Unknown Unknown Author
Title: RIWAYA: SITAISAHAU FACEBOOK SEHEMU YA TATU
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
RIWAYA: SITAISAHAU facebook MTUNZI: EMMY JOHN Pearson SIMU: 0654 960040 SEHEMU YA TATU Mchomo wa wivu ukanishambulia na kunijeruhi moyoni,...

clip_image001

RIWAYA: SITAISAHAU facebook
MTUNZI: EMMY JOHN Pearson
SIMU: 0654 960040

SEHEMU YA TATU
Mchomo wa wivu ukanishambulia na kunijeruhi moyoni, nikaanza kuhisi zile ndoto zangu zimeanza kufifishwa. Happy alinisalimia akiwa na tabasamu mwanana. Dokta akiungana naye kutabasamu. Nami nikajilazimisha nikatabasamu!!!
“Kesho nitarejea nyumbani mara moja….kuna dharula imejitokeza. Lakini kitu kimoja nahitaji mfanikiwe kupitia mimi.” Alianza kutueleza dokta, tukiwa ndani ya gari la kukodi. Kisha akaendelea, “Nitarejea hivi punde tu!! Na nikiwa huko nitakuwa nawasaidia, msisite kunieleza lolote nami nitawasaidia, hata mimi kufika hapa nilikuwa nasaidiwa kwa hiyo ni zamu yangu kusaidia.” Aliongea kwa ukarimu mkubwa.
Kwa mahesabu ya harakaharaka zile dola thamani yake ilikuwa milioni sita za kitanzania. Hizo ndizo Dokta alituachia tugawane.
Kwangu mimi ilikuwa kama ndoto ya mchana!!!
Siku iliyofuata dokta huyu wa ajabu akarejea huko anapojua
yeye!! Hakutaka kusindikizwa uwanja wa ndege.
Ile hali ya kumshuhudia Happy akiwa na Dokta Davis ilinitia mashaka sana na kuhisi kwamba muda wowote ule nitanyang’anywa tonge mdomoni. Hivyo nikalazimika kuchukua tahadhari na kuanza kumpeleleza Happy kujua iwapo ana mawasiliano ya ukaribu na Davis ama ni wasiwasi wangu tu.
Niliamini kabisa Davis alikuwa ni mali yangu na si ya mtu mwingine, hivyo Happy kama alitaka kunizunguka basi alikuwa hanitendei haki hata kidogo. Na ulikuwa ni utovu wa nidhamu.
upelelezi wangu ukaanza kimya kimya!! Lakini kabla haujazaa matunda likatokea tukio jingine tena lililonisahaulisha juu ya upelelezi ule!!
Ilikuwa siku tulivu ya jumamosi nikiwa chumbani kwangu. Chumba ambacho kwa sasa kilikuwa na mabadiliko kidogo tofauti na awali, nilikuwa na luninga, spika kubwa na redio na pia nilifanikiwa kuweka kabati ndogo, Simu yangu iliita alikuwa ni dokta Davis akiwa amepiga na zile namba zake za kigeni!! Nikapokea.
Dokta alizungumza mengi huku kubwa zaidi akinigusia kuhusu biashara tuliyozungumza. Ni hapo ndipo nikaikumbuka biashara ya mtandao. Siku tulivyochat naye katika mtandao wa facebook huenda sikumuelewa vyema. Sasa alikuwa ananielewesha vyema ni jinsi gani mimi nitahusika katika biashara hiyo inayolipa mamilioni mengi kwa muda mfupi.
“Sasa hapo biashara hiyo inafanyikaje? Huo mtandao uko vipi?.” Nilimuuliza kwa utafiti. Kwani hakuwahi kunielekeza moja kwa moja juu ya biashara hiyo ya mtandao.
“Umeuliza swali hili wakati muafaka sana. Nilitaka kukueleza kuwa umependekezwa kuwa mwakilishi wetu katika nchi yako ya Tanzania. Hongera sana Isabela.” Aliniambia kwa furaha na kabla sijauliza chochote aliendelea, “Ni lini utapata walau siku nne za kuwa free uweze kunitembelea huku niweze kukupa maelekezo zaidi?”
“Wewe upo wapi??” Nilimuuliza.
“Lusaka Zambia, lakini tutakutana Ndola.”
“Ndola ndio wapi?.” Nilijawa na maswali mfululizo. Niliwahi kupasikia Ndola lakini sikujua ni wapi
“Mkoa mmoja hapahapa Zambia.”
“Kwa sasa nipo free sana. Hatujaanza kuwa bize.” Nilimjibu huku nikiwa nafurahia mazungumzo hayo ambayo yalikuwa yakimaanisha kuwa Isabela nilikuwa nimekaribia kuajiriwa!!
“Waweza kukimbia mara moja kuja huku ofisini kwetu kwa ajili ya kusaini mikataba?.” Aliniambia, nikacheka kimya kimya yaani yeye Zambia alipaona karibu sana eti ananiambia nikimbie mara moja. Makubwa!!
“Naweza ila…”
“Usijali mambo ya nauli na kila kitu kampuni yetu itakulipia. Kesho zitaingizwa kwenye akaunti yako.”
Ni hilo haswaa nilitaka kumuulizia na sasa alikuwa amenipa jibu tayari. Nilistaajabu, dokta alikuwa anaotea mambo ambayo nilikuwa nawaza!!!
Baada ya kukata simu ile nilitamani sasa kila mtu aitambue furaha yangu, nipo chuo mwaka wa pili napata kazi nje ya nchi, mshahara zaidi ya milioni mbili. Nani kama Isabella, mara nikamsahau Happy aliyekuwa anakisumbua kiichwa changu. Kama mimi nimechaguliwa ya nini kujihangaisha naye!!!
Nikafumba macho, nikatamani sana kumshirikisha mwalimu Nchimbi ambaye ni mama yangu mzazi lakini nikaona ni mapema sana, nikataka kumwambia Happy lakini nikahisi huyo alikuwa mpinzani wangu katika kumuwania Davis. Nikakaa kimya sikumwambia mtu yeyote. Nikaanza kuona masaa yakiwa hayaendi kabisa!! Nilitamani ifike hiyo siku ya kuondoka!!
Siku moja kabla ya kuondoka nilizungumza na kiongozi wa darasa letu Class Representative ‘CR’ kuhusu kazi zitakazokuwa zinatolewa darasani awe ananiandika kuwa nipo japo sitakuwepo, mwanzoni alinikatalia katakata na kudai hawezi kuwa muongo kiasi hicho na ni hatari kwa usalama wake hapo chuoni. Nilimtazama na nikamsihi sana lakini hakuonekana kushawishika!! Lni hapo ndipo nilipokumbuka kuwa pesa ndio kila kitu!! nilipotoa noti moja baada ya nyingine hadi zikafika noti kumi nyekundu alilainika na kugeuka kibaraka. Tena akawa mzungumzaji mkuu!! Pesa bwana!!
(SAFARI YA ZAMBIA)
Kesho yake asubuhi nilikuwa katika basi la kampuni ya Mohamed kuelekea jijini Dar es salaam kasha niunganishe kwenda jiji las Mbeya kabla ya kuikamilisha safari ya Zambia, Ndola. Kusaini mkataba!! Mkataba nisioufahamu!!
Nilijihisi kama malikia na lilikuwa kosa kubwa sana kujaribu kunifananisha na mwanafunzi yeyote wa chuo kikuu cha mtakatifu Augustino ambacho nilikuwa nasoma. Hata wale wa huko Dar pia hawakutakiwa kufananishwa na mimi Hakuna ambaye angeweza kukaa ngazi moja na mimi
kwa sababu wengi wao waliishi kwa kutegemea mkopo wa bodi yao hiyo, sasa mimi nilikuwa nina pesa yangu na kubwa zaidi nilikuwa naingia kazini. Hao watoa mikopo ningepata fursa ya kukutana nao nadhani ningekuwa na jeuri ya kuwashushua kwa tabia yao ya unyonyaji uliopitiliza. Na laity kama wangenibishia kwa lolote ningewashushia mvua ya matusi.
Isabela malikia!! Nilijipa jina hilo!!
Nikiwa safarini kuelekea Mbeya nikitokea jijini Dar es salaam baada ya safari ndefu kutoka Mwanza siku iliyopita, tulipofika Makambako nilianza kuifikiria familia yangu niliwaza kumjengea mama yangu nyumba ya kifahari kisha nimtoe baba yangu katika ulevi sugu kwa kumuwekea pombe za kisasa ndani. Hizo niliamini zitamnenepesha badala ya kumkondesha kama alivyokuwa kipindi hicho. Wadogo zangu waliokuwa wakisoma shule za kata nao nadhani walitakiwa kusoma shule zenye hadhi ya mshahara nitakaokuwa napokea dada yao. Tena wote nawapeleka shule za bweni!!! Nilijiapiza huku pua zangu zikinusa kwa mbali harufu nzuri ya sabuni ambayo nilitumia asubuhi kuoga katika hoteli ya kifahari jijini Dar es salaam.
Nilitoa tabasamu hafifu kisha nikaendelea kuuchapa usingizi.
Nilifika Mbeya mjini salama kabisa. Dereva teksi wa kwanza niliyekutana ndiye alipata bahati ya kuniendesha msichana ambaye nilikuwa na malengo makubwa kama mimi. Alitakiwa kujisifu kama angekuwa kichwani mwangu na kutambua mimi ni nani.
Alinifikisha hadi hoteli maridadi yenye hadhi ya kulaliwa na watoto wa vigogo na vigogo wenyewe. Nililipia na kulala hapo kesho yake mapema nikawa Tunduma halafu mwisho ikafuata safari ya Ndola. Hata ule uchovu haukusumbua mwili wangu nilitamani kuikanyaga ardhi ya Zambia na kasha kuusaini ule mkataba nianze kula pesa nyingi!!
Ndani ya basi tulilokuwa tumepanda walikuwepo watu mchanganyiko. Hakuna aliyekuwa na hadhi kama mimi niliamini hivyo. Yaani nilikuwa najisikia kuwa na uwezo hata wa kuamuru basi hilo lisimame na likasimama lakini sikufanya hivyo.
Majira ya saa kumi na moja jioni kwa mara ya kwanza katika maisha yangu nilikanyaga ardhi ya nchi tofauti na Tanzania. Isabella ndani ya Ndolla Zambia
Mwanzo wa safari ya kwenda Marekani!!! Nilijiwazia hivyo.
Nilitegemea kuhangaika sana baada ya kuwa nimeshuka pale kituoni. Lakini la!! Haikuwa hivyo. Nilipotelemka tu. Nilitumia dakika moja tu kushangaa wanawake wawili waliokuwa wamependezea katika mavazi yao ya suti walinipokea begi langu dogo huku wakinisalimia kwa nidhamu kubwa sana.
#Mamaa Isabela!!” waliniuliza ili kuthibitisha kama ni mimi!!
Niliwajibu kwa tabasamu kuwa ni mimi, sasa nilianza kuamini kuwa Dokta Davis atakuwa ni mtu mkubwa sana. tofauti na mwonekano wake wa awali.
Niliongozwa hadi katika gari aina ya Noah, nilitaka kuingia humo lakini nikaambiwa hilo ni kwa ajili ya mizigo. Nikacheka moyoni huku nikiwaza kuwa laiti kama ningepewa hilo gari. Chuo wangekoma!!
Mh!! Mzigo gani sasa?? Nilijiuliza. Hakuwepo wa kunijibu.
Mimi natamani gari nyie mnawekea mizigo!! Dharau hii!!
Baada ya hapo nikapelekwa katika gari jeusi la milango sita.
Hapo nikafunguliwa milango nikaingia ndani. Niliokutana nao mle ndani wote walikuwa na nyuso zilizong’aa tofauti na ule wa dokta Davis. Japo walikuwa weusi na sura zao zikitangaza roho flani hivi isiyokuwa na ukarimu sana lakini walitabasamu.
Naishi kama malikia nchi za watu?? Mwalimu Nchimbi natamani ungeyaona haya rest in peace umasikini!!!! Nilijitamba kichwani mwangu huku nikikaa vyema na kuzijibu salamu za watu pale ndani.
Safari ikaanza. Sikuwa naujua mji hata mmoja lakini safari nayo haikuwa fupi.
Nilitamani sana niulize kuwa pale ni wapi lakini ningeanza kumuuliza nani?? Hilo likawa swali. Laiti kama dokta angekuwepo hapo sawa.
Nikiwa bado nashanga shangaa hapa na pale mara mwendo ulipungua kisha honi ikapigwa. Geti likafunguliwa na watu waliovaa nguo nyeupe sana. Gari zikaanza kuingia, yetu ikiwa ya pili kuingia.
Tulipotaka kushuka milango ilifunguliwa na akina kaka wenye kila sababu za kuitwa watanashati na wanamazoezi. Nikazidi kuvimba kichwa kwa mema haya niliyokuwa natendewa katika nchi ya kigeni.
Nikiwa bado sijafungua kinywa kuzungumza tangu nijibu salamu garini, walinifuata akina dada watatu wakanielekeza kwa ishara za mikono niwafuate. Sikuwa na kipingamizi niliwafuata. tuliingia katika chumba kilichokuwa na mvuto hata kwa yule asiyejua ubora wa chumba. Lakini mimi nilikuwa naujua ubora nilitambua.
“You have to re-dress madame” (Unatakiwa ubadili mavazi yako).
Waliniambia kwa pamoja. Sauti zao tamu zilinikonga moyoni. Nikatabasamu!!
Wakanipa maelekezo na baada ya dakika kadhaa nilitoka mle ndani nami nikiwa nang’ara katika mavazi meupe sana.
Nilikuwa nimependeza sikuhitaji kumuuliza mtu.
Sasa tukarejea katika magari tena. Mi nilijua tumefika mwisho kumbe lile lilikuwa geti la kwanza tu.
Mwendo wa dakika tano tukashuka tena. Tukaingia geti jingine kubwa. Hapo tukatelemka na kuanza kutembea juu ya kapeti jekundu.
Red kapeti!!! Niliwaza. Nikafanya tabasamu.
Nikiwa juu ya lile kapeti nikajihisi kuwa na hadhi ya Rihanna, Beyonce ama Lady Gaga. Kisa tu nipo juu ya zulia jekundu.
Hapa kama ni kazi nimepata!! Nilijiaminisha. Kasha nikaikumbuka kampuni moja nchini Tanzania iliyowahi kuniita kasha kuniambia eti kuna kazi ya kutembeza vipodozi mtaani malipo kwa siku ni kutokana na bidhaa kiasi gani umeuza!!!
Wapuuzi kabisa wale, hivi walinionaje kwani mimi!! Nilatukana kimoyomoyo kwa lugha ya kiingereza.
Nilikuwa makini katika kulikanyaga lile zulia jekundu, sikutaka kuonekana mshamba katika hilo.
Nilijilazimisha kutembea mwendo wa kilimbwende wakati niliamini kuwa iwapo nitathubutu kuingia katika mashindano ya ulimbwende basi nitashika nafasi ya mwisho ama sitapata walau kigezo cha kusimama jukwaani kama mlimbwende. Maana nilikuwa cha ufupi na nilikuwa na dalili ya kuwa kibonge, chipsi za kukurupukia ziliniletea dalili zote za kitambi kichanga!!
.
Niliongozwa hadi katika chumba kikubwa sana, kila kitu pale ndani kilikuwa cheupe kasoro ngozi yangu ambayo ilifanya kama uchafu pale ndani. Sikujali!!!
“Utalala hapa ndani…na hawa watakuhudumia.” Nilipewa wakinamama wawili kwa ajili ya kunihudumia. Umri wao sidhani kama unatofauti sana na wa mwalimu Nchimbi yule mama yangu mzazi. Lakini matabasamu yao ni kama walikuwa na miaka kumi na nane.
Ungekuwa wewe ungejisikiaje. Mwenzako nilijisikia kama malkia.
Nilipata huduma zote za msingi, kahawa ya maziwa, wine, kasha wakaniwekea nyimbo za taratibu hadi nilipopitiwa na usingizi na kuamka siku iliyofuata. Baada ya kuwa nimeoga na kupewa nguo nyingine nyeupe tena nilikaribishwa kifungua kinywa.
Ilikuwa kufuru nyingine tena niliyoweza kuishuhudia. Meza ilikuwa imesheheni kila aia ya makorokoro. Kazi kwako mlaji kujihudumia. Kiaibuaibu nikajinyima kula nilivyovitamani nikala nilivyovizoea. Na ushamba pia ulichangia. Kuna vyakula sikuelewa kama vinaliwa kwa kijiko ama uma, harufu yake nzuri ikabaki kunisurubu. Nikaogopa kujaribu!!!
Majira ya saa tano asubuhi niliongozwa tena kuelekea katika ile gari ya milango sita. Nikaingia humo kwa namna ileile kama malkia. Safari yetu ikaishia katika sehemu nyingine ya kifahari. Sikuwa naielewa nchi ya Zambia hivyo sikujua lolote.
“Mukuba Hotels.” Hilo ndilo neno nililoweza kulisoma baada ya kuunyanyua uso wangu juu. Sikujua maana ya Mukuba. Lakini bila shaka zilikuwa lugha za huko kwao. Hii hoteli ama jumba la kifalme!! Nilijiuliza.
Tuliingia hadi ndani huku mimi nikiwa mfuata mkia nisiyejua lolote linaloendelea mbele. Baada ya kukatiza kona kadha wa kadha sasa tukakutana na mlango ulioandika kwa maandishi yenye rangi ya dhahabu!! Dr. Davis. Moyo wangu ukapiga kwa nguvu. Paa!!
Ina maana Davis anaishi hapa? Nilitamani kuuliza ila nikasita, hakika nilikuwa nimeshtuka sana!!
Nikiwa nasubiri ajitokeze mtu kwa ajili ya kubisha hodi ili tuweze kuingia ndani maana sikuona mahali pameandikwa ‘PULL/PUSH’ mara mlango ule wa vioo ulianza kufunguka wenyewe, tukaingia ndani.
Sasa tulikuwa watu watatu pekee!! Wale wawili baada ya kuingia ndani pamoja nami wakatoka nje. Bila kusema neno!!
Sasa nikabaki peke yangu.
Kiti cha kuzunguka kilichokuwa kimegeuziwa ukutani kikazungushwa taratibu. Vazi la suti likanisabahi, kisha uso ukanyanyuka.
“You are most welcome honorouble Isabela!!” Sauti ilizungumza. Kisha akatabasamu. Alikuwa anafanana na Davis lakini sikutaka kuamini. Labda ndugu yake au au au…
“Ndo mimi mbona unashangaa.” Aliniwahi. Ni kama alijua nilichokuwa nawaza. Alikuwa ni Davis. Sauti yake ilikuwa maridadi zaidi ya siku ya kwanza kukutana naye. Hapa sasa nikakiri kuwa mtu anaweza kuuficha utanashati ama urembo wake kutokana na mavazi dhaifu anayoyavaa!! Davis alikuwa amebadilika sana.
Nikachukua nafasi. Bila kusema lolote alibonyeza kitufe mara kikashuka mfano wa kitrei cha kuwekea vyombo.
“Unatumia kinywaji gani.” Aliniuliza mimi nikiwa bado nashangaa.
“Aaaah!! Chochote.” Nilijiumauma huku nikijilazimisha kucheka!!
Akabonyeza vitufe kadhaa, kikaondoka na kurejea tena baada ya dakika tano.
Maajabu ya nane ya dunia jamani!! Sikuwahi kuona kitu kama hiki katika maisha yangu!!. Kile kitrei kilikuwa na glasi mbili za juisi. Akatwaa moja akanipatia. Sijawahi kuona tangu nizaliwe!!
“Asante.” Nilimshukuru. Hakujibu.
Dokta Davis aliyekuja Tanzania hakufanana hata kidogo na huyu. Huyu alinuka pesa tena pesa nyingi.
“Karibu Ndolla Zambia, hii ni ofisi yangu ndogo ya huku, nyingine ipo Lusaka, Accra na kubwa zaidi ipo Washington.” Alinielezea kwa sauti iliyojaa ujivuni. Lakini alikuwa amechangamka!!
Nilikuwa makini kumsikiliza, huku nikiduwaa hiyo ofisi aliyoiita ndogo, hata pale chuoni kwetu Mwanza hakuna ofisi kubwa iliyoikaribia kwa muonekano!!
Sasa hii ni ofisi ndogo!! Je hiyo kubwa ya Washington ipoje!!
Isabela nikapatwa na matamanio ya kuendelea kuwa karibu zaidi na Davis, na kwa mara ya kwanza nikakiri kuwa iwapo Davis na kampuni yake wakitaka niachane na chuo ili niajiriwe nitaacha!! Wakitaka nihame nchi nikafanye nao kazi nitahama!!
Isabela mimi nilikuwa ninatamani mafanikio, umasikini mkubwa niliokulia, safari yangu ngumu kabisa kimasomo niliyopitia hadi kufika chuo kikuu, fedheha zote nilizozipata kisa tu sina pesa!!
Nilikumbwa na hasira ya mafanikio!!

***ISABELA ndani ya Ndolla Zambia, katika ofisi ndogo ya Davis….kila kitu ni kigeni kwake…..NINI KITAJIRI..
**DAVIS anajihusisha na nini?? Na huo Udokta ni udokta kweli???
##MAONI yako ni muhimu sana kwetu!!!...ukimaliza kuisoma bofya LIKE kuonyesha tupo pamoja pia….
ITAENDELEA….!!!!

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top