Unknown Unknown Author
Title: MBUNGE MURJI HANA HATIA, MAHAKAMA HAKIM MKAZI MTWARA YAMWACHIA HURU
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mtwara imetupilia mbali mashtaka ya uchochezi yaliyokuwa yakimkabili Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Hasnain ...

clip_image002Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mtwara imetupilia mbali mashtaka ya uchochezi yaliyokuwa yakimkabili Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Hasnain Murji, hivyo ameachiwa huru.

Murji alikuwa akikabiliwa na tuhuma za uchochezi wa vurugu za kupinga kujengwa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka mkoani Mtwara hadi jijini Dar es Salaam, zilizosababisha vifo vya watu watatu na wengine kadhaa kujeruhiwa Mei, mwaka huu.

Uamuzi wa kutupilia mbali mashtaka hayo, ulitolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Dyness Lyimo, baada ya kukubaliana na hoja za upande wa utetezi uliowakilishwa na mahakamani hapo Wakili Peter Kibatala.

Katika utetezi wake, Kibatala aliiomba mahakama hiyo imfutie mteja wake mashtaka hayo kwa madai kwamba, hati ya mashtaka iliyowasilishwa mahakamani hapo ilikuwa na upungufu mkubwa wa kisheria.

Kibatala alidai miongoni mwa upungufu uliokuwamo kwenye hati hiyo, ni pamoja na kutokuwa na maelezo yanayoonyesha waziwazi kosa alilokuwa akishtakiwa mteja wake.
Alidai vifungu namba 129 na 132 vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai namba 20 kama ilivyorejewa na marejeo ya mwaka 2002, vinataka hati za mashtaka zizingatie na kutekeleza suala hilo.

Kwa mujibu wa Kibatala, kinyume cha hivyo, vifungu hivyo vinaipa mahakama uwezo wa kufuta hati ya mashtaka yenye upungufu wa kisheria.
Kwa kuzingatia hoja hizo, jana Hakimu Lyimo aliitupilia mbali hati hiyo ya mashtaka na kuamwachia huru Murji.

Murji (46) alipandishwa kizimbani Juni 10, mwaka huu na kufunguliwa kesi ya uchochezi.
Mbunge huyo alisomewa mashtaka na Mwanasheria wa Serikali, Kisheni Mtalemwa akisaidiana na Zuberi Mkakatu, na kudai kuwa Januari 19, mwaka huu katika maeneo ya Ligula mjini hapa alichochea watu kufanya vurugu kinyume cha sheria.

Katika kesi hiyo, pia kulikuwa na washtakiwa wengine 91 walisomewa mashtaka hayo.
Baadhi yao waliachiwa kwa dhamana na wengine walipelekwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti hayo.

Murji alirudishwa rumande baada ya kukana mashitaka na kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambayo alitakiwa awasilishe mahakamani hati ya kusafiria, mdhamini mmoja mwenye mali isiyohamishika, yenye thamani isiyopungua Sh milioni 20 na iwe imefanyiwa tathmini pia asifanye mikutano yoyote ya hadhara bila kibali cha kamanda wa polisi wa mkoa.Murji hakuwa na pasi yake ya kusafiria siku hiyo.

Mbali ya Murji, viongozi wanne wa vyama vya upinzani nao wana kesi dhidi yao wakikabiliwa na mashitaka matatu likiwamo la kula njama, kufanya uchochezi na kuamsha hisia mbaya kwa wananchi.

Viongozi hao ni Katani Ahmed Katani (33) Mwenyekiti wa Vijana wa Chama cha Wananchi (CUF) na Saidi Kulaga (45) Katibu wa Wilaya ya Mtwara CUF, Hassan Uledi (35) Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi wa Wilaya ya Mtwara na Hamza Licheta (51) Katibu Mwenezi wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) wa Mkoa wa Mtwara, wote wakazi wa Mtwara.

SOURCE : NIPASHE

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top