Unknown Unknown Author
Title: SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 16
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 16 MTUNZI: NYEMO CHILONGANI ILIPOISHIA....!!! “Ni lazima niende Iran,” alijisemea. Hakutaka kuchelewa,...
SIMULIZI:: SITALIA TENA
SEHEMU YA 16
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI
SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 16
ILIPOISHIA....!!!
“Ni lazima niende Iran,” alijisemea.
Hakutaka kuchelewa, akaanza kufanya harakati za safari, baada ya saa moja, alikuwa na vibali vyote, akachukua ndege ya baba yake na kuondoka zake kuelekea huko huku moyo wake ukiwa na presha ya kumuona Saida aliyekuwa na mtoto wake tumboni.

SONGA NAYO SASA.....Ndani ya ndege Kareem alikuwa na presha kubwa, moyo wake ulikuwa na kiu kubwa ya kumuona Saida, aliiona ndege ikienda taratibu sana, mara kwa mara aliwaambia marubani kwamba walitakiwa kufanya haraka kwani kile alichokuwa akikifuata nchini Iran kilikuwa muhimu kuliko kitu chochote kile.

Kwa sababu kutoka Oman mpaka Iran hakukuwa mbali, walichukua saa mbili wakafika huko. Kareem akateremka na kuwasiliana na Saida na kumwambia hoteli aliyokuwepo, hakutaka kupoteza muda, akakodi teksi na kuanza kuelekea huko.

“Unaijua Al Muntaz ilipo?” aliuliza. “Hii hoteli ya nyota tano?” “Ndiyo! Unajua ilipo?” “Hakuna dereva teksi asiyeijua,” alijibu dereva huyo na kuanza kuelekea huko.

Moyo wake ulimkumbuka mpenzi wake, hakutaka kusikia kitu chochote kile kwa wakati huo, alikuwa akimfikiria Saida na ndiye mtu pekee aliyetaka kumuona kwa mara nyingine, aliufikiria ujauzito ule, mtoto aliyekuwa tumboni alikuwa muhimu sana.

Walichukua dakika kumi wakafika katika hoteli hiyo, harakaharaka akateremka na kumlipa dereva kisha kuelekea mapokezi. Hapo, alichokifanya ni kupanga chumba, hakutaka kugundulika lengo lake la kufika mahali hapo, alipopewa chumba, harakaharaka akaanza kuelekea huko.

Kwa sababu aliambiwa chumba alichokuwepo msichana huyo, akaufuata mlango na kuanza kuugonga. Saida ambaye alikuwa ndani aliposikia mlango ukigongwa, harakaharaka akaelekea mlangoni na kuufungua.

Hakuamini kama kweli alikutana na Kareem kwa mara nyingine, akamrukia mpenzi wake na kumkumbatia mpaka kutaka kudondoka chini. Wakajivuta mpaka ndani. Kila mmoja alikuwa akilia, walikata matumaini ya kuonana tena lakini mwisho wa siku walionana kitu kilichowapa furaha kila mmoja.

Kareem alimwangalia Saida mara mbilimbili, kwake, alionekana kama mzimu, alijua kabisa kwamba msichana huyo alifariki na asingeweza kumuona tena maishani mwake lakini kitu kilichomfurahisha, akakutana naye kwa mara nyingine tena.

“Siamini kama nimekutana na wewe tena mpenzi,” alisema Kareem huku akimwangalia Saida. “Hata mimi siamini. Nilidhani kwamba ndiyo ungekuwa mwisho wa kila kitu,” alisema Saida kwa sauti ya chini. “Kwa nini upo Iraq? Ilikuwaje? Niliambiwa kwamba ulitupwa baharini! Imekuwaje upo hapa? Tena siku chache niliona ukiwa umewekewa bunduki?” aliuliza Kareem, muda wote waliokuwa wakizungumza hayo walikuwa wamekumbatiana tu na hawakutaka kuachana.

“Ni stori ndefu sana mpenzi!” alisema Saida na kuanza kumuhadithia Kareem kile kilichokuwa kimetokea tangu alipoachana naye kule Muscat.

Kareem hakuamini, wakati mwingine alihisi kama Saida alikuwa malaika kwani matatizo yote aliyoyopitia, jinsi alivyokuwa akinusurika alihisi kabisa kwamba hakuwa binadamu, binadamu asingeweza kuwa na bahati kubwa kama aliyokuwa nayo.

“Ni lazima tuondoke hapa,” alisema Kareem. “Tunaondoka vipi?” “Kwani kuna ugumu gani?” “Nimewekewa ulinzi mkubwa huko nje!” “Tutaondoka tu! Wala usijali! Niachie mimi!” “Sawa! Ila kesho asubuhi natakiwa kuondoka!” “Kuelekea wapi?” “Syria!”

Kareem akashtuka, hakuamini alichokisikia, kwa maana hiyo ilikuwa ni lazima kuondoka hapo hotelini siku hiyohiyo. 

Ilikuwa ni usiku, hakujua angeondoka vipi lakini ilikuwa ni lazima kuondoka hotelini hapo siku hiyo.

Kareem hakutaka kubaki ndani ya chumba hicho, kwa haraka sana akatoka na kuelekea katika chumba alichotakiwa kukaa, alibaki humo huku akifikiria ni kwa namna gani angeweza kuondoka ndani ya hoteli hiyo pamoja na mpenzi wake, lilimuumiza kichwa, alikaa na kujifikiria na baada ya dakika kumi, akainuka, kitu kilichokuja kichwani mwake ni kwamba ilikuwa lazima kumtoa msichana huyo ndani ya hoteli hiyo kama tu angemtumia mhudumu wa ndani ya hoteli hiyo.

Akainuka, alionekana kuwa na haraka sana, kitu alichokifanya ni kuchukua simu na kupiga mapokezi kwamba alikuwa akihitaji huduma ndani ya chumba chake, baada ya dakika mbili tu, msichana mmoja akafika na kuingia chumbani kumsikiliza mteja kwani mwenyewe alitaka aingie ndani kwanza.

“Nikusaidie nini?” “Naomba uniokoe, nipo kwenye tatizo kubwa sana,” alisema Kareem huku akimwangalia msichana huyo. “Tatizo gani?” “Ninahitaji mavazi ya mhudumu wa hoteli hii! Naomba unisaidie,” alisema Kareem, wakati akiyaongea hayo, hakuishia kusimama, tayari mkono uliingia kwenye suruali yake, akatoa mabunda mawili ya fedha na kumpa mhudumu yule.

Zilikuwa ni rial laki mbili, hicho kilikuwa kiasi kikubwa sana, kwa mwezi ndani ya hoteli hiyo alikuwa akilipwa kiasi cha rial elfu saba tu ambacho kwa fedha za Tanzania ilikuwa ni zaidi ya laki saba, kitendo cha kuonyeshewa fedha hizo, macho yalimtoka.

“Rial laki mbili, naomba unisaidie,” alisema Kareem. “Za kike au kiume?” “Kike.”

Hakutaka kukiacha kiasi hicho cha fedha, akakichukua na kisha kutoka ndani ya chumba kile huku akionekana kutokuwa na hofu hata kidogo. Hakukuwa na kamera ndani ya chumba kile hivyo aliamini hakukuwa na mtu yeyote aliyemuona wakati anachukua kiasi hicho cha fedha.

Akaondoka mpaka katika chumba kilichokuwa na nguo nyingi pamoja na mataulo na mashuka, akachukua nguo zilizotakiwa na kisha kurudi ndani ya chumba hicho na kumpa Kareem, hakujua alitaka kutumia katika nini, alichokuwa amekiangalia ni fedha tu.

Alipozipokea, akamshukuru na kumuongeza bunda jingine lililompagawisha zaidi msichana huyo. Akashukuru tena. 

Akamuuliza namba ya simu ya chumba alichokuwa Saida, akapewa, msichana huyo alipoondoka tu, akachukua simu na kumpigia. “Saida...” aliita. “Abee...” “Tunaondoka leo hiihii, tena usiku huuhuu,” alisema Kareem. “Kivipi?” “Usijali! Niachie mimi, unachotakiwa ni kufanya kile nitakachokwambia. Ukifika saa 1.00 usiku, toka chumbani kwako, tembea kwa mwendo wa taratibu kuelekea katika choo cha wafanyakazi, utaukuta mlango ukiwa wazi, ingia humo. Humo ndani utakutana na nguo za wafanyakazi wa hoteli hii. Chukua sekunde hamsini tu kubadilisha na kuvaa haraka sana. Ukimaliza, ondoka kuelekea nje. Ukifika nje, saa 1.03 kuna gari litakuja na kusimama mbele ya hoteli, kuna mwanaume atateremka na kukwambia uingie, usisite, ingia. Umesikia?” alisema Kareem mfululizo.

“Ndiyo! Ila nitaweza?” “Naamini utaweza!”

Alipomaliza kuzungumza maneno hayo, akakata simu na kisha kutoka chumbani humo. Alichokitaka kilikuwa ni kutafuta gari, alitaka kukodi kwa siku nzima kwani hiyo ndiyo ambayo ingetumika katika kumtorosha Saida hapo hotelini.

Hilo halikuwa tatizo, kwa sababu alikuwa na fedha, akafanikiwa kupata gari. Saa 1.05, akamuona mfanyakazi wa hoteli hiyo akitoka ndani ya hoteli, ilikuwa ngumu kugundua kwamba mtu huyo alikuwa Saida.

Alivalia mavazi ya mfanyakazi wa hoteli hiyo, alikuwa na nikabu na hata wale watu waliokuwa wakihakikisha analindwa, alipokuwa akiteremka hakukuwa na aliyejua kwamba alikuwa Saida.

Alipofika nje, akaliona gari limefika kama alivyoambiwa lakini cha ajabu, mtu aliyeteremka alikuwa Kareem. Hakutaka kuuliza, akafungua mlango na kuondoka mahali hapo kwa mwendo wa kawaida.

Wafanyakazi wengi wa hoteli ile ambayo walimuona Saida akiingia ndani ya gari lile walishangaa, hawakujua alikuwa nani, haikuwa kawaida kwa mfanyakazi kuondoka muda huo tena huku akiwa na mavazi ya kazi, wakahisi kulikuwa na kitu, inawezekana alifiwa.

“Siamini kama nimetoka salama,” alisema Saida huku akizivua nguo zile alizokuwa nazo, akapewa boksi lililokuwa na nguo nyingine, akalichukua na kuzitoa nguo hizo na kuvaa humohumo garini.

“Tunaondoka kuelekea Dubai,” alisema Kareem. “Halafu Tanzania?” “Ndiyo! Hapa tunakwenda uwanja wa ndege, nimekuja na ndege ya baba, tutaingia na kundoka, hilo wala usihofu kabisa,” alisema Kareem huku akitoa tabasamu pana.

Safari ilikuwa ikiendelea kama kawaida, kila mmoja alijua kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa kuteseka, ndiyo ungekuwa mwisho wa kuhangaika kurudi nchini Tanzania.

Wakati wamefika karibu na soko kuu la Musjadiakr lililokuwa katikati na Mji wa Bandar Abbas, wakashtukia kuona magari mawili yakija kwa kasi, yakawavuka na kisha kwenda mbele yao na kuziba njia.

Hata kabla Kareem hajajua ni kitu gani alitakiwa kufanya, wanaume wanne waliokuwa na bunduki wakateremka, kitu cha kwanza wakapiga risasi tano hewani, watu wote wakatawanyika, wakalifuata gari hilo, wakawateremsha wote wawili kinguvu na kuanza kuondoka nao.

“Who the hell are you?” (nyie ni wakina nani?) aliuliza Kareem lakini hata kabla hajapewa jibu, akapigwa kitako cha uso, akaona giza mbele yake, damu zikaanza kumtoka, wala hazikupita hata sekunde kumi, akapoteza fahamu, hakujua ni kitu gani kiliendelea baada ya hapo.

Je, nini kitaendelea? Je, tayari Serikali ya Oman imewakamata? Kwa nini safari ya kwenda Tanzania inakuwa ndefu hivi? USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

++++++++++++++++++++++++++++++++++++++

++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
KUWA KARIBU NASI LINDIYETU.COM
Usipitwe!! Ungana na Familia hii kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata Infortainment zote!! Usikose kujiunga na Youtube channel yetu ili kupata Exclusive mbalimbali kali kutoka LindiYetu TV

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top