POLISI WATOA MSAADA KWA VITUO VYA WATOTO YATIMA NCHINI

clip_image001

Na. TAMIMU ADAM, Jeshi la Polisi

Jeshi la Polisi Tanzania limeungana na majeshi ya Polisi duniani kuadhimisha siku ya Polisi duniani ( Police day) kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na Operesheni katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Akizungumzia siku hiyo, Msemaji wa Jeshi hilo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Advera Senso alisema askari wa Jeshi la Polisi kote nchini wameadhimisha siku hiyo maalumu Kwa Polisi kwa kufanya usafi, kutoa huduma za kijamii, misaada katika vituo vya watoto yatima pamoja na kuwatembelea wazee wasiojiweza kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya Polisi.

Akitolea mfano wa kituo cha watoto yatima kilichopo chamanzi wilaya ya Temeke jijini, Dar es salaam kinachojulikana kwa jina la Yatima Group Trust Fund, SSP. Senso alisema askari wa kikosi cha Polisi bendi walianzimisha siku hiyo kwa kufanya usafi katika kituo hicho pamoja na kupita nyumba hadi nyumba kutoa elimu ya ulinzi jirani.

Mbali na kushiriki katika kufanya usafi kikosi hicho cha bendi ya Polisi kilitoa msaada wa vyakula, ambapo kichangia mifuko mine ya unga, kilo 20 za sukari, kilo 20 za maharage na mchele kilo 50. kikosi hicho pia kilitoa mafuta ya kupikia lita 20, sabuni miche 57 pamoja na chumvi pakiti 30.

Aidha, katika baadhi ya mikoa kama Mkoa wa morogoro, Singida, siku ya polisi imeanzimishwa kwa kufanya usafi katika eneo la standi ya zamani ya mabasi kwa kushirikiana na wananchi pamoja na uongozi wa manispaa ya singida kwa kutoa elimu ya ulinzi shirikishi ili kuimarishwa usalama katika maeneo mbalimbali ya mkoa ikiwemo standi ya zamani ya mabasi.

SSP. Senso alibainisha kuwa siku ya polisi hapa nchini imeanzimishwa kwa kufanya Operesheni kali katika mikoa mbalimbali ambapo katika mkoa wa Mwanza, Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata bunduki ya kivita aina ya SMG ikiwa na risasi zake 65 ambayo ilitumika katika tukio la Busisi.

Mbali na operesheni hiyo, Polisi mkoa wa mwanza kwa kushirikiana na wadau mbalimbali yakiwemo makampuni ya vinywaji baridi iliendesha bonanza la mpira wa miguu lililofanyika katika uwanja wa mabatini lililoshirikisha timu sita ikiwemo timu ya Polisi mkoa wa mwanza.

Aidha, msemaji wa jeshi hilo aliwataka wananchi walioko katika sehemu mbalimbali hapa nchini kuadhimisha siku hiyo ya polisi kwa amani na usalama pamoja na kuwataka kuendeleza dhana ya polisi jamii kwa vitendo kwa kutowaonea haya watu wanaofanya vitendo vya uhalifu ndani ya jamii.

Post a Comment

Hii ni Blog kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Nchi yetu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...

Previous Post Next Post