RIWAYA: SITAISAHAU facebook
MTUNZI: EMMY JOHN Pearson.
MAWASILIANO: 0654960040
SEHEMU YA KWANZA
“Isabela….Isabela…” nilisikia sauti ya mwanamke ikiniita, niligeuka mara moja maana sauti ile ni kama niliwahi kuisikia mahali. Lakini sikukumbuka ni wapi. Giza totoro lilinizuia kuweza kumtambua mtu yule aliyeniita kwa ufasaha kiasi kile tena gizani.
Nilianza kujiuliza iwapo nirejee nyuma kurudi kumtafuta ama niendelee mbele ambako pia sikuwa na uhakika ni wapi. Manyunyu ya mvua yalikuwa yamenilowanisha hasa na nguo yangu ilikuwa imeshikana na mwili. Nilikuwa natetemeka huku michubuko kadhaa katika mwili wangu ikiniwashawasha. Kilikuwa kitendawili aidha niende mbele ama nirudi nyuma kuifatiliza hiyo sauti.
Ile hali ya kujiuliza niende mbele ama nirudi nyuma ikanifanya niwe kama naigiza igizo lisilokuwa rasmi.
“Isabelaaaa!!!.” Iliita tena sauti hii. Sasa ilisikika dhahiri kuwa sauti ile ilikuwa katika kulia, mwenye sauti ile alikuwa katika uchungu mkubwa na bila shaka aliuhitaji sana msaada wangu. Nilitamani kuitika lakini midomo ikawa mizito. Nilipolazimisha kuitika nikawa kama nanong’oneza, sauti haikutoka. Koo lilikuwa limekauka sana. Hapo ndipo nikagundua kuwa nilikuwa na kiu sana.
Nikiwa bado katika kigugumizi mara nikasikia kama hatua za mtu ama mnyama zikikatiza taratibu. Mara moja nikajiziba mdomo wangu, pumzi zangu zisiweze kusikika kwa huyo mtu. Sikuamini hata kidogo kwamba huyo anaweza kuwa yule mwanadada
aliyekuwa ananiita kwa jina langu, maana huyo alisikika kutokea upande mwingine na wala sio huu aliosikika huyu anayekatiza. Nikaamua kutulizana.
Baada ya muda pakawa kimya, kwa tahadhari kubwa nikaanza kunyata kwa kutembelea vidole kwa mbele vya miguu. Moyo ulikuwa katika mwendo kasi ambao hapo kabla sikuwahi kuufikiria.
Moyo wangu ulikuwa katika majuto makubwa na tamaa yangu ilikuwa inaniponza sasa. Pesa nisizozitolea jasho zikawa zimenifikisha katika maluweluwe haya. Maluweluwe ya kutisha. Ulimwengu ukawa unanihukumu.
Nilimfikiria yule dada aliyekuwa ananiita, nilielewa kabisa kuwa nilikuwa namfahamu lakini swali likaja.
Anaitwa nani?? Ni wapi tulionana??
Baada ya dakika thelathini za kutangatanga katika kipori hicho kidogo hatimaye niliifikia barabara.
Ilikuwa ni barabara ya vumbi ukubwa wake ulikuwa unatosha gari kupita bila wasiwasi. Nikaamua kuifata barabara ile ili niweze kutoka eneo lile la hatari kabisa. Niliifata barabara ile kwa urefu mkubwa sana…miguu ilichoka lakini sikuwa tayari kukubali kukaa chini. Hata kama ningelia kwa wakati ule isingesaidia kitu nilikuwa katika hali ngumu sana.
MIEZI SITA NYUMA
Maisha ya chuo yalikuwa yamenipiga haswa, mwalimu Nchimbi ambaye ni mama yangu mzazi naye alikuwa ameungana na waalimu wenzake katika mgomo wa nchi nzima dhidi ya masilahi finyu ya waalimu hivyo hakuwa na senti yoyote ya kuweza kunisaidia, baba naye alizidi kupata umaarufu katika vilabu vya pombe kwa kucheza na kuimba hovyo baada ya kuwa amegida za kutosha.
Kaka yangu alizidi kuchanganywa na madawa ya kulevya huku dada yangu mkubwa akiwa bize na ulokole aliouamini kuliko hata mume wake waliyezaa naye watoto watatu. Sikuwa na mtu yeyote wa kumwomba msaada kwani kaka yangu mwingine ambaye kidogo alikuwa
anajiweza alikuwa haambiliki wala hashikiki mbele ya mke wake halafu
kibaya zaidi mke wake tayari tulikuwa tumegombana.
Mkopo wa asilimia ishirini niliokuwa napokea ulikuwa unaishia katika kulipa madeni.
Maisha yalikuwa yameniwia magumu sana, na marafiki hawakuwa na kikubwa cha kunisaidia.
Muda wangu mwingi nilikuwa naupoteza katika kusoma vitabu na pia kuperuzi mitandao ya kijamii, facebook ukiwa namba moja. Picha zangu ziliwafanya watu wengi wasiweze kuamini kuwa nina matatizo lakini ukweli nilikuwa naujua mimi binafsi.
Kawaida ya wavulana walikuwa hawaishi kutoa maombi yao ya kuwa wananipenda lakini nilijaribu kuwakwepa kwani niliamini kuwa kujiingiza katika mahusiano ni sawasawa na kujiongezea matatizo katika maisha yangu kwani wanaume hawaaminiki hata kidogo.
Kila mwanaume huwa ana mbinu zake za kumuingia msichana, na mimi kama msichana nilikuwa nimezikariri na kumwelewa mwanaume iwapo anakaribia kunitongoza ama la. Lakini kati ya wanaume wote aliibuka mwanaume mwingine naweza kumuita wa ajabu kupita wote. Yeye alikuwa hatabiriki leo mara anaelekea kwenye mapenzi mara kesho siasa, akisema leo kuhusu mpira wa miguu basi siku nyingine ataleta masuala ya dini.
Jina lake lilisomeka kwa kifupi kama Dk. Davis. Na kamwe sikuwahi kulijua jina lake kamili zaidi ya kujua kuwa anaitwa dokta davis. Kwa kuwa ule ni mtandao wa kijamii sikuwa na haja ya kumjua sana, haikuwa na maana yoyote ile.
Picha za dokta Davis zilikuwa za kawaida sana na hakuonekana kama ni mtu anayeweza kuwa na msaada wowote. Ule udokta wake nikauchukulia kama ule wa kutafuta sifa facebook.
Haikupita siku bila Davis kunitumia ujumbe, sikumtilia maanani sana.
Siku moja majira ya jioni, nikiwa nimekaa chumbani kwangu, hasira zikiwa zinafukuta kichwani baada ya wanachuo wenzangu tuliokuwa tunaishi hostel moja jijini Mwanza, kunisimanga kuwa silipii umeme halafu ni bingwa wa kuutumia. Kwanza nilitaka kuulaani umasikini lakini nikahisi nitakuwa nauonea. Nikaanza kumlaani mwalimu Nchimbi, mume wake, baba na babu zao kwani niliamini kama wangefanya kazi kwa bidii bila shaka wangeupiga kikumbo umasikini.
Laana zangu, ambazo nilitaka kuzifikisha hadi kwa mizimu yao zilikatishwa na mlio katika simu yangu. Ulikuwa ujumbe umeingia. Niliogopa kuufungua maana niliamini ni watu wanaonidai. Nilitamani kuzima simu lakini nikakukumbuka kuwa nilikuwa nimem-bip mama yangu dakika saba zilizopita na alikuwa hajanipigia bado.
Nikapiga moyo konde nikaufungua ule ujumbe.
“Umepokea Tshs. 66,666 kutoka kwa Magreth Pearson. Salio lako jipya ni 66,666”
Zile laana zikakoma mara moja, mawazo yote yakahamia katika simu yangu. Nikausoma vyema tena ule ujumbe. Ulikuwa upo sahihi. Nilipoangalia salio langu kweli lilikuwa lieongezeka.
Nikajiuliza huyu Magreth ni nani. Jibu halikupatikana.
Nikazungusha kichwa huenda yupo mtu nilikuwa namdai jibu likawa hapana ni mimi nilikuwa nadaiwa.
“Huenda ni mtu kakosea kutuma!!!” likaja wazo hilo. Likachukua nafasi kubwa. Mara moja pepo la tamaa likaniingia nikamwomba msamaha kimoyomoyo huyo aliyetuma kimakosa. Kisha nikazima simu. Sikuwa nataka tena habari za mwalimu Nchimbi huko Makambako.
Upesi upesi nikakimbilia katika vibanda vya kutolea pesa nikawasha simu na kuitoa ile pesa upesi.
Kisha kwa mara nyingine nikazima simu tena.
Kitu cha kwanza niliwakata kidomodomo wanachuo walionisemasema. Nikalipia umeme!!!!
Heshima kidogo ikarudi!!! Usiku huo nilipika pilau, pilau yenye hadhi ya kuitwa pilau.
Najua iliwauma!!! Nilifanya makusudi!!!
Kesho yake baadhi wakawa marafiki zangu tena.
Baada ya siku tatu nikaiwasha simu yangu. Hapakuwa na meseji yoyote iliyoingia ikilalamika juu ya kukosea kutuma pesa!!!!
Sikuhangaika kujiuliza kulikoni.
*******
Ile pesa ilipokwisha nikarejea kwenye msoto kama ilivyo ada, nikawa najiliwaza katika mtandao wa kijamii wa facebook.
Kama kawaida Dokta Davis, alikuwa amesheheni katika kisanduku cha kuhifadhi ujumbe.
Leo Davis alikuwa na topiki nyingine kabisa, Dokta Davis alikuwa anazungumzia biashara ya mtandao.
Biashara ya mtandao?? Nikajiuliza…cha kushangaza kabla sijamuuliza hilo swali tayari alikuwa amenipa majibu.
Akaniuliza kama napenda kufanya biashara.
Kidogo nisimjibu maana kwa picha zake biashara kubwa kwake labda ya kuuza ubuyu karanga za kuchemsha. Sasa anataka kufanya biashara gani na mimi?? Nilijiuliza na kupatwa hasira kidogo. Lakini kwa kuwa sikuwa na kazi ya kufanya nikaendelea kuchat naye lakini vinginevyo nisingemjibu upuuzi wake aliotaka
kuniambia.
“Unaweza kuvuna hadi milioni mbili…si lazima iwe mwisho wa mwezi!!!.” Ujumbe wake ulisema. Mh!! Macho yakanitoka, nikaingiwa na dharau kabla ya kuendelea na mazungumzo hayo.
“Kivipi??” nilimuuliza ilimradi tu..
“Kirahisi sana.” Alijibu. Sikuridhika na jibu lile nikambambika maswali mfululizo hatimaye Davis akanitumia kwa kirefu ni biashara gani hiyo aliyotaka kufanya nami na kwanini anichague mimi.
Baada ya dakika mbili nilikuwa nimemaliza kuusoma ujumbe mrefu wa Dokta Davis. Nilikuwa natetemeka, mapigo ya moyo yalikuwa katika mwendokasi wa kutisha sana. Macho yalikuwa hayafumbi bali yanaitazama simu yangu!!! Nilikuwa simuoni Dokta Davis lakini nilikuwa katika TAHARUKI!!!!!
SIKUAMINI!!!!!
***ISABELA ameambiwa nini cha kushangaza na dokta Davis?
**Pesa aliyoipokea ilitumwa na nani??
Kwanini anasema ‘SITAISAHAU facebook??”
bofya LIKE Kama umeipenda....na usikose hata episode mojaaa
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.