Khatimu Naheka na Musa Mateja
WINGA mpya wa Yanga, Mrisho Ngassa (pichani), jana amejiunga rasmi na kikosi chake hicho zikiwa ni siku chache baada ya kumaliza majukumu yake Taifa Stars, lakini akaeleza kile anachoamini ndiyo sahihi katika sakata lake la kusajiliwa na timu mbili.
Msimu uliopita, Ngassa aliitumikia Simba kwa mkopo akitokea Azam, lakini Simba imekuwa ikidai iliingia naye mkataba wa mwaka mmoja, uliotarajiwa kuanza baada ya ule wa mkopo kumalizika, suala ambalo winga huyo amekuwa akilipinga.
Winga huyo hivi karibuni alisaini mkataba wa miaka miwili na Yanga, Championi likawa gazeti la kwanza kuandika, lakini klabu mbili za Simba na Yanga zimepeleka jina lake kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Akizungumza na Championi Jumatano, jana asubuhi kwenye mazoezi ya Yanga katika Uwanja wa Loyola, Dar, Ngassa alisema taarifa zinazotolewa na Simba kuwa amesaini nao mkataba hazina ukweli. Akasema anaamini viongozi wa klabu hiyo wana nia ya kutaka kumharibia maisha yake.
Ngassa alisema ameshangazwa na taarifa zinazotolewa na Simba sambamba na kuwasilisha jina lake katika orodha ya wachezaji watakaokuwa nao msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
“Sikuwa na mpango wa kuendelea kuitumikia Simba, ndiyo maana sikusaini mkataba wowote nao, nimeshangazwa na hili walilolifanya, sijajua huyo ni Ngassa gani aliyesaini huo mkataba wanaodai nimesaini! Nadhani kuna baadhi ya viongozi wa Simba wana nia ya kutaka kuniharibia maisha yangu.
“Ninachojua sasa ni suala moja kuwa mimi ni mchezaji wa Yanga, hata akili yangu sasa ipo katika kuitumikia klabu yangu mpya, lakini naamini TFF wanafanya majukumu yao kwa umakini mkubwa.Mwisho naamini watatoa ukweli halisi juu ya hilo,” alisema Ngassa.
Wakati Ngassa akiyasema hayo, Kocha Mkuu wa Yanga, Ernie Brandts, ameonyesha kushtushwa na taarifa hizo za Ngassa kusaini klabu mbili, lakini akasisitiza kuwa bado anamhitaji nyota huyo katika kikosi chake kwa kuwa yupo katika mipango yake.
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.