Wakiongea kwa nyakati tofauti katika tamasha hilo ambapo Kampuni ya Simu za mkononi ya Tigo ilikuwa ikitambulisha msimu wake mpya wa Tabasamu, uko na Tigo pamoja na kuufunga ule wa Jisikie Huru, ulitumika kwa miaka kadhaa iliyopita, wasanii hao walisisitiza kampuni kubwa kuwatambua wakitaka Tabasamu hilo lisiishie kwa mashabiki na kampuni hizo pekee, bali liwafikie wao pia.
Katika tamasha hilo ambalo burudani ‘ilibamba’ wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya, wamesema kwamba muda wa wao kutumiwa unastahili kufika mwisho wakizitaka kuiga mfano wa Tigo, ambayo walisema angalau imeonyesha mwelekeo.
Wasanii waliozungumza na mtandao huu katika fukwe hizo walisema kuwa muziki wao unatumika zaidi kwenye milio ya simu hata wakati mwingine katika matangazo ya biashara, lakini kwao kipato bado kidogo.
Wamewasihi wenye kampuni hasa za simu zinazojihusisha na kazi za sanaa kupitia upya rasimu ya malipo kwao.
“Tunashukuru Tigo wao angalau wameonyesha nia kwa kutuhusisha kwenye kampeni hizi na sasa wanatulipa vizuri na wengine waige,” alisema Mheshimiwa Temba kutoka Kundi la TMK Family, ambaye alipanda jukwaani siku hiyo na kuimba akiwa na Chegge Said.
Katika tamasha hilo, wasanii mbalimbali akiwamo Roma, Madee, Juma Nature na Rachel walikuwa nyota, huku Nature akitumia jukwaa hilo pia kumtambulisha msanii mwenye umri mdogo katika kundi lake la Wanaume Halisi, Dogo Lila, anayetajwa kuja kuwa mpinzani wa Dogo Aslay kutoka Kundi la Wanaume Family.
Kwa upande wake Rachel alikonga nyoyo za mashabiki kwa staili yake ya kunengua kiuno bila mfupa akizidi kujizolea mashabiki wengi hasa wa kike hasa kutokana na uchezaji huo huku akifananishwa na mwanamuziki Rehema Chalamila a.k.a Ray C.
Naye Juma Nature, kipenzi cha vijana wa mtaani aliibua shangwe baada ya kupanda jukwaani, huku Meneja wa Chapa ya Tigo, William Mpinga, akisema kuwa msimu huu ni maalumu kwa kampuni yake kuonyesha inavyojali jamii ya Watanzania.
“Safari hii tumedhamiria, huku tukibadilisha msemo wetu kutoka Kujisikia Huru, kwenda Tabasamu kwa kuwa uko nasi na kuhakikisha kweli kila mwanajamii kwa nafasi yake anatabasamu anapokuwa karibu na kampuni yetu au anapotumia mawasiliano ya kampuni yetu,” alisema Mpinga.
Tags
HABARI ZA WASANII