Na Abdallah Khamis
WAFUASI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Nachingwea, Mkoa wa Lindi, wanadaiwa kumteka, kumpiga na kumvunja pua Katibu Mwenezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wilayani humo Andrea Mlaponi.
Tukio hilo linadaiwa kutokea juzi kati ya saa 1:00 na 2:00 usiku wakati Mlaponi akirejea nyumbani kwake kutoka katika mkutano wa kampeni wa Kata ya Stesheni.
Watekaji hao wanadaiwa kutumia gari yenye namba za usajili T 820 BJA, mali ya CCM Mkoa wa Lindi.
Taarifa ya kutekwa kujeruhiwa na kuvunjwa pua kwa Mlaponi ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni wa CHADEMA, Benson Kigaila, wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuelezea mikakati inayofanywa na CCM, kwa kushirikiana na serikali kuwadhuru wananchi na kisha kutumia propaganda za kisiasa kuisingizia CHADEMA.
Wakati Kigaila akielezea uhusika wa serikali na CCM katika uhalifu huo, katika tukio la Lindi, Kamanda wa Polisi mkoani humo, George Mwakajinga na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nachingwea, Eric Kayombo wametupiana mpira juu ya tuhuma za kutekwa na kumpiga Mlaponi.
Kigaila alisema baada ya kupata taarifa ya kutekwa kwa Mlaponi, aliwasiliana na OCD wa Nachingwea, majira ya saa sita usiku ambapo alielezwa kuwa taarifa hizo zimeshafika polisi na zinashughulikiwa.
Alisema jana asubuhi, aliendelea kuwasiliana na OCD huyo baada ya wananchi kumueleza kuwa katika tukio la kutekwa kwa Mlaponi walimkamata mtu mmoja na kuwatambua wengine kwa majina pasipo hatua zozote kuchukuliwa na Jeshi la Polisi mkoani Lindi.
“Usiku wa jana (juzi) baada ya utekaji huo wa viongozi wetu, wananchi walipeana taarifa wakazuia barabara na kufanikiwa kumkamata mtu mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Dismas Lucas, wakamkabidhi polisi na wengine walitajwa na mtuhumiwa aliyekamatwa. Jambo la kushangaza polisi Nachingwea hawajashughulika kuwakamata watu hao. Hii inatia hofu dhamira ya jeshi letu katika kusimamia haki na usalama wa wananchi,” alisema Kigaila.
Alisema tukio hilo la viongozi wa CCM kuwadhuru wananchi ni mpango mkakati ulioandaliwa kwa lengo la kuidhohofisha CHADEMA.
Aliongeza kuwa licha ya kufanya juhudi za kutaka kujua kinachoendelea kutoka kwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nachingwea, alisema kiongozi huyo wa umma amekuwa mzito kuchukua hatua zinazostahili kwa waliotajwa kuhusika na uaharamia huo.
Tanzania Daima iliwasiliana na OCD wa Nachingwea kupitia simu ya kiganjani juu ya tukio hilo ambapo awali alitaka kujua kama mwandishi anayempigia simu yupo mkoani Lindi na alipoelezwa kuwa yupo Dar es Salaam, akasema tukio hilo halipo.
Alipobanwa juu ya kukiri kwake kwa viongozi wa CHADEMA kwamba wana taarifa za tukio hilo na wanalishughulikia, OCD Kayombo alisema anayefaa kuongelea hilo ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC).
“Wewe hayo maswali unayoniuliza mimi sitoi taarifa kwako, muulize RPC atakupa majibu hayo kwa kuwa nimeshamueleza kila kitu,” alisema Kayombo na kukata simu.
RPC Mwakajinga alipopigiwa simu kuelezea hatua zilizochukuliwa na jeshi lake katika tukio la kutekwa, kupigwa na kuvunjwa pua kwa Mlaponi, alisema katika mkoa huo hakuna tukio la aina hiyo lililotokea.
“Hayo unayoniambia ni mageni kwangu na hakuna tukio hilo,” alisema Mwakajinga na kukata simu kama alivyofanya OCD Kayombo na baada ya hapo aliizima kabisa.
Mkoani Mwanza, inaelezwa kuwa kundi la watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa CCM, wamewavamia makada wa CHADEMA Kata ya Nyampulukano wilayani Sengerema kisha kuwashambulia na kulipiga kwa mawe gari lenye namba za usajili T 869 AQK, walilokuwa wakilitumia kwenye kampeni.
Tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 5 asubuhi, katika eneo la Kiwanja cha Ndege Mission Sengerema, ambapo imeelezwa kuwa wafuasi hao wa CCM walimjeruhi kada mmoja wa CHADEMA na baadaye kada huyo kukamatwa na kuwekwa ndani katika Kituo Kikuu cha Polisi Sengerema.
Taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza kwamba wakiwa katika safari yao ya kuelekea kwenye mkutano wa kampeni, makada hao wa CHADEMA walivamiwa na wafuasi wa CCM kwa sababu za kisiasa.
CHADEMA kupitia mgombea wake wa udiwani kata hiyo ya Nyampulukano, Zakaria Emmanuel Mnwanizi inatajwa kuwa katika nafasi nzuri ya kushinda nafasi hiyo huku CCM kupitia mgombea wake, Charles Gabriel Lugabandana ikitajwa pia kutoa upinzani mkali.
Kada wa CHADEMA anayedaiwa kuumizwa sehemu mbalimbali za mwili, ametajwa kwa jina la Rajab William Tunge.
Mkufunzi kutoka Kurugenzi ya Mafunzo ya CHADEMA Kanda ya Ziwa Magharibi, Baraka Nafari aliieleza Tanzania Daima kwamba, licha ya makada hao kushambuliwa na wafuasi wa CCM, lakini polisi wilayani Sengerema wamemkamata na kumuweka rumande Tunge.
“Sisi tumeshambuliwa, lakini polisi wamemkamata mtu wetu ambaye ameumizwa na wamemuweka selo. Tunalaani sana kitendo cha polisi hapa Sengerema kufanya kazi kwa maagizo ya CCM.
“Baada ya sisi watu wa CHADEMA kushambuliwa na gari letu T 869 AQK kuvunjwa vioo kwa mawe na wafuasi wa CCM, tulienda polisi tukakuta tumefunguliwa jalada la kuwashambulia watu wa CCM, wakati wao ndio wametuvamia na kutuumiza,” alilalamika Nafari.
Vyama vingine vinavyoshiriki katika uchaguzi huo mdogo Kata ya Nyampulukano, ni NCCR-Mageuzi na TLP.
Mkoani Arusha, kampeni za udiwani zinazotarajiwa kuhitimishwa leo kabla ya uchaguzi kesho, zimekuwa moto kutokana na matukio ya wafuasi wa CCM na CHADEMA kushambuliana na kulazimisha polisi kuingilia kati.
Habari kutoka Arusha zinasema kuwa Polisi wamekuwa wakiwakamata vijana wa CHADEMA na kuwaweka ndani kwa madai kuwa wamekuwa chanzo cha vurugu.
Chanzo: Tanzania Daima
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.