Unknown Unknown Author
Title: CHENGE: NIMEITWA KUHOJIWA ESCROW
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
Mbunge Andrew Chenge. Siku moja baada ya Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma kusema imewaita watuhumiwa tisa wa sakata la uchotwaji w...
Mbunge Andrew Chenge
Mbunge Andrew Chenge.

Siku moja baada ya Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma kusema imewaita watuhumiwa tisa wa sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow, mbunge wa Bariadi Mashariki (CCM), Andrew Chenge, amekiri kupokea barua ya wito wa kuhojiwa.

Chenge ambaye hadi anakumbwa na kashfa hiyo alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, alipoulizwa jana kama amepokea barua ya wito huo, alijibu kwa kifupi na bila kufafanua: “Nimepokea barua yangu tu.” Katika kashfa hiyo, Chenge alipata mgawo wa Sh. bilioni 1.6.

Kwa upande wake, mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja, alipoulizwa swali hilo alisema: “Sina la kusema kwa hilo.”

Ngeleja aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, alipata mgawo wa Sh. milioni 40.4.

Naye, aliyekuwa Waziri wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, alisema hajapokea barua ya wito huo.
Akizungumza kwa njia ya simu, Profesa Tibaijuka ambaye ni Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM), alisema hajapata wito wowote na kwamba hata bungeni hayupo.
“Mimi nimekuambia kwamba sijapata wito wowote, kwanza mimi naumwa na hata bungeni sipo, kama wameniita waulize wenyewe waliokuambia,” alisema Prof. Tibaijuka.

Awali kabla ya kutoa majibu hayo, alipopigiwa simu, Prof. Tibaijuka alipokea akasikiliza swali, badala ya kujibu alisema hasikii vizuri halafu yuko kwenye kikao, lakini sekunde chache alipopigiwa tena alipokea na kusema anaumwa na kwamba hajapokea barua ya wito.
Prof. Tibaijuka katika kashfa hiyo, alipata Sh. bilioni 1.6.

Katika kashfa hiyo, Baraza la Maadili limekusudia kuwahoji vigogo tisa kuanzia Februari 23, mwaka huu.

Mbali na watuhumiwa wa kashfa ya Escrow ambayo hadi sasa imesababisha kujiuzulu kwa mawaziri wawili, Prof. Tibaijuka na Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini), pia Baraza hilo limewaita kwa ajili ya kuwahoji Meya wa Manispaa ya Tabora na Mkuu Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo. Huyu alihojiwa tena mwaka jana.
Baraza hilo litatoa uamuzi wa ama wahusika hao kufikishwe mahakamani au la, kulingana na hatia watakazokutwa nazo.

Ofisa Habari wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Johanither Barongo, alisema juzi kwamba mahojiano hayo yatafanyika kwa muda wa wiki tatu na yataongozwa na Jaji mstaafu, Hamisi Msumi na wajumbe wengine wawili, Hilda Gondwe na Celina Wambura.

Barongo alisema Baraza hilo litafanyika katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam na litakuwa la wazi kumpa fursa mtu yeyote kushuhudia.Mbali na wabunge hao, Barongo alisema watuhumiwa wengine wa kashfa ya Escrow watakaohojiwa ni pamoja na majaji na wakurugenzi.
Watuhumiwa hao walipata mgawo kutoka kwa James Rwegamalira wa VIP Engineering and Marketing Limited zikiwa ni mgawo wa Tegeta Escrow.

Mbunge wa Lupa (CCM), Victor Mwambalaswa, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini alilazimishwa kujiuzulu kutokana na kamati yake kushindwa kuisimamia Wizara ya Nishati na Madini juu ya kashfa hiyo.

Viongozi wengine waliojipatia mgawo katika akaunti hiyo ni aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Dk. Enos Bukuku (Sh. milioni 161.7), majaji wawili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Profesa Eudes Ruhangisa (Sh. milioni 404.25), Jaji Aloysius Mujulizi (Sh. milioni 40.4) na Mkurugenzi wa Wakala wa Usajili na Ufilisi (Rita), Philip Saliboko (Sh. milioni 40.4).

Wengine ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emmanuel Ole Naiko (Sh. milioni 40.4), Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Lucy Appollo (Sh. milioni 80.8).
Ofisa Sheria Mkuu wa Tume hiyo, Filotheus Manula, alisema wao wamewafikisha watuhumiwa hao katika Baraza hilo kulingana na sheria ya maadili ya viongozi wa umma inavyosema.

Manula alisema Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1993, kifungu cha (8), kinasema kati ya adhabu ambazo viongozi wa umma wanaweza kuchukuliwa pale wanapobainika wamekiuka sheria za utumishi wa umma ni pamoja na kuonywa, kushushwa cheo na kusimamishwa kazi.

Nyingine alisema ni kufukuzwa kazi na kushauriwa kujiuzulu; na kwamba hatua nyinginezo ambao Baraza linaweza kuwachukulia baada ya kuwakuta na hatia ni kuwafikisha mahakamani.

Prof. Tibaijuka alifukuzwa kazi na Rais Jakaya Kikwete Desemba mwaka jana wakati Chenge alijiuzulu Uenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti.

Katika sakata hilo, wengine ambao hawahusiki katika shauri la Baraza hilo ambao walipata mgawo huo ni viongozi wa umma wastaafu ambao ni Daniel Yona ambaye alikuwa Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, (Sh. milioni 40.4) na Mbunge mstaafu wa Sumbawanga, Paul Kimiti (Sh. milioni 40.4).

Kadhalika, wengine ambao siyo watumishi wa umma waliohusika katika mgawo huo ni Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Katoliki la Dar es Salaam Eusebius Nzigilwa (Sh.milioni 40.4), Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini (Sh. milioni 80.8) pamoja na Padri Alphonce Twimannye Simon (Sh. milioni 40.4).

Aidha, vigogo hao wanahojiwa wakati tayari kuna maofisa kadhaa wa Serikali ambao wamepandishwa kizimbani kwa kuhusika kwenye sakata hilo.

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top