RIWAYA: SITAISAHAU facebook
MTUNZI: EMMY JOHN P.
SEHEMU YA ISHIRINI NA MBILI
John alikuwa ananiona? Nilijiuliza.
Lile joto likazidi. Abiria wakashuka garini.
Kuna kitu hapa!! Mapambano mapya!! Nikajisemea huku nikiendelea kumzuia John.
John sasa akanizidi nguvu.
Akanitoka. Akashuka chini. Nikajaribu kumkimbilia.
Huko nikamkuta akiwa anafanya jambo la ajabu. John alikuwa anajarfibu kuisukuma gari kwa kuitikisa.
Ajabu! Ikaanza kutikisika kweli. Mtikisiko ule ukawashtua wengi. Sasa vilio vikaanza kusikika. Kila mtu kuitetea nafsi yake.
Watu wakashuka upesi kwa kugombania mlango. Basi likaanguka.
Lilipoanguka John akatazama mahali. Na mimi nikageuza jicho kutazama. Yalikuwa makaburi
Makaburi yaliyo na historia ya kushangaza. Makaburi ambayo yalimtoa nishai mchina alipojaribu kupitisha umeme juu yake. Umeme ukagoma kuwaka.
Haya yalikuwa makaburi ya Kiyeyeu.
Yalikuwa yanafuka moshi wa dhahabu!!
Vita!!
Mayowe yakatawala, akinamama wakiwa wamesahau watoto wao na wanaume nao wakiwasahau wake zao sasa kila mmoja alikuwa akiipigania nafsi yake. Sikuwa katika umoja na akina Jesca tena! Hapa sasa kila mwenye macho hakungoja kuambiwa tazama!!
Makaburi yale mawili yaliendelea kufuka ule moshi wa rangi ya dhahabu.
Wenyeji wa kijiji kile walikuwa katika taharuki kubwa sana huku wakizungumzia juu ya kukasirika kwa mizimu.
Nani sasa aliyeikasirisha? Walijiuliza.
Vilio vilisikika tena kutokea gizani. Watu wakakimbilia huko. Waliporejea ilikuwa taarifa ya mama mmoja aliyekuwa anakimbia ameshambuliwa na kitu kisichofahamika na hatamaniki tena. Amekufa!!
Hali ikatulia kwa muda. Akajitokeza mzee mmoja wa makamo akitembea kwa kutumia mkongojo.
Huyu hakuogopeshwa hata kidogo na hali iliyokuwa inaendelea. Alisimama mbele ya kundi na kuanza kusema anachokifahamu, alielezea historia fupi ya makaburi ya Kiyeyeu na majanga yanayotokea iwapo wazee wale waliolala katika makaburi yale wakikerwa na jambo. Hapa sasa akafikia kusema kuwa kuna mtu mmoja katika msafara alikuwa ameikasilisha mizimu!!
Ni lazima abaki ili kuwanusuru wenzake. Kama akiendelea mbele basi litatokea balaa kubwa zaidi ya hili. Alizungumza kwa sauti ya juu na kila mmoja aliweza kusikia. Sauti yake na umri wake vilikuwa vitu viwili tofauti!!
“Hivyo kama unajua una lolote la kuikera mizimu hii ni heri ubaki nyuma kuwanusuru wenzako.” Alizungumza kisha akatuachia mtihani wa kuamua aidha kujitokeza ama la!
Maneno yake niliamini kabisa yalikuwa yanamlenga John. Nilijisikia uchungu sana, John alitakiwa kubaki nyuma. Yaani harakati zangu zote hizo zinaishia hapa!! Niliumia sana.
Niliangaza huku na huko. Sikumuona John!! Nilitaka kumuita lakini niliamini kuwa hawezi kunisikia.
Kimya kilitawala akisubiriwa mtu huyo ambaye ameikera mizimu aweze kujitoa kundini. Hakuna aliyejitokeza.
Mzee akaendelea kusubiri!! Bado hakujitokeza mtu yeyote.
Kimya kilikatishwa na sauti ya mwanaume akipiga mayowe. Tukageuka nyuma kumtazama. Alikuwa amejishika shingo yake huku akipiga kelele. Mara damu zikaanza kumtoka puani, masikioni na mdomoni. Badala ya kumsaidia kila mtu akawa anamuogopa!!
Hatimaye akaanguka na kutulia tuli! Alikuwa amekata roho!!
Kina mama wakapiga kelele sana, wanaume wakabaki kushangaa.
Yule mzee wa kimila akaipaza tena sauti yake, “Kama asipojitokeza mtu huyu majanga yataongezeka. Mizimu inakasirika.”
Sasa watu wakaanza kusemezana huku wakisisitizana kuwa mtu huyu ajitokeze ili mizimu itulie. Bado hakuweza kujitokeza mtu yeyote.
Zikaanza kutolewa hirizi miilini mwa watu, lakini yule mzee wa kimila akapinga kuwa hizo ndio tatizo.
Waliokuwa na dawa za kienyeji wakatoa. Bado haikuwa tiba.
Kiza kinene kikatanda kama dalili ya mvua. Mwanga mkali ukamulika bila kutoa kelele. Watu watatu wakasalimia na ardhi.
Ilikuwa radi!! Na walikuwa maiti tayari.
Roho ikaniuma sana, nikajiona mimi ndiye muhusika. Nikatamani John atokezee nimtangaze kuwa ndiye chanzo. Lakini John hakuwepo tena!!
Vile vifo vya radi ya ghafla vilimshtua kidogo yule mzee.
Mara akabadilika sura na kuwa kama aliyekasirika!!
Akatoa amri ya watu kujipanga msitari. Amri ikasikilizwa. Wanaume na wanawake mstari mmoja, mistari ilipopangwa ndipo nilimuona John. Na yeye alikuwa amepanga mstari. Akaanza kupita na kufanya kile anachokijua mwenyewe. Alimfikia John, na yeye akamuona akamshika mkono. Ina maana John anaonekana? Nilijiuliza.
Nikiwa katika hali ya mashaka ya kila kinachoendelea. Mara yule mzee mkongwe alinifikia, alikuwa anatabasamu, mgongo wake uliopinda ulimfanya awe ameinama na kuwa mfupi sana!!
“Shkamoo babu.” Nilimsalimia.
“Marahaba mjukuu wangu.” Alinijibu kwa ukarimu sana.
Kisha akanishika mkono.
Alipofanya hivyo kwa wasafiri wengine hakutumia muda mrefu, lakini kwangu ni kama alitumia sekunde nyingi.
“Unaitwa nani binti.”
“Isabela!!”
“Nani alikwambia unaitwa Isabela.” Aliniuliza huku akinitazama usoni.
“Naitwa Isabela mzee.” Nilitaharuki kutokana na maswali ya mzee huyu.
“Hilo sio jina lako binti.”
“Sio jina langu?”
“Na litakugharimu sana na kuwaumikza wengine katika maisha yako.” Kauli nzito za mzee huyu zilinishangaza.
Isabela sio jina langu? Ni miaka zaidi ya ishirini tangu nipewe jina hilo. Sasa leo ananiambia kuwa hilo sio jina langu? Maajabu haya.
“Hautaendelea na safari hii…kuwaepusha wenzako na mabalaa yasiyowahusu.” Alininong’oneza. Nikahisi ubaridi ukinipenya mwilini, mapigo ya moyo yakapungua kasi. Nikakata tamaa.
Mimi tena? Sio John!! Maajabu haya.
“Kama unao upendo waruhusu wenzako waende zao. Janga lako haliwahusu hata kidogo.” Alinisihi. Nikatikisa kichwa kukubali. Huku nikiamini kwa asilimia kadhaa kuwa tatizo ni John na yule mzee hajui kitu.
Mzee akawatangazia watu kuwa tatizo limekwisha. Na kweli nilipokubali tu waondoke zao. Nilipogeuka makaburini. Ule ukungu haukuwepo tena.
Abiria wakaingia katika basi lile la ziada lililokuja kutuchukua.
Tofauti na mawazo yangu. Kuwa John atazuia basi lisiondoke baada ya yeye pia kuwa mmoja kati ya abiria. Haikuwa hivyo. Basi liliwaka vyema. Na kutoweka!!
Ilikuwa usiku mnene lakini kinyume na taratibu za usafiri Tanzania, basi lile lilisafiri usiku. Hayakusikika malalamiko ya kubanana tena. Kila mmoja alitaka kutoweka eneo lile. Hata madereva na makondakta wote walikuwa waoga.
Nilibaki na yule babu!!! Akina Samson, Jesca, na Jenipher walitaka kubaki na mimi lakini kwa maneno ya yule babu kuwa mzigo wangu hauwahusu. Niliwaruhusu waende zao huku nikiwapatia pesa nyingine ya ziada.
“Nendeni mkautangaze ushuhuda huu popote pale. Msifiche hata moja lililotokea. Hata kama sitafika huko mtakapokuwa. Naamini sisi ni washindi.” Niliwaeleza. Wakalia kwa uchungu. Samson akagoma kabisa kuondoka lakini hatimaye alikubali kuondoka.
Nilibaki na mzee yule tukizungumza. Alinieleza juu ya jina langu. Akadai kuwa hakuwa akijua nilikuwa naitwa nani lakini Isabela halikuwa jina langu.
“Rejea nyumbani ukalitafute jina lako. Jina lako limepotea ama limefichwa. Na ukiendelea kuamini kuwa wewe ni Isabela basi maisha yako yatakuwa ya tabu sana. Utawatesa wenzako nawe utateseka sana.” Alinieleza yule babu.
“Unaweza kwenda kupumzika nyumbani kwangu. Kesho upatafute nyumbani kwenu. Ukalitafute jina lako.”
Tuliongozana na yule mzee hadi nyumbani kwake. Hapo tulipokelewa na mbwa wengi sana waliomlaki bwana huyu kwa furaha.
Wahehe na mbwa!! Niliwaza.
******
Nililala katika mkeka. Ni kama nililala kwa sekunde kadhaa hatimaye pakapambazuka.
Mzee akaniamsha, akanisihi sana nihakikishe Napata jina langu halisi na hapo nitaendelea na maisha yangu vizuri.
“Jina langu ni nani?” nilijiuliza kwa sauti akanisikia.
“|Hata mimi silijui lakini ni lazima ulipate ili kuzikwepa laana za ukoo wako. Fuatilia historia yako vyema mwanzo hadi mwisho. Historia ya kweli ipo kwa mama…kamuulize mama yako. Wewe ni nani? Lakini nakukumbusha kuwa wewe sio Isabela”
Mzee alinisindikiza hadi njia ya mabasi.
“Usizungumze na mtu yeyote, kwa usalama wako na abiria wenzako.” Alifanya kunisemesha kwa sauti hafifu. Nikamsikia na kumwelewa.
Basi likapita. Nikapanda!! Mzee alinilipia nauli huku akichukua fursa ya kuzungumza na kondakta.
Safari ya kurejea Makambako. Safari ya kwenda kulitafuta jina langu. Jina lililopotea.
Kaka aliyekuwa pembeni yangu alikuwa anaongea maneno mengi sana. Lakini sikuwa namjibu chochote.
Hatimaye tukaifikia Makambako!! Nikashuka garini nikaikanyaga ardhi ya Makambako kwa huzuni sana!! Hatua kwa hatua nikaanza kuelekea nyumbani.
***
ISABELA bado katika utata sasa hatakiwi kuzungumza na mtu…..nini kitajiri MAKAMBAKO????
ITAENDELEA!!!!
About Author
JE, UNA HABARI, PICHA, TANGAZO, MAKALA NA USHAURI? USISITE KUWASILIANA NASI SIMU / WHATSAPP NAMBA 0625535420.
Advertisement
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.