Unknown Unknown Author
Title: ZAHANATI YAKOSA CHOO NA SHIMO LA KUTUPA TAKA NGUMU, WAJAWAZITO WALAZIMISHWA KUONDOKA NA "UCHAFU" WAO BAADA YA KUJIFUNGUA
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
AKINAMAMA  wajawazito wanaokwenda kujifungua katika zahanati ya Buganika wilayani Kishapu mkoani wamekumbwa na changamoto ya kulazimisha...

AKINAMAMA wajawazito wanaokwenda kujifungua katika zahanati ya Buganika wilayani Kishapu mkoani wamekumbwa na changamoto ya kulazimisha kubeba uchafu wao mara baada ya kujifungua kutokana na kukosekana kwa choo wala eneo la kutupia taka ngumu katika zahanati hiyo.

Hali hiyo imeonekana wauguzi kuwalazimisha wajawazito kwenda wakiwa wamebeba mifuko ya rambo kwa ajili ya kubebea makondo ya nyuma na uchafu mwingine baada ya kujifungua jambo ambalo ni hatari kiafya ikiwa hutozwa kiasi cha shilingi 10,000 kama gharama za huduma badala ya wajawazito kutibiwa bure kwa mujibu wa sera ya afya.

Akizungumzia hali hiyo hivi karibuni mjini Shinyanga mmoja wa wezeshaji kutoka mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Anna Sangai alisema wakazi wa kijiji cha Buganika walitoa malalamiko hayo wakati wa zoezi la uraghabishi katika vijiji vya Buganika, Mwabayanda, Ngh’wigumbi na Buchambi ambapo baadhi ya wakazi wa maeneo hayo walihoji utaratibu huo iwapo unatumika kwingineko.

Sangai ambaye ni Ofisa utafiti, ushawishi na ujenzi wa pamoja alisema kitendo cha wajawazito kulazimishwa kubeba uchafu wao baada ya kujifungua kinahatarisha afya zao pamoja na watoto waliozaliwa kwa vile hawana utaalamu wa jinsi ya kuhifadhi uchafu huo usiweze kuwaletea madhara au kuliwa na mbwa na wanyama wengine kama fisi.

Pia alisema wauguzi katika zahanati hiyo wanakiuka sera ya afya nchini kwa kuwatoza fedha wajawazito wanaokwenda kujifungua huku wakiwalazimisha kwenda na maji, taa au tochi kwa ajili ya kuvitumia iwapo watajifungua nyakati za usiku kutokana na zahanati kutokuwa na nishati ya umeme na mafuta ya taa kwa ajili ya taa zilizopo kituoni.

Mwezeshaji huyo alisema ni muhimu hivi sasa jamii ikaelimishwa ili kuzielewa haki zao za msingi wanazostahili kupatiwa kwa mujibu wa sera za nchi ambapo alitoa wito kwa waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuweza kutoa elimu ya kina itakayosaidia jamii iondokane na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika maeneo yao.

Kwa upande wake mganga mkuu wa wilaya ya Kishapu, Dkt. Daniel Msaningu alikiri zahanati hiyo kutokuwa na choo na eneo la kutupia taka ngumu ikiwemo makondo ya nyuma baada ya wajawazito kujifungua ambapo hata hivyo ameitupia lawama serikali ya kijiji cha Buganika iliyokuwa imepewa maelekezo ya kuchimba choo cha muda.

Kuhusu suala la wajawazito kutozwa fedha na kutakiwa kwenda na vifaa wanapokwenda kujifungua alisema ni mapungufu ya baadhi ya watumishi wasiozingatia maadili ya kazi yao kwa vile huduma za afya kwa wajawazito zinatolewa bure na kwamba mtumishi anayekwenda kinyume na maelekezo hayo anavunja sheria za kazi.

“Ni kweli zahanati hiyo haikuwa na choo tulikubaliana na serikali ya kijiji wachimbe choo cha muda pamoja na shimo la kutupia makondo ya nyuma wakati tukijiandaa kujenga choo cha kudumu pamoja na Placenta Pit ikiwemo kichomea taka, tayari fedha imeishapatikana hivi sasa tunatafuta mkandarasi kwa ajili ya ujenzi huo,” alieleza Dkt. Msaningu.

Hata hivyo alielezea kushangazwa kwake na hatua ya serikali ya kijiji cha Buganika kutotekeleza maelekezo waliyokuwa wamekubaliana kwamba badala kuifunga zahanati hiyo kwa kutokuwa na choo kijiji kijenge choo na shimo la muda la takataka wakati wakisubiri ujenzi wa kile cha kudumu.kwa vile ikifungwa watakaoathirika ni wanakijiji wenyewe.

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top