha likionekana dhahiri kuwa na hasira lilitapika. Maajabu!! Samson yule jasiri katika vita hiyo akatangulia kisha jambia lake likafuata.
“Njia ya kutoka hapa ni ipi?” nilimuuliza Osman huku bado akiwa katika himaya yangu.
“Sijui.” Akanijibu kwa jeuri. Nikamchoma tena kisu katika sehemu ileile kilipopitia awali.
“Nasemaaaaa!” akapiga kelele.
“Dakika moja tu nakupa sema upesi.”
Osman akaanza kutoa maelekezo ya namna gani ya kutoka katika kijiji hicho cha maajabu!!
Maelezo yalikuwa yamenyooka!! Japo yalikuwa na masharti. Sikuwa na budi kuendelea kumshikilia. Ni huyu angetuwezesha kutoka.
Joka lilizidi kuhangaika.
Sasa lilitazama mahali alipokuwa Osmani na mimi. Likatambaa kwa hasira kali sana likawa linatufuata. Nikajikuta namuiachia Osmani. Nikaanza kukimbia. Joka likawa linaufuata uelekeo wangu.
Mungu wangu!! Kumbe linaniona sasa hivi. Nimekwisha.
Nilizidi kutimua mbio. Hatimaye mbio za sakafuni zikaishia
ukingoni! Nikaanguka chini. Joka nalo hilo likanifikia.
Likaachama mdomo wake mkubwa.
Sasa nakufa! Nilikubali yaishe.
Achaaaaaa!! Nilipiga kelele za mwisho za kutokwa na roho. Huku nikitegemea zitakuwa kelele za mwisho. Haikuwa hivyo. Niliweza kuwa hai tena. Joka lilikuwa limeufumba mdomo wake. Likatulia tuli.
Nikaduwaa kulikoni nyoka huyu hajanimeza. Au! Au! …nikakosa majibu.
Joka likaendelea kutulia kama lina urafiki na mimi. Kwa uoga nikasimama na kuanza kutambaa taratibu. Joka limetulia halina habari. Nikasimama. Bado tuli! Nikaanza kuondoka hadi nikatokomea! Nyoka ametulia.
Maajabu makubwa sana haya!!
*****
Nilirejea hadi kule walipokuwa wanakijiji wenzangu. Osmani alikuwa amehitisha mkutano tena. Alionekana mwenye furaha sana na ni kama alikuwa anatoa karipio kali.
Samson niliyedhani amekufa kumbe alikuwa amezimia tu baada ya kutemwa na yule nyoka. Nilimkuta akiwa amefungwa kamba nyingi sana. Bila shaka adhabu yake ilikuwa imewadia.
Nilimuona Jesca pia. Lakini John pekee ndio nilikuwa sijamuona.
Nilikuwa na hasira. Nikatumia ule mwanya wa joka kutulia. Nikamvamia Osmani. Nikamkaba tena. Safari hii sikutaka mambo mengi sana, nilihitaji njia ya kutokea.
“Wakati wa kuwa watumwa wa shetani umekwisha. Tunatakiwa kuishi maisha yetu tuliyoshi awali. Manyanyaso haya yote na yasiendelee. Tusikubali kabisa uonevu huu. Sasa tunatoka humu. Kila mwenye nia na aungane nami sasa. Tunatokaa!!” niliunguruma kwa sauti kuu. Wale wasiokuwa na Chapa walinisikia na kuniona. Wale waliokuwanayo waliduwaa wasijue kinachoendelea.
Samson alifunguliwa kamba alizokuwa amefungwa. Sasa Osmani akawa anatuongoza kuielekea njia ya kutokea.
Chapa ya 666 ilikuwa katika mkono wake wa kuume.
Kijiji kilikuwa kikubwa sana. Tulipenyeza njia hadi njia bado hatukufika tulipokuwa tunahitaji.
Sasa tulifika mahali palipokuwa na majani makavu lakini laini sana. Tulipokuwa pale. Osmani akaniponyoka. Kisha akapiga mluzi fulani hivi. Wakatokeza kenge wa ajabu. Wakubwa kama mamba. Walikuwa wanne. Na dhahiri walikuwa na njaa. Walishambulia katika namna yha ajabu na upesi sana.
Waliua! Watu kumi wakaanguka chini. Mamba wale badala ya kula nyama wakawa wananyonya damu.
Ilikuwa zamu yangu sasa. Osmani alikuwa pembeni akitucheka. Kuna unga fulani alijipaka usoni, sasa aliweza kuniona vizuri.
“Achaaaa!!” nilijikuta natamka neno lililoniokoa midomoni mwa joka lile kuu. Kenge hawa wa ajabu wakatulia palepale wakafunga vinywa vyao. Osmani akashangaa na mimi pia nikashangaa.
Samson ambaye naye alikuwa amekata tamaa alishangaa.
Nikawahi kuipoteza hali yangu ya kushangaa. Nikamwendea Osmani. Nikamkaba tena. Nikampiga makofi mawili akaanza kutema damu.
“Njia ya kutokea!!” niliamuru.
Akageuka, akatunyooshea mkono. Palikuwa na mlango mdogo wa mbao zilizooza. Nikawaamuru wanakijiji wsaliosalia wapite. Wakapita!!
Hadi walipomalizika ndipo mimi na Osmani tulipita. Kabla hatujamaliza kupitia nilisikia kilio kikubwa. Kuna mtu alikuwa akiniita.
Sauti ile ilikuwa ya John!
Nikasita kutoka. Nikarejea nyuma niweze kuchungulia.
John alikuwa anagalagazwa na lile joka kubwa.
Huruma na mapenzi yangu kwa John ikanijia. Nikaweka kando yote aliyowahi kunitendea. Nikarudi kwa kasi. Neno acha likiwa mdomoni mwangu. N ilipofika nikaamuru kwa sauti kuu. Joka lile likatii kwa nidhamu. Nikaduwaa. Nikamchukua John na kuanza tena kuitafuta njia ya kutokea.
Kosa kubwa! Nilimuacha mbali waziri wa miundombinu!
Osmani akawa amepotea! Sikujua ni wapi pa kupita.
John hakuwa akiniona wala kunisikia. Nilitamani ajue ni mimi nipo naye. Lakini haikuwa hivyo.
Nilifanikiwa kukipata kisu. Nikaamini sasa nitaiondoa alama ya 666 katika mwili wake na ataweza tena kuona.
Hofu! Na kukata tamaa. John alikuwa na alama ile shingoni mwake. Mwili ukafadhaika.
Siwezi kumchinja John!! Siwezi!! Niliapa.
Lakini nitafanya nini sasa.
Kitu kama tetemeko la ardhi likatwaa mawazo yangu. Nikamvuta John asiyejielewa nikamkumbatia. Tetemeko hilo lilivyopita hapakuwa tena na lile joka.
Lakini kitu kipya kikajitokeza. Ulikuwa mwanga mkali kama jua vile!! Nikatafakari ni kitu gani hicho. Sikuweza kutambua.
Mara ule mwanga ukapotea. Nikaja kushtuka nimepigwa kibao katika shavu langu. Nikaanguka.
Niliposimama nikapigwa tena, na sikumuona kiumbe aliyekuwa ananifanyia hivyo.
Mapigo yakaongezeka. Nikawa navuja damu.
Sikuweza kusimama tena.
Sauti ya Jenipher ikanijia kichwani, “Ukinywa damu unakuwa kama wao!!”
Maneno hayo yakanifanya nipatwe na ari mpya. Nikatambaa nikamfikia John.
Badala ya kumchinja! Nitamnyonya damu walau kidogo tu.
Nikamfikia. Nikamkamata. Akaanguka chini, nikajirusha shingoni mwake. Nilipoifikia shingo yake nikamkumbuka yule mganga wa kinaijeria. Hapo sasa nikakumbuka sio mara yangu ya kwanza kunywa damu. Nikapenyeza meno yangu pale pale kwenye alama ya 666 aliyopigwa shingoni.
Damu ikaanza kutoka. Nikaimeza huku nikiwa nimeikunja sura yangu.
Nguvu za ajabu zikaniijia.
Amakweli wa giza pambana naye kigizagiza.
Sasa niliweza kumuona adui yangu aliporejea tena. Alikuwa ni Dokta tuliyekutana katika mtandao, alikuwa ni Dokta Davis.
Alikuwa ananisogelea tena aweze kunipiga. Nikaudaka mkono wake. Akataka kujitoa hakuweza. Nikaweka sawa kisu changu nilichokuwa nimekificha kwa nyuma. Nikazamisha katika sehemu zake za siri huku nikipiga kelele.
Akaanguka chini na kuanza kujirusharusha.
Nikamkumbuka yule ninja wa kisukuma, Samson ambavyo hakuwa na huruma. Na mimi nikamuiga. Nikamrukia Davis na kuanza kumchoma visu.
Nilimchoma kwa fujo zote.
Nikafadhaishwa baada ya yule Davis ambaye sasa niliamini naenda kummalizia alipogeuka kuwa joka kubwa la kijani. Haraka nikawahi kujitoa lakini nilikuwa nimechelewa sana. Joka lile likawahi kujiviringisha kuanzia kiunoni likawa linapanda juu. Sasa lilikuwa limenifunga hadi kifuani.
Ajabu!! Lilikuwa linawasha sana nilitamani kujikuna lakini haikuwezekana na mikono ilikuwa imefungwa tayari.
Nililiamuru liniachie lakini halikuiheshimu amri yangu. Nikazidi kuwashwa, nikajaribu kujigalagaza, haikuwezekana. Sasa likaanza kujikaza, muwasho ukaenda likizo, maumivu yakaingia kati. Lilizidi kukaza, mara likaongeza kujiviringisha hadi likaniziba usoni. Kifo kikanukia harufu ya kukera.
Nikabaki jicho moja tu kuona nje!! Viungo vingine vyote vilikuwa vimefunikwa. Sikuwa na ujanja. Jicho langu likamuona John akiwa ameshangaa kama tahira. Nilijaribu kutoa sauti haikutoka, nilikuwa namwomba John kwa mara ya mwisho aweze kuniokoa. Hakuweza kunisikia.
Nikatazama juu nikakutana na mawingu yenye rangi inayoshabihiana na buluu, nikaikumbuka rangi ya mtandao wa kijamii. Ni huku nilikutana na Dokta Davis. Akanipa zawadi ya utajiri, akanipatia kazi nyepesi inayonipatia kipato kikubwa. Nikamuamini sana. Sasa alikuwa amegeuka joka kubwa na lilikuwa linaniua.
Hakika lazima nife!! Jitihada zangu zote hazikuwa na maana tena.
John hakuwa msaada wowote kwangu. Na hakuwepo mwingine wa kunipa msaada.
Nilipofikiria ni nani mwingine wa kunisaidia akili yangu ikarejea kwa mwalimu Nchimbi. Mama yangu mzazi. Nikajaribu kuita sauti haikutoka. Mama naye hakuwa na msaada katika hali hii.
Nikayakumbuka maneno ya mama. Miaka mingi sana nikiwa mdogo aliwahi kunikambia maneno.
“Yupo mtu anakusikia hata usipotoa sauti.” Hili lilikuwa jibu alilonipa baada ya kumuuliza iwapo mabubu na viziwi wanaweza kuzungumza na Mungu. Jibu lake hadi ukubwani halikunitoka.
Nami sasa nilikuwa bubu. Jaribio la mwisho kabisa ni kuzungumza na yule anayesikia wakati wote. Ajuaye unachokiwaza. Kila wakati, mahali popote.
Mungu! MUNGU PEKEE!!
“Eeh! Baba sijui kama nilistahili adhabu hii. Na kama ilikuwa stahili yangu baba. Nichukue kwako sasa. Nimeumia na IMETOSHA.” Nilizungumza katika nafsi yangu. Kisha nikasubiri kuiaga dunia hii chungu.
**Hatariii.......
NINI KITAJIRI.....ISABELLA AMEMKUMBUKA Mungu!!!
RIWAYA HII INAPATIKANA YOTE KUANZIA MWANZO HADI MWISHO KWA WANAOHITAJI.....GHARAMA 3000/ Wasiliana na Emmy...0654 960040
ITAENDELEA
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.