Maelezo ya Jumla ya Hadithi - Siri ya Mtungi
“Siri ya Mtungi” ni tamthilia ya televisheni inayofurahisha, inayoonyesha maisha ya Cheche, mpigapicha mwenye bashasha na mmiliki wa Studio ya Kupiga Picha ya Mtungi. Ana mke mrembo, Cheusi, aliyemzalia watoto wawili wenye afya na huku akiwa na ujauzito wa mtoto wa tatu.Cheche anampenda sana mkewe, lakini mawazo ya kuanzisha biashara mpya na kuwepo ujio wa mtoto mwingine wa tatu yanawapa wakati mgumu. Anajaribu kuwa baba mwema, lakini, kama ni uchawi au bahati tu, anawavutia sana wanawake…na wale makahaba! Cheche pia ana uhusiano wa karibu na mpenzi wake wa shuleni, Tula.Kizito, ni baba mkwe wake Cheche, aliyemsaidia kuanzisha biashara yake. Ni mtu anayeheshimika sana katika jamii ya Bagamoyo na kila mara anashughulika na watoto wake Nuru na Matona katika karakana yake ya magari. Pamoja na hayo, Kizito ana watoto wengine wengi aliozaa na wake zake watatu, Farida, Mwanaidi na Vingawaje, aliyefariki hivi karibuni.
Mhalifu wa mjini ni Masharubu, tajiri mwenye nguvu anayemiliki mabanda na biashara za kitapeli. Baada ya kuvumilia matusi kwa muda mrefu, mkewe alimkimbia na kumwachia binti yao mrembo, Nusura. Nusura ni ua la yungiyungi lililochanua kwenye lile geto. Ni mjanja, mwanamke shupavu ambaye udhaifu wake ni mahusiano yake na Duma, mmoja wa wapangaji wa Masharubu. Duma ana moyo wa dhahabu lakini anahangaika kimaisha kama DJ mjini Bagamoyo.Karibuni tu alimleta mdogo wake, Stephen, toka kijijini, ili mvulana huyo aingie shule ya kujitegemea na kupata fursa ya maisha bora lakini, mpaka muda huu Duma anashindwa kumtimizia mahitaji muhimu. Muhimu zaidi, Duma anashindwa kuwa mfano bora kwa mdogo wake, Stephen anayechoshwa na shule na kutaka kuwa ‘mtoto wa mjini’ kama kaka yake.
Nyendo za Nusura na Kizito zinapishana kuashiria bahati kwa Kizito, ambaye yuko tayari kuendelea mbele na maisha yake kufuatia kifo cha mkewe mdogo. Nusura kwa upande wake amechoshwa na wasiwasi katika mahusiano yake na Duma, hivyo yuko tayari kwa mambo ya kiungwana zaidi. Nusura anajikuta yuko njia panda kati ya penzi la Duma na lile lililotulia kama maji lenye uelekeo wa ndoa na Kizito. Hana ufahamu wowote kuwa kuna dhoruba inayochemka katika maji yale ya samawati. Siri zitasimuliwa, maisha kuchanwachanwa na mioyo kuvunjwa kwenye mji huu wa Bagamoyo.
‘Siri ya Mtungi’ imetayarishwa na MFDI Tanzania ikishirikiana na JHUCCP Tanzania kwa msaada wa Wau wa Marekani kupitia USAID.
Tamthilia hiyo itakuwa inarushwa hewani na vituo viwili hapa nchini navyo ni ITV na EATV, Itaanza kuruka hewani kuanzia Jumapili Tarehe 9/12/212 katika kituo cha ITV saa 3:30pm EAT, Na Kurushwa tena EATV Jumatano tarehe 12/12/2012 saa 3:30pm EAT .