SIMULIZI:: SITALIA TENA
SEHEMU YA 12
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI
SEHEMU YA 12
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI
ILIPOISHIA....!!!
Alichokifanya ni kuchukua boti ya baba yake, hakutaka kuwaaga, akaondoka Oman na kuanza kuelekea huko baharini, hakujua kulikuwa na umbali gani ila kwa sababu alikuwa na nahodha ambaye alifahamu njia za kuelekea Dubai, hakuwa na hofu, hata kama angeipata maiti yake, ingemfariji kuliko kuikosa na kuliwa na samaki.
ENDELEA NAYO SASA...
Mustaf Al Jabir alikuwa miongoni mwa wauza madawa ya kulevya maarufu nchini Pakistan hasa ndani ya Jiji la Karach. Kila mtu alimfahamu kama mfanyabiashara mkubwa aliyekuwa akimiliki hoteli nyingi za nyota tano pamoja na visima vya mafuta nchini humo.Alijijengea jina kubwa Pakistan, watu wengi walimpenda kwani bilionea huyo hakuwa na roho mbaya, maisha yake yote yalitawaliwa na upendo mkubwa aliokuwa akiwafanyia wananchi wenzake kwa kuwajengea shule, hospitali, barabara na kuwapelekea maji ambayo yalikuwa ni ya shida mno huko Karach na nchi nyingine zilizokuwa na jangwa.
Alipendwa, serikali ilijua kwamba mtu huyo alikuwa akijihusisha na biashara hiyo haramu lakini hawakuweza kumkamata, walijua nguvu kubwa aliyokuwa nayo, namna alivyokuwa akiwapenda wananchi na kuwapa kila kitu walichokuwa wakikihitaji.
Alikuwa na kundi kubwa la vijana ambao walikuwa wakiyasafirisha madawa hayo kwenda nchi mbalimbali duniani. Wapo waliokuwa wakisambaza katika bara hilohilo la Asia, wapo waliokuwa wakipeleka Afrika na wengine walipeleka mpaka Marekani kitu kilichomfanya kuwa na utajiri mkubwa mno.
Vijana wake walijulikana kila kona, katika viwanja vingi vya ndege, bandarini na sehemu nyingine zote. Kila siku akaunti yake ilikuwa ikisoma kiasi kikubwa cha fedha huku akikisiwa kuwa bilionea wa kwanza duniani kutokana na utajiri mkubwa aliokuwa nao ila kwa sababu alijihusisha sana na madawa ya kulevya, hakuwekwa katika orodha ya mabilionea wakubwa.
Alijijengea heshima kubwa, kila alipokuwa aliwekewa ulinzi mkubwa. Wapakistan walimpenda, walimsujudia kwani mbali na utajiri mkubwa aliokuwa nao, yeye ndiye aliyekuwa na uwezo wa kuikopesha fedha serikali ya nchi hiyo na nchi nyingine jirani kama Afghanistan, India, Iran na nchi nyingine nyingi.
Mizigo yake mingi alikuwa akiituma kupitia majini, aliamini kwamba huko kulikuwa salama kuliko angani. Kila wiki ilikuwa ni lazima awatume vijana wake kupeleka mizigo Afrika na sehemu nyingine kupitia majini.
Walikuwa wakiisafirisha huku wakilihonga jeshi la maji kiasi kikubwa cha fedha. Meli zote zilizokuwa zikipita baharini zilikuwa zikikaguliwa lakini meli za Mustaf Al Jabir zilipokuwa zikipita, hakukuwa na askari aliyethubutu kuzikagua kwani tayari mabosi wao walipewa kiasi kikubwa cha fedha.
Wakati Saida akiwa anazama majini, meli ambayo ndiyo ilikuwa ikipita katika eneo hilo ilikuwa ni ya Mustaf Al Jabir ambayo ilikuwa ikielekea Dubai kwa ajili ya kupeleka madawa ya kulevya kama kawaida.
Nahodha aliyekuwa akiiongoza meli hiyo, kwa mbali aliweza kuliona pipa moja kubwa likiwa baharini, alipopiga tochi yenye mwanga mkali, akamuona mtu mmoja akiwa amelishikilia pipa hilo.
Hakupiga honi, alichokifanya ni kuwaita wenzake na kuwaambia kile alichokiona, wenzake wote wakapiga macho mahali pale, walimuona mtu huyo kwa mbali lakini alionekana kuchoka na kukata tamaa, na baada ya sekunde chache akaliachia pipa lile na kuanza kuzama, wakajaribu kupiga honi ili kumshtua kwamba kulikuwa na msaada lakini mtu huyo alikuwa amekwishazama.
“Tufanye nini?” aliuliza nahodha, alionekana kuchanganyikiwa. Japokuwa alikuwa akipiga mishe za madawa ya kulevya, lakini alikuwa mwanaume mwenye huruma mno.
“Sayyed....Nenda kamuokoe...” alisema jamaa mmoja, aliyeitwa Qadir alikuwa akimwambia mwenzake.
Kwa haraka sana kijana aliyejulikana kwa jina la Sayyed akavua kanzu yake harakaharaka na kuzama baharini. Huyo ndiye aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kuogelea kuliko wengine, alijua kubana pumzi kwa muda mrefu na ndiye ambaye alikuwa akichukua kiasi fulani cha dawa ya kulevya kilichokuwa kwenye mfuko wa nailoni na kuzama nacho majini kama tu walitaka kuyapitisha sehemu fulani.
Akaingia baharini, akapiga macho huku akiwa na tochi, kwa mbali akamuona mtu huyo akiendelea kuzama kuelekea chini, hakutaka kuchelewa, harakarahaka kwa mwendo wa kasi akamfuata, akamkuta na kisha kumchukua na kuanza kupanda naye juu.
Wenzake walipomuona, wakamtupia boya ambalo akalishika huku akiwa na mtu huyo kisha kuanza kuvutwa. Kila mmoja alishangaa, mtu aliyekuwa akizama alikuwa mwanamke, hawakujua alikuwa nani na ilikuwaje mpaka kufika hapo baharini.
Wakamchukua na kumlaza chini kisha kuanza kumkandamiza kwa ajili ya kuyatema maji aliyokuwa ameyameza, walifanikiwa kwa kiasi kikubwa, wakamchukua na kumpeleka kitandani, hapo akatulia.
Kila mmoja alikuwa na maswali, hawakujua ni kitu gani kilitokea kwa msichana huyo, walitaka kufahamu hilo hivyo walisubiri kwa hamu kubwa azinduke ili awaambie sababu ya kuwa baharini pale, sehemu iliyokuwa hatari sana kwa maisha yake.
“Alikuwa anafanya nini hapa?” aliuliza nahodha Ishmael.
“Hata sisi wenyewe hatujui, cha msingi tusubiri arudiwe na fahamu ili tumuulize,” alisema Sayyed.
Kila wakati walikuwa wakiingia ndani ya chumba hicho wakimwangalia Saida, kila mmoja alitamani kumuona msichana huyo akirudiwa na fahamu na kuwaambia kile kilichokuwa kimetokea.
Waliona muda ukienda lakini msichana huyo bado hakuwa amerudiwa na fahamu. Zilipita saa mbili ndipo Saida akayafumbua macho yake. Alishangaa kujiona akiwa kitandani, hakujua alikuwa wapi na kwa namna gani alikuwa mahali hapo, akainuka na kukaa kitandani.
Chumba kilikuwa kizuri sana lakini alipoona hapo alipokuwa kukiyumbayumba, akahisi kwamba alikuwa ndani ya meli. Alifikaje hapo? Akaanza kukumbuka. Mara ya mwisho kabisa alikumbuka kwamba alikuwa baharini, alikata tamaa na alikuwa tayari kwa ajili ya kufa na hivyo kuzama ndani ya maji, kilichotokea hapo, hakujua.
Wakati akijiuliza, mara mlango ukafunguliwa na Sayyed kuingia, kwanza uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana. Alichokifanya kabla ya kuzungumza kitu chochote kile ni kuchukua chupa ya uji na kisha kumpa, harakaharaka Saida akanywa, akamaliza na kuongeza tena, akanywa, alikunywa vikombe vitatu vikubwa ndipo akakaa sawa.
“Who are you? What were you doing here?” (Wewe ni nani? Ulikuwa unafanya nini hapa?) aliuliza Sayyed huku akimwangalia msichana huyo.
“My name Fatma Ahmed....” (naitwa Fatma Ahmed) aliamua kudanganya.
“What were you doing here in the middle of the see?” (ulikuwa ukifanya nini hapa katikati ya bahari?) aliendelea kuuliza Sayyed.
Alichokifanya Saida ni kumwambia kwamba alikuwa safarini kuelekea Dubai lakini kwa bahati mbaya watu aliokuwa nao ndani ya meli hiyo waliamua kumtosa baharini baada ya kugundua kwamba alikuwa amezamia.
Sayyed akasikitika sana, alichokifanya ni kuwaita wenzake na kuwaambia vilevile kwamba alikuwa amezamia kwenye meli, ila akatoswa baharini. Kwa jinsi alivyokuwa mrembo, kila mtu akasikitika, msichana kama yeye hakutakiwa kupata mateso kama aliyokuwa ameyapata.
Wanaume hao wakajitambulisha kwamba walikuwa watu salama hivyo hakutakiwa kuwa na hofu yoyote ile, alichotakiwa ni kuvumilia na mwisho wa siku wangefika naye Dubai na hivyo kumuacha aondoke.
Kidogo Saida akapumua, akaona kwamba sasa alikuwa akielekea Dubai bila tatizo lolote lile, alimshukuru Mungu kwani hakuamini kama kweli angepata msaada mkubwa namna hiyo. Alitamani kumpigia simu Kareem na kumwambia kilichokuwa kimetokea lakini hakutaka kumwambia kipindi hicho, alisubiri mpaka watakapoingia Dubai.
Alipewa kila kitu ndani ya meli hiyo, walikaa naye na kumfanya kama ndugu yao. Kwa kuwa yeye ndiye alikuwa msichana pekee ndani ya meli hiyo, akawa anapika chakula na kula.
Aliwaamini watu hao, aliwaona kwamba walikuwa watu wazuri lakini nyuma ya pazia, hawakuwa watu wazuri kama walivyokuwa akijionyesha, walikuwa watu wabaya na ilikuwa ni afadhali kufa baharini kuliko kukutana na watu hao ambao vichwa vyao vilikuwa vikifikiria mambo mengi sana.
“Tumepata tulichokuwa tukikihitaji!” alisema Sayyed.
“Ndiyo hivyo! Kwa hiyo sasa hivi mzigo utachukulika, si ndiyo?” aliuliza Qadir.
“Kama kawaida. Tukitoka Dubai, hakuna kurudi Karach, kwanza ni kwenda Iran kuchukua mzigo wetu tufanye yetu halafu tukauze mzigo wetu,” alisema Ishmael.
Wao walikuwa vijana wa mzee Mustaf Al Jabir, walikuwa wakimfanyia biashara kwa kipindi kirefu huku wakiwa waaminifu kwa kila mzigo waliokuwa wakipewa. Siku zilizidi kwenda mbele, mzigo waliokuwa wakipewa ulikuwa ukipimwa na haukutakiwa kupungua uzito kwa staili yoyote ile.
Hilo liliwaumiza, kwa kipindi kirefu walitamani kufanya biashara yao lakini tatizo likawa moja tu kwamba hawakuwa na fedha na hata mzigo hawakuwa nao. Waliwafahamu wafanyabiashara wote, walijua mahali walipotakiwa kuchukua mzigo, hawakuwa na fedha yoyote ile lakini waliambiwa kwamba kama wangekuwa na mtu wa kumuweka bondi, lisingekuwa tatizo, wangepewa mzigo wakauze.
Kitendo cha kumpata Saida, kikawapa uhakika kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wa matatizo waliyokuwa nayo kwani wangewafuata wauza madawa ya kulevya na kuwaachia Saida huku wao wakipewa mzigo wa madawa ya kulevya na kuondoka nao kwenda kuuuza.
Safari iliendelea na baada ya siku mbili, wakafanikiwa kufika Dubai salama. Hiyo ilikuwa furaha kwa Saida kwani aliamini kwamba watu hao wangemuacha aondoke zake lakini kitu kilichomshangaza, watu hao hawakumuacha.
“Kwa nini hamtaki niondoke?” aliuliza Saida.
“Subiri kwanza.”
“Nisubiri nini?”
“Tumekwambia usubiri! Husikii?” alisema Sayyed kwa hasira kiasi kwamba Saida akaogopa.
Waliijua kwamba kama wasingemdhibiti basi angeleta tatizo, walichokifanya ni kumchukua na kumfungia katika chumba kimoja, hawakutaka aondoke, na kama chakula, walimpa kila walipopika.
Saida hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, hakujua sababu iliyowafanya watu hao kuamua uamuzi kama huo wa kumfungia. Walionekana watu wazuri, wema lakini kwa kile walichokuwa wakimfanyia, tayari akawaona watu hao kuwa wakatili.
Akakaa chumbani humo huku akilia, alijuta, wakati mwingine alitamani kuona akifa ndani ya bahari kuliko kuokolewa na watu ambao waliamua kumuonyeshea makucha kwamba hawakuwa watu wazuri japokuwa kipindi cha nyuma nyuso zao zilionyesha tabasamu pana.
Kumbukumbu zake zikarudi kwa Kareem, mwanaume huyo aliyekuwa akimpenda alimfanyia kila kitu katika maisha yake, alithubutu kufanya vitu vya hatari ili mwisho wa siku awe salama lakini safari yake ya kutoka Oman na kwenda Dubai tayari ilikuwa na misukosuko mikubwa.
Mara baada ya mzigo kushushwa hapo Dubai, siku mbili mbele safari nyingine ikaanza, walitakiwa kurudi Karachi nchini Pakistan lakini kwa sababu tayari walimpata mtu wa kumuwekea bondi, wakaona ingekuwa afadhali kuunganisha mpaka Iran.
Wakati Saida akilia njia nzima lakini kwa wanaume hao ilikuwa ni furaha tele, kila wakati walikuwa wakigongesheana chupa za pombe kwa kuamini kwamba nao wangekuwa wafanyabiashara wakubwa tu kupitia Saida.
Kutoka Dubai mpaka Bandar Abbas nchini Iran hakukuwa mbali, walitumia siku moja njiani wakafika hapo. Walichokifanya ni kuwasiliana na bwana Sadiq Al Duwir na kumwambia kwamba walitaka kuonana naye kwani kulikuwa na biashara waliyotaka kuifanya.
Hilo halikuwa tatizo, walichokifanya ni kuelekea nyumbani kwake huku wakiwa na Saida aliyetakiwa kutulia vinginevyo angeuawa, hivyo akatulia. Walipofika huko, ndani ya jumba kubwa, lililozungushiwa ukuta mrefu wenye nyaya za umeme kwa juu huku kukiwa na walinzi zaidi ya kumi waliokuwa na bunduki mikononi mwao.
“Tulia, tena unatakiwa kuonyesha tabasamu pana, vinginevyo hutotoka salama humu,” alisema Sayyed huku akimwangalia Saida ambaye kwa hofu kubwa, akaanza kutabasamu kwa kuogopa kuuawa.
Wakaingia ndani, sebuleni ndani ya nyumba hiyo, wakatulia kwenye makochi makubwa, nyumba nzima ilikuwa na kamera ndogo za CCTV ambazo zilifungwa katika kila kona, wakatulia hapo mpaka mzee Sadiq Al Duwir alipotokea na kuzungumza nao.
“Tumekuja kuchukua mzigo,” alisema Qadiri.
“Mmekuja na hela leo?”
“Hapana. Tumekuja na huyu mtu mumshike kama bondi. Tukiuza mzigo, tunakuja kukupa hela halafu unatupa mtu wetu,” alisema Ishmael.
“Hakuna tatizo. Mzigo wa kiasi gani?”
“Dola milioni moja.”
“Sawa ila kama mkikaa mwezi mzima hamjarudi, kama kawaida yangu namuua kama nilivyowahi kufanya kwa wengine,” alisema mzee Sadiq Al Duwir.
“Hakuna tatizo. Ila amini kwamba tutarudi,” alisema Ishamael.
Hilo halikuwa tatizo, kwa wafanyabiashara wa madawa ya kulevya, biashara ya namna hiyo ilikuwa ikifanyika sana, walichokifanya ni kumuacha Saida mikononi mwa mzee huyo katili kisha wao kuchukua mzigo wa madawa ya kulevya na kuondoka nayo huku wakiwa na furaha tele.
“Kweli tumrudie yule msichana?” aliuliza Sayyed.
“Ili iweje? Hii ndiyo imetoka. Mzigo mkubwa sana, hakuna kurudi, kama wakitaka kumuua, acha wamuue, hakuna kurudi tena,” alisema Sayyed huku akiachia tabasamu pana.
Walichokuwa wakikihitaji kilikuwa ni mzigo wa madawa ya kulevya ambayo waliamini kwamba ndiyo ungekuwa mtaji wao wa kufanya biashara yao. Hawakumjua Saida, walikutana naye tu baharini, hawakujua alitoka wapi na alikuwa akielekea wapi na ndiyo maana hata kumuweka kama bondi.
Je, nini kitaendelea? Usikose Sehemu inayofuata.
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
KUWA KARIBU NASI LINDIYETU.COM
Usipitwe!! Ungana na Familia hii kupitia Facebook, Twitter na Instagram ili kupata Infortainment zote!! Usikose kujiunga na Youtube channel yetu ili kupata Exclusive mbalimbali kali kutoka LindiYetu TV
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.