Unknown Unknown Author
Title: SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 13
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 13 MTUNZI: NYEMO CHILONGANI ILIPOISHIA.....!!! Walichokuwa wakikihitaji kilikuwa ni mzigo wa madawa ...
SIMULIZI:: SITALIA TENA
SEHEMU YA 13
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI

SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 13
ILIPOISHIA.....!!!
Walichokuwa wakikihitaji kilikuwa ni mzigo wa madawa ya kulevya ambayo waliamini kwamba ndiyo ungekuwa mtaji wao wa kufanya biashara yao. Hawakumjua Saida, walikutana naye tu baharini, hawakujua alitoka wapi na alikuwa akielekea wapi na ndiyo maana hata kumuweka kama bondi.

SONGA NAYO SASA....
Kareem alichanganyikiwa, hakuamini kile alichokisikia kutoka kwa rafiki yake kwamba mpenzi wake, Saida alikuwa ametupwa baharini. 

Aliondoka na boti yake, njiani, machozi yalikuwa yakimbubujika, alilia sana kwani huo haukuwa muda wa kumpoteza Saida, alitakiwa kuwa naye maisha yake yote na ndiyo maana alijitolea kwa kila kitu, hata kama ni pesa, alikuwa tayari huku akitaka kumuona akifika Tanzania salama kabisa.

Bahari ilitisha, alizunguka sehemu kubwa, aliogopa lakini hakutaka kurudi nyuma, lengo lake lilikuwa ni kumtafuta Saida mpaka ampate. Alizunguka kwa siku nzima, akamkosa, akakata tamaa na kuona kwamba tayari msichana huyo alifariki dunia baharini hivyo akaamua kurudi nyumbani.

Aliomboleza, alikosa amani, juhudi zote alizokuwa amezifanya zilikuwa kubwa lakini hakuwa na jinsi, akatulia nyumbani na moyo wake ukimwambia kwamba tayari Saida alikuwa amekufa baharini.

Maumivu hayakutoka, baada ya mwezi mmoja huku bado kichwa chake kikimfikiria msichana huyo, akaona taarifa kwenye Mtandao wa WhatsApp kwamba kulikuwa na msichana alikuwa katikati ya wanaume wawili walioshika bunduki, nyuso zao zikiwa zimezibwa na vitambaa wakiwataka watu waliomuweka mwanamke huyo kama bondi waende kuwalipa fedha zao na kumchukua kwani vinginevyo wangemuua.

Alimwangalia vizuri mwanamke yule, alikuwa Saida. Hakuamini alichokuwa akikiona, Saida alikuwa akilia, tumbo lake lilianza kuonekana. Kareem akabaki akitetemeka, hakuamini alichokuwa akikiona kama kweli msichana aliyekuwa akimwangalia alikuwa Saida au msichana mwingine.

Hakuridhika, akaona kama kwenye simu hakuwa akiona vizuri, alichokifanya ni kuichukua ile video na kuiweka kwenye kompyuta yake ili aweze kumwangalia mwanamke yule kwa umakini, ni kweli alikuwa Saida na tumbo lilianza kuonekana.

“Imekuwaje? Imekuwaje awe hai? Ni yeye au?” alijiuliza huku akionekana kushangaa.

Wakati yeye akijiuliza, video ile ilikuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii, Serikali ya Oman ilipomuona Saida, ikamkumbuka kwamba msichana huyo ndiye yule aliyekuwa akitafutwa kwa udi na uvumba mara baada ya kutoroshwa siku ambayo alitakiwa kufa. Alifikaje huko? Ilikuwaje mpaka awe mikononi mwa wauza madawa ya kulevya?

“Ni lazima akamatwe na kurudishwa huku. Waambie vijana wa IT waangalie hiyo video imepigwa wapi,” alisema Kamanda Mkuu wa Jeshi la Polisi hapo Oman.

Watu wa IT wakaingia kazini, ilikuwa ni lazima wagundue mahali ambapo video ile ilichukuliwa, uzuri ni kwamba ilipigwa nje na si ndani hivyo ilikuwa rahisi sana kugundua kwamba video hiyo ilichukuliwa kutoka nchini Iran katika Mji wa Bandar Abbas sehemu iitwayo Shamiliha.

Hakukuwa na muda wa kupoteza, ilikuwa ni lazima wawasiliane na polisi wa Iran kitengo cha Interpool na kuwaambia kwamba kulikuwa na mtuhumiwa ndani ya nchi yao hivyo ilikuwa ni lazima akamatwe haraka iwezekanavyo.

“Mmesema wapi?” aliuliza polisi kutoka Iran. “Shamilaha!” “Shamilah?” “Ndiyo!” “Mmh!”

Polisi hao walijua fika eneo hilo alikuwa akiishi muuzaji gani wa madawa ya kulevya, walimfahamu mzee Sadiq Al Duwir, naye alikuwa muuzaji mkubwa wa madawa ya kulevya ambaye alikuwa akihonga sana serikalini kwa lengo la kulindwa.

Hakutaka kusakamwa, hakutaka kufuatiliwa na polisi yeyote yule na ndiyo maana alitumia kiasi kikubwa kuwahonga wakuu wa nchi. Polisi walipopewa taarifa hiyo, wao wenyewe wakashindwa la kusema kwani walijua fika kwamba mtu huyo alikuwa hatari, mwenye nguvu ambaye hakutaka kuambiwa lolote lile.

“Ila...” “Kama mtashindwa semeni tuwalete polisi wetu,” alisema polisi kutoka Oman. “Subiri niongee na kiongozi.”

Tayari kukaonekana kuwa na ugumu katika suala hilo. Saida alikuwa mtu muhimu sana, alitafutwa na serikali kila kona.

Wananchi wote kipindi hicho walikuwa wakisikilizia serikali ingefanya nini kwani kama kutafutwa, mtu huyo alitafutwa sana.

“Ni lazima tutume jeshi huko,” alisema waziri mkuu wa nchi hiyo.

Hawakuwa na jinsi, siku hiyohiyo jeshi la Oman likatumwa nchini Iran kwa ajili ya kumkamata Saida ambaye aliikimbia adhabu ya kifo nchini Oman. Ndege zilikuwa zikienda kwa kasi mno, baada ya nusu saa tu, tayari zikafika nchini humo katika kambi ya kijeshi iliyokuwa Golkan ambapo hakukuwa mbali kutoka Shamilaha.

“Ndege mbili ziende, moja iende upande wa Kusini na nyingine Kaskazini. Wanajeshi wengine waende kwa gari, hii ni misheni ambayo hatuhitaji mtu yeyote kutuingilia. 

Tumekwisha zungumza na jeshi la hapa Iran, tumeruhusiwa, hatupo hapa kupambana bali kumchukua mtu wetu,” alisema kamanda mkuu wa jeshi lililokwenda huko.

“Sawa mkuu!” “Najua wote mnajua mahali alipo. Katika Mji wa Shamilaha, kuna jumba moja kubwa, lina ghorofa nne, kuna uzio mkubwa, ni lazima twende usiku huuhuu. Tuna GPS, tayari tumechukua mtambo unaotuonyesha mtuhumia alipo. Ni lazima twende usiku huuhuu. Kumbukeni kwamba hakuna kuua, ila inapotokea, hatuna jinsi,” alisema kamana huyo. 

Hapohapo wa ndege wakapanda na wa magari yaendayo kasi wakapanda. Ilionekana kama jeshi limeingia vitani kumbe lilikuwa likienda kumkamata mtu aliyezini tu Oman, tena mwanamke ambaye wala hakuwahi kuwa mwanajeshi au gaidi.

*********************************** 
Mzee Sadiq Al Duwir hakuonekana kuwa na hofu kabisa, moyoni mwake aliamini kwamba vijana waliokuwa wamemuweka bondi Saida wangeweza kurudi kwake kumlipa fedha na kuwapa mtu wao.

Alikaa na Saida vizuri tu huku akimtaka asitoke ndani ya jumba hilo kubwa. Aliwaambia vijana wake kwamba wafanye kila linalowezekana ili msichana huyo asitoke ndani kwani kichwa chake kilikuwa fedha nyingi tu.

Saida hakuwa na amani, alishindwa kuelewa sababu zilizomfanya kunusurika kifo huku akichukukuliwa na kuingia kwenye hatua nyingine ya kifo. Alikuwa mtu wa kulia tu, aliyakumbuka maisha aliyoishi nchini Tanzania, alipata kila kitu, aliishi kwa amani kabisa lakini mwisho wa siku, maisha yakabadilika, akaishi kwa hofu kubwa huku kila wakati akikichungulia kifo.

Alipewa chakula kizuri, alikula lakini hakuyafurahia maisha kabisa. Alikuwa katika nchi ngeni, hakumfahamu mtu yeyote yule, wote, kwake walionekana kuwa wageni.

Baada ya wiki moja kuwa kwenye jumba hilo, Saida akaanzisha urafiki na mwanaume aitwaye Ahmed Said. Alikuwa mwanaume mwenye sura nzuri, mwembamba, aliyekwenda hewani, ndevu nyingi ambazo alizipaka hina.

Kila siku wawili hao walikuwa wakizungumza pamoja kama marafiki. Mbali na kuzungumza sana, Ahmed akagundua kwamba Saida hakuwa mtu mwenye furaha, akahisi kulikuwa na kitu nyuma ya pazia tofauti na watu ambao walikuwa wakiwekwa bondi kwa mzee huyo.

Alimzoea, hakutaka kujificha, akamuuliza nini lilikuwa tatizo lake, Saida hakusema, hakuona kama angeweza kusaidiwa na mwanaume huyo kwani kwa jinsi alivyokuwa akimwangalia, aliona akiwa kama wanajeshi wengine waliokuwa ndani ya jumba hilo.

Alimdanganya lakini baada ya siku ishirini kupita, akamwambia ukweli tangu alipokuwa kwenye meli na kutupwa baharini na baadaye kuokotwa na vijana waliokwenda kumuweka bondi.

“Pole sana...kwa hiyo si ndugu zako?” “Ndiyo! Waliniokoa na sikujua kama wangekuja kuniweka huku.” “Kwa maana hiyo hakuna uwezekano wa wao kurudi. Pole sana,” alisema Ahmed huku uso wake ukionyesha ni jinsi gani alimuonea huruma msichana huyo.

Mzee Sadiq Al Duwir alikuwa akihitaji fedha zake, kila wakati alikuwa akiwasiliana na vijana waliomletea Saida lakini hawakumwambia siku ya kupeleka pesa hizo kwani kama mzigo, walimwambia kuwa ulikwisha.

Alisubiri mpaka ulipofika mwezi mmoja ndipo akawaambia vijana wake watengeneze video huku wakiwa na Saida na kuwataka watu walioacha mzigo wao warudi kulipia fedha walizotakiwa kulipa na kumchukua mtu wao.

Wakamchukua Saida na kuanza kujirekodi video hiyo huku wakionyesha bunduki ambazo wangezitumia kumuua msichana huyo endapo tu wasingelipwa fedha zao. 

Baada ya kumaliza kurekodi video hiyo, ikatupwa katika mitandao ya kijamii na kuanza kuzunguka dunia nzima. Kila mtu aliyeitazama, alishangaa na kumuonea huruma msichana huyo.

Je, nini kitaendelea? Je, Saida atakufa? Je, itakuwaje akikamatwa na kurudishwa Oman?
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
KUWA KARIBU NASI LINDIYETU.COM
Usipitwe!! Ungana na Familia hii kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata Infortainment zote!! Usikose kujiunga na Youtube channel yetu ili kupata Exclusive mbalimbali kali kutoka LindiYetu TV

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top