MSHAMBULIAJI wa Sevilla, Luis Alberto atafanyiwa vipimo vya afya Liverpool kesho baada ya klabu hizo mbili kufikia makubaliano ya kuuziana nyota huyo kwa Pauni Milioni 6.8.
Kinda huyo wa umri wa miaka 20, ambaye atasaini Mkataba wa miaka minne, amekuwa akicheza kwa mkopo Barcelona B na alitarajiwa kubaki Sevilla, lakini kwa fedha iliyotolewa klabu hiyo imeamua kumuacha aondoke.
Barcelona imeamua kuachana na nia ya kumsajili moja kwa moja baada ya kumaliza muda wake wa kucheza kwa mkopo, na Alberto atakuwa mshambuliaji wa pili kusajiliwa Liverpool baada ya Iago Aspas kutoka Celta Vigo.
Usajili huu unaleta shaka juu ya mustakabali wa mshambuliaji wa Uruguay, Luis Suarez, ambaye amekuwa akihusishwa na kuondoka majira haya ya joto.
REKODI YA LUIS ALBERTO NGAZI YA KLABU:
2009-2012 - Sevilla B Mechi 77 mabao 25
2011 - hadi sasa - Sevilla Mechi 7 hakufunga bao
2012-13 - Barcelona B (mkopo) Mechi 37 mabao 11
Habari hizo zinakuja siku moja baada ya Mkurugenzi wa Michezo wa Sevilla, Monchi kusema ofa iliyotolewa na Liverpool ni kiduchu kwa Alberto - lakini klabu hiyo ya Merseysiders imekamilisha mpango.
Alberto ameichezea mara moja timu ya taifa ya vijana ya Hispania chini ya umri wa miaka 21, na amefunga mabao 11 katika mechi 38 alizoichezea Barcelona B msimu uliopita.
Amefunga mabao 25 katika mechi 77 alizoichezea Sevilla B kati ya mwaka 2009 na 2012, na ameichezea klabu hiyo mechi saba za La Liga.
Mbadala wake? Usajili huu ni dalili kwamba anatafutwa mbadala wa Luis Suarez anayetaka kuondoka Anfield