MTUNZI: EMMY J.P
SIMU: 0654 960040
SEHEMU YA MWISHOOOO
“Kwa hiyo mwanangu anaweza kufa pia.” Aliniuliza kwa wasiwasi.
“Sijui nisemeje lakini kiukweli naogopa sana…” nilimjibu.
“Sasa Bela mimi nafanyaje hapa katika hili.”
“Dada kama unaweza kujua lolote lile kuhusiana na mimi tafadhali nieleze tumuokoe mtoto. Hana makosa hata kidogo.” Nilimsihi Suzi. Kilio cha mtoto kilikuwa juu kama kilivyoanza na alikuwa anazidi kujikunja mkono.
Suzi alinitazama usoni kama anayesoma kitu fulani kwangu.
“Bela…yapo baadhi ninayoyajua….nitakueleza, sio kwa imani za kishirikina hapana!! Nakueleza kwa kuwa ni lazima uyajue. Kama mwenyezi Mungu amenipa pigo hili ili nikueleze siri hii basi nakueleza. Lakini jitahidi kuwa na moyo mgumu.” Nilianza kutetemeka kwa maneno hayo ya dada, hakika nilikuwa namuheshimu kwa kuwa na siri nzito nzito.
Kabla ya kunieleza aliniongoza katika sala. Nikamfuatisha hadi alipomaliza.
Sasa uwanja ukawa wake nami nikawa katika zamu ya kusikiliza.
“Siri hii hata aliyenieleza hajui kama alinieleza.”
“Kivipi?”
“Mzee alikuwa amelewa siku hii. Na pesa ya kulewa nilimpa mimi. Baada ya kulewa akawa anasemezana nami kwa njia kama ya kupitiwa ama hajui anazungumza na nani.”
Nikakubali kwa njia ya kichwa.
Suzi alinielezea juu ya upendo wa baba kwa mama yangu ulivyomlazimisha kufanya jambo hili la ajabu. Tendo la kuiba mtoto na kumpatia mama bila yeye kujua.
“Aliiba mtoto…kivipi?”
“Baada ya mimi kuzaliwa mama alizaa mtoto mwingine, akafariki dunia akiwa tumboni. Siku chache kabla ya kuzaliwa. Baada ya hapo akashika mimba nyingine tena. Alipojifungua tu mtoto akafariki tena.” Alinieleza dada Suzi, taarifa ile ya pili ikanisisimua kuliko ile ya kwanza, maana nilikuwa naifahamu hiyo kuwa iliwahi kutokea. Hii ya pili sikuwa naifahamu.
“Baba akazungumza na manesi, akawapatia pesa nyingi ambazo ziliwafanya wasahau wajibu wao. Wakakiuka maadili wakaiba mtoto na kumpelekea mama halafu yule mtoto aliyekufa akapelekwa wanapojua wao.”
“Kwa hiyo mama alipozinduka?”
“Akajikuta ana mtoto wa kike….akaamini ni mtoto wake wa kumzaa.”
“Kwa hiyo mama anajua kuwa hayo yalitokea?” niliuliza kwa hamaki.
“Si yeye wala ndugu mwingine anayefahamu jambo hili. Kama nilivyokwambia hata mimi baba alinieleza akiwa amelewa.”
“Sasa huyo mtoto mwingine yupo wapi sasa hivi? Na anaitwa nani jamani”
Ndiye huyu mbele yangu, anaitwa Isabela.”
Nilipiga yowe la mshtuko!! Suzi akawahi kuniziba mdogo na kunikanya kuwa niwe mtulivu kama kweli nimeamua kuichukua siri hiyo. Nikajilazimisha kutulia.
“Isabela…wewe sio mtoto wa familia hii ya mwalimu Nchimbi, mimi sio dada yako wa damu, mwalimu sio mama yako na hata marehemu pia hakuwa baba yako.” Alisema Suzi huku akiwa amenitazama usoni moja kwa moja. Nikashtushwa na kauli hiyo. Nilitegemea kuwa Suzi atabadili kauli hiyo huenda amesema kimakosa, lakini hakubadili.
Mapigo ya moyo yakaenda kasi sana!! Nikatamani ile iwe filamu na itamalizika baada ya muda fulani. Lakini hali ikaendelea kuwa kama ilivyo.
“Dada Suzi, kwahiyo mimi…eeh!” nilikuwa nimepegawa.
“Hiyo ndiyo siri Isabela. Haya je inahusika kwa namna yoyote na tatizo la mwanangu???”
“Dada yawezekana kweli yahusika sana. Kwa maana hiyo mimi sio Isabela. Hili jina alinipa nani.”
“Baba na mama….namaanisha mwalimu Nchimbi na marehemu mume wake.”
“Basi mimi sio Isabela. Mama yangu na baba yangu watakuwa wapi Mungu wangu!!” nilijiuliza huku nikijikuna kichwa changu pasipo kuwashwa.
Wakati najikuna kichwani zikarejea zile kumbukumbu za kudekezwa sana na mwanamke huyu ambaye sasa naambiwa kuwa sio mama yangu. Upendo wa dhati alionionyesha tangu nikiwa mdogo ulizidi kunifanya kimya kimya nipingane na kauliza dada yangu. Lakini ule uwezo wa dada kutunza siri ulinirejesha kuamini kuwa ule ni ukweli.
“Kwa hiyo inakuwaje.” Alinishtua Suzi na kunifanya nikumbuke kuwa tulikuwa na tatizo.
Natakiwa kulipata jina langu na ukoo wangu!! Nilimwambia Suzi.
*****
Kama ilivyokuwa kwangu ndivyo ilivyomuwia mwalimu Nchimbi ugumu sana kuweza kuamini alichokuwa anaelezwa na dada Suzi. Alimanusuru azimie kama zisingekuwa jitihada za dada Suzi kulegeza maneno makali na kuyafanya laini.
Hatimaye mama aliyekuwa mbishi kipindi chote cha maziungumzo alikubali kwa shingo upande kuwa mimi sio mwanaye.
Kwa kuokoa maisha ya mtoto wa dada Suzi ambaye alikuwa analia mfululizo tuliamua kwa pamoja kushirikiana kulitatua tatizo hili.
Hospitali!! Hapa ndio tulianzia kumtafuta mama yangu. Ilikuwa hospitali ya serikali na ni miaka mingi sana ilikuwa imepita. Kila kitu kilikuwa kimebadilika, hakuwepo wa kuweza kutusikiliza na kutusaidia.
Mtoto akiwa amebaki nyumbani, sisi tukiwa katika hekaheka hizi ndipo mama alipokuja na wazo la kumwendea mkunga ambaye alimzalisha. Mama alikiri kumkumba mama huyo ambaye ni mstaafu tayari.
Hakuna aliyelalamika kuhusu kuchoka. Tulitembea kwa miguu. Tulipofika maeneo ambayo mama alihisi kuwa ndipo anaishji yule mkunga tulianza kuulizia. Ilituchukua muda mfupi tu kuweza kuyapata makazi yake.
“Ameenda sokoni lakini atarudi muda si mrefu.” Msichana tuliyemkuta pale nyumbani alitujibu.
Tukajiweka katika mkeka tulioukuta pale nje na kumsubiri.
Kama tulivyoelezwa mama huyo mkongwe kiasi alifika, kwa kumtazama alionyesha kuwa ujanani alikuwa mrembo sana lakini mwenye maringo.
Licha ya uzee huo bado alikuwa na maringo kiasi katika sauti yake.
Alitukaribisha huku akiwa amesimama kwa namna ya kutusikiliza shida yetu ni ipi.
Kila mmoja akamwachia mama jukumu la kuzungumza.
“Naitwa mama Isabela au …” kabla hajamaliza kujitambulisha ilisikika sauti kutokea dirishani, “Shakamoo mwalimu!!”
“He! We ni nani tena unanisalimia umejificha…” alisema mama kwa kitetemeshi cha ualimu.
Yule mkunga akasaidiana nasi kutazama mlangoni. Akatoka msichana kwa makisio ni umri wa miaka kumi na moja.
Akamsalimia mama kwa kupiga magoti.
Kabla ya kujibu mama akaanza kuvuta kumbukumbu.
“Eliza….nimekosea!!!” alimkumbuka jina lake kwa usahihi.
“Mjukuu wangu huyu, kumbe ni mwanafunzi wako.” Yule mkunga aliyekuwa amesimama akasema huku sasa akikaa. Mwanafunzi yule akawa ameujenga urafiki kati yetu.
Tukakaribishwa ndani!!!
Baada ya utambulisho mama alianza kujielezea juu ya jambo lililotuleta. Alianzia mbali sana hadi akalifikia lengo letu.
Mama yule kwanza, alishtushwa na taarifa hiyo kisha akasema kuwa hajui lolote kuhusu tukio hilo.
“Kwa hiyo una uhakika kuwa nilizaa mtoto na akawa hai?” mama alimuuliza akiwa amemkazia macho. Mkunga akawahi kukwepesha macho yake, nikamsoma na kugundua anatudanganya.
“Sikumbuki..ujue nimewazalisha akinamama wengi sana…hakika sikumbuki.” Alijitetea huku akiwa na hofu.
Aliusimamia uongo wake huo hadi pale nilipoamua kuyaingilia mazungumzo haya, hasira ilikuwa imeanza kunitawala.
Nikarusha karata yangu!!!
“Mama mimi nadhani nimpigie simu yule baba aliyeshuhudia tukio hili, najua nikimpigia atakuja na yule askari. Kwa hiyo tutaufahamu ukweli.”
Yule mama akatowa yowe la hofu huku akizungumza kikabila cha kwao, hakika alitaharuki kusikia polisi.
“Mwanangu…usipige simu subiri tunayazungumza haya yanaisha.”
Uwanja ukawa wake akazungumza.
Kama dada Suzi alivyosimuliwa na marehemu baba juu ya uwepo wangu katika familia ile ndivyo ilivyokuwa kwa nesi huyu ambaye mara kwa mara alitusihi tuyamalize kindugu.
“Na mama yangu ni yupi?” nilimuuliza ghafla akashangaa.
“Sikuelewi unaniuliza mimi au?”
“Ndio nakuuliza wewe…..mimi ni huyo mtoto azliyeibiwa.”
Akakodoa macho yake kwa hofu. Nikaiskia hasira ikinichemka sana nikatamani kumrukia.
“Kwakweli mimi sijui labda Gloria ndio atakuwa anafahamu.”
“Gloria ndio nani?” mama alimuuliza.
“Tulikuwa naye..huyo ndiye aliyenishawishi.
*****
Hatukupoteza muda, tulimpa nafasi kidogo ya kujiandaa tukaondoka kuelekea kwa huyo aliyemuita Gloria. Haikuwa safari ndefu sana, tulitumia taksi.
Na yeye tulimkuta vilevile akiwa yupo katika uzee.
Baada ya salamu mbili tatu. Moja kwa moja ikawa zamu ya yule nesi kumueleza mwenzake juu ya tukio la miaka zaidi ya ishirini iliyopita.
Kama ilivyokuwa wakati tunamueleza na yeye alileta ujanja wa kutaka kumruka mwenzake lakini alipothibitishiwa kuwa akileta udanganyifu yupo shahidi na polisi pia. Naye akanywea!
“Tunachohitaji kujua ni kitu kimoja tu!! Mama aliyeibiwa mtoto ni nani.” Nilikoroma kwa hasira. Suzi na mama wakawa wakimya.
“Ni Dina….Dina yule…..”
“Dina ni nani na anakaa wapi.”
“Dina ni kichaa…eeh! Mungu nisamehe mimi nisamehe…” alianza kulia yule mwanamke.” Hakuna aliyembembeleza.
Neno lake la kuwa Dina ni kichaa liliniacha njia panda, ina maana mama yangu ni kichaa na anaitwsa Dina? Hapana haiwezi kuwa!!! Nilipinga kimya kimya.
Baada ya kutulia tena akatueleza juu ya kichaa aliyepewa mimba miaka mingi iliyopita. Mimba iliyotaka kuchukua uhai wake kwa sababu ya kukosa matunzo. Ilikuwa kama bahati diwani wa kata hiyo ambaye alikuwa mwanamke alipata kukutana na kichaa huyu. Wakati huo mimba ilikuwa na miezi saba. Huruma ilimshika kutoka na na imani yake ya kiroho..”
“Ooh!! Jesus jesus!!” Suzi alinong’ona huku akiwa kama anasali.
Akaendelea yule mama. “Basi akafika mwenyewe hospitali na kutoa amri ya mwanamke yule kusaidiwa. Hatua za haraka zikachukuliwa. Mwanamke akaanza kukamatwa kinguvu na kupelekwa kliniki. Baadaye akafungiwa kabisa bila kutoka hospitali. Hatimaye miezi tisa ikatimia akajifungua bila kufanyiwa upasuaji. Mtoto wa kike!!!!
Wakati anajifungua mtoto huyu ndipo ilipatikana biashara hii ya kuiba mtoto. Hakika hali ilikuwa ngumu sana kiuchumi. Utawala wa serikali ya awamu ya kwanza ulikuwa umechachamaa sana hivyo kwa pesa tuliyotangaziwa na yule kijana ambaye simkumbuki jina mimi na mwenzangu hatukuweza kuikataa.
Pia tuliamini kuwa yule kichaa asingeweza kumlea mtoto wake. Hivyo kwa huruma tukamchukua yule mtoto na kumuuza.”
Simulizi ile ilinisisimua sana!! Nilikuwa natetemeka kwa kila neno alilotamka yule mwanamama. Nilijihisi kama nusu mwanadamu nusu nimekufa!!
Kimya kikatanda. Kila mmoja akiwaza lake. Mimi nikizidi kuamini maneno ya mzee yule wa Iringa. Kuwa lile halikuwa jina langu na wala haukuwa ukoo wangu.
“Mama yangu yupo wapi?” hatimaye niliuliza.
“Kwa kweli ni siku ya nne hivi sijamuona lakini huwa anapatikana stendi na majalalani.” Nikasisimka tena kusikia maneno haya. Mama yangu anaishi majalalani!!!
Niliumia.
Hapakuwa na jipya tena kwa pale. Kwa kuwa huyu mama alikuwa anamtambua Dina ilimlazimu kuzunguka nasi siku nzima kumtafuta.
Siku ya kwanza hatukufanikiwa kumuona.
Siku ya pili majira ya mchana baada ya kuzunguka siku nzima bado kimya. Tukapewa taarifa za juu juu kuwa aliingia katika gari ya kwenda Mbeya.
Huo ukawa mwanzo wa safari nyingine.
“Tulimshusha Uyole.” Kondakta alitueleza baada ya kufanikiwa kulipata lile gari alilosadikiwa kupanda mama yangu.
Wakati huu nilikuwa mimi na mama pamoja na yule mkunga. Dada Suzi alirejea nyumbani kwa ajili ya kulea mtoto ambaye sasa kilio kilikuwa kinapungua na kidogo alikuwa ananyonya.
Safari ya kwenda Mbeya ikafuata. Tukaweka kituo Uyole. Kama vile chokoraa tulianza kuzurura huku na huko bila mafanikio. Yule mkunga ndiye aliyekuwa anaulizia mara kwa mara maana ni yeye alikuwa anaujua muonekano wa huyo Dina.
Siku mbili Uyole bila mafanikio. Mama alikuwa amechoka dhahiri lakini asingeweza kusema, nadhani kwa kuwa aliamini nipo katika matatizo pia ni kama mwanaye wa kumzaa, maana hata titi lake nilikuwa nimenyonya.
Siku ya nne inakuja habari nyingine kuwa Dina alionekana sokoni. Asubuhi na mapema tukafunga safari kuelekea Uyole sokoni.
Tulisubiri kwa masaa kadhaa.
Kelele za akina mama zilitushtua, walikuwa wanahangaika huku na huko kutaka kushuhudia jambo huku wengine wakiwa wanakimbia.
“Yule pale Dina!!” mkunga alipiga kelele huku akitujelekezea kwa kidole.
Mwanamke mnene, akiwa na malapulapu mwilini alikuwa akiwaponda watoto na mawe. Huku akiwa na fimbo mkononi. Alikuwa anajongea eneo la soko. Jambo hilo liliwapagawisha akina mama na sasa walikuwa wanapiga kelele.
Nilimtazama mwanamke huyu anayesadikiwa kuwa ni mama yangu. Mara ghafla nikajikuta nipo wima, nikakimbia mbio mbio. Umati ulikuwa unashangaa na hata mwalimu Nchimbi alibaki kunitazama tu asijue la kufanya.
Macho yetu yalipogongana nikaona kitu!!
Ni kama kioo mbele yangu na nilikuwa najitazama.
Damu nzito kuliko maji!!!
Sikuogopa mawe aliyoshikilia, mavazi yake machafu!!
Nikamsogelea na kumkumbatia.
Maajabu!! Na yeye akanikumbatia huku akizungumza kabila nisilolielewa. Kimya kikuu kikatawala!!
Hakuna aliyetusogelea.
“Mama!!” nilinyanyua kinywa changu na kumuita!!
“Su…Subira…..” aliniita kwa mshangao.
Alipotaja jina hilo. Nikajikuta kama nasukumwa chini. Nikaanguka kama mzigo.
Nikajikuta katika filamu ya ajabu huku mimi nikiwa wa ajabu zaidi.
Nilikuwa napambana na mamia ya watu. Na sasa nilikuwa ana kwa ana na Dokta Davis. Alikuwa ananiogopa sana, nami sikuwa na huruma. Nikiwa na panga kubwa mkononi. Nilimkaribia na kumfyeka.
Nikatazama maadui wengine wanaonikabiri na wao nikawatenda nilichomtenda Davis.
Likafuata pambano kuu la kupambana na joka la maajabu.
Lilinisumbua lakini kila liliponijeruhi na mimi niliondoka na kipande kimoja cha mwili wake.
Pambano lilikuwa kali hadi walipotokea viumbe weupe sana wakaniweka kando kisha wakalimaliza joka.
Kisha wakakiteketeza kijiji kile cha maajabu. Lakini cha kushangaza mimi sikuungua kabisa.
Moto ulipokwisha nikajikuta nimesimama peke yangu. Uchi wa mnyama. Nilikuwa nimechoka na nilikuwa natokwa jasho.
Ule ujasiri niliokuwanao ukayoyoma na sasa nikawa naogopa.
Mara ghafla…”Mamaaaaaa!!” nikapiga kelele kubwa na kutaka kukimbia.
Nilipojaribu kufanya hivyo nikakabiliana na kamba ngumu zikiwa zimeifunga mikono yangu na miguu. Nilikuwa natokwa jasho sana.
Niliangaza huku na kule bila kupata majibu.
Mara kundi la watu likafika pale chumbani.
Wote walikuwa wakinishangaa. Nikamuona mwalimu Nchimbi.
“Mama ni nini hiki…mbona nimefungwsa hivi.” Niliuliza huku nikiwa nashangaa.
Mwanaume mmoja nisiyemtambua akaanza kunielezea juu ya vurugu nilizokuwa nafanya licha ya kupigwa sindano ya usingizi.
“Ni ugonjwa wa kushangaza sana.”
Alinielezea tukio zima la kuanguka baada ya kukumbatiana na kichaa ambaye alitoweka pia baada ya mimi kuanguka.
“Mama yangu!!” niliwaza!! Kisha nikatabasamu na akili ikiwa imerejea sawia.
Nilipofunguliwa kamba niliwaelezea juu ya yote yaliyokuwa yananikabili katika maono yangu ya ajabu.
“Nimeikamilisha kazi!!!” hatimaye nilitamka hayo.
Tulikuwa hospitali ya mkoa ya Mbeya. Baada ya siku nne niliruhusiwa kuondoka. Niliambatana na mwalimu Nchimbi.
“Naitwa Subira!!” nilimweleza mama.
“Najua!!” aliniambia, nikashangaa.
“Umejuaje.”
“Ulisisitiza sana wakati ukiwa umepoteza fahamu zako.”
Nilitabasamu naye akatabasamu.
*******
Mtoto wa dada Suzi alikuwa halii tena japo mkono wake ulibaki kuwa vile umejikunja.
Amani ikautawala moyo wangu!!!
Taarifa pekee iliyoniumiza ni juu ya kifo cha mama yule kichaa aliyekufa baada ya kugongwa na gari.
Japo nilipata nafasi ya kusikia neno moja tu kutgoka kwake lakini alikuwa amenisaidia mengi mno.
Familia yangu ilimzika kwa heshima zote kama ndugu.
Baada ya kuyaweka haya yote pembeni niliirejesha akili yangu jijini Mwanza.
Mama alikopa pesa nikasafiri kurejea chuoni.
Safari ilikuwa njema sana.
Maria akawa mwenyeji wangu jijini Mwanza. Akanielezea juu ya yote yaliyotokea. Hapakuwa na lolote baya, zaidi ya maajabu ya kanisa fulani kudai limemtoa John msukule kutoka gamboshi.
Nilitabasamu na kukiri kuwa dini imegeuka biashara. Lakini sikumwelezea Maria juu ya yote tuliyoyapitia.
“Jesca na Jenipher je?” nilimuulizia na kutegemea jibu la maajabu tena.
“Kumbe mwenzangu na wao hawakufa..eti vilizikwa vinu badala ya watu!! Dunia ina mambo.” Alijibu.
“Kwa hiyo bado wapo chuo.”
“Hapana hawapo kwa sasa. Lakini Jesca yupo mtaani.’
“Amakweli dunia ina mambo…” nilimuunga mkono.
Maria hakujua lolote lile kuhusu yaliyonisibu mimi. Na alikuwa kama anayenifahamisha juu ya yaliyotokea huku akiamini kuwa ile ruhusa niliyoomba ndio iliyonifanya nitoweke ghafla.
“mwenzangu na mimi siku moja sijui nikaota madudu gani. Wacha nipagawe..” Maria alinisimulia alichokiota na kilikuwa sawa na kilke kichotutokea msituni.
Maria hakujua kama ni kweli alikuja kule msituni!!!
“Nilipiga kelele wewe nikamuita Mungu, mama na mizimu yote!!” aliendelea kusimulia.
Baada ya mazungumzo hayo marefu. Niliingia kuoga.
Baada ya kuoga nikiwa katika kutafuta nguo ya kubadilisha nikakutana na kadi ya benki. Nikaitazama huku nikiweka mbali kabisa tamaa.
Nilipokuwa nimebadilisha nguo, nikaanzisha moto mdogo nyuma ya nyumba na kuviteketeza baadhi ya vitu ambavyo nilihisi vitakuwa vinanikumbusha juu ya Dokta Davis. Nilitaka kuiteketeza kadi ya benki pia lakini nikakumbuka kuwa ilikuwa pia kwa ajili ya matumizi ya chuoni. Nikaghairi zoezi hilo.
******
Baada ya wiki moja nikapata fursa ya kukutana na John!! Nilikutana naye akiwa anaelekea kanisani.
“Bwana asifiwe dada..Bela.” alinisalimia huku akionekana kutokumbuka lolote.
Nikamjibu, tukabadilishana naye mawili matatu. Akaenda zake huku akinisihi kuwa akitoka kanisani atanitafuta.
Niliondoka pale nikiwa natabasamu na kujipongeza kwa vita ile kuu ambayo nimeibuka kuwa mshindi. Vita ambayo nimepoteza kipande kidogo tu cha nyama yangu lakini kwa ukombozi wa mamia ya watu..kutoka katika milki ya Shetani na chapa yake ya 666.
Japo sikutaka tena kurejea katika mtandao huo lakini nilikiri kwa kila neno la lugha ninayoifahamu kuwa kamwe SITAISAHAU facebook.
SEMA LOLOTE KUHUSIANA NA RIWAYA HII KUTOKA KWA EMMY…….MAWAZO YAKO YATAMJENGA ZAIDI. USIACHE KUBOFYA LIKE KAMA TULIKUWA PAMOJA KUANZIA MWANZO HADI MWISHO……
TUMA UJUMBE WAKO PIA KATIKA NAMBA YA EMMY, 0654 960040…….HADITHI NYINGINE ZA EMMY J.
HARUFU YA KIFO
YATIMA
MWALIMU NCHIMBI
CHUKI.
SIRI
MWISHOOOOO….!!!!!!
TUMA UJUMBE WAKO PIA KATIKA NAMBA YA EMMY, 0654 960040…….HADITHI NYINGINE ZA EMMY J.
HARUFU YA KIFO
YATIMA
MWALIMU NCHIMBI
CHUKI.
SIRI
MWISHOOOOO….!!!!!!
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.